Habari za Punde

Mamlaka Kamili ni kumrejesha Sultan kuiongoza Zanzibar kwa mlango wa nyuma - Viongozi wa CCM


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                   27.9.2015
---

VIONGOZI wa CCM Zanzibar wameeleza kuwa hoja inayotolewa na chama cha CUF ya kutaka kuleta Mamlaka Kamili ni dhamira ya kumrejesha Sultan kuja kuiongoza Zanzibar kwa njia ya mlango wa nyuma.

Viongozi hao waliyasema hayo leo katika Mkutano wa  Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika katika uwanja wa Sun Rise, Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja uliohudhuria na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema kuwa CUF hawana hoja na kushangazwa na kauli inayotoa kuwa Zanzibar haina Mamlaka kamili wakati tayari Zanzibar inayo mamlaka Kamili ila nia ya chama hicho ni kurudisha uongozi wa Kifalme.

Alisema kuwa viongozi wa CUF wameishiwa hoja na hawana la kuwaambia wafuasi wao na hivi sasa wamekuwa wakitumia jina lake kwa kunokesha mikutano yao. "labda kwa kwa sababu mimi mweusi na siwezi kujifanya mweupe kama Jusa",alisema Balozi Seif.

"Kama mimi mweusi ndio alivyoniumba Mungu sasa na wale waliokuwa na vilema visivyoonekana inakuwaje",alisema Balozi na kueleza mwaka huu CUF wanaanguka  huku akisisitiza kuwa Serikali inatolewa kwa nguvu za kura.

Aidha, Balozi Seif Ali Idd, alisema kuwa CUF hawana ajenda na liliopo hivi sasa ni kubwabwaja na kuwaeleza wanaCCM kilichobaki ni kwenda kupiga kura tarehe 25 mwezi huu, na CCM kupata ushindi na kueleza kuwa CUF haina ubavu wa kuishinda CCM.

Balozi Seif alisema kuwa tayari chama cha CUF wanajua kuwa mara hii wanashindwa na  ndio maana wamekuwa wakipita kununua vitambulisho vya kupigia kura kwa wanaCCM.

Alieleza kuwa mikakati wanayopaka ya kufanya vurugu Oktoba 24, 25 na 26, tayari imeshajulikanwa na kutumia fursa hiyo kuwata wazee wa CUF wa Mkoa wa Kaskazini kutowaachia watoto wao kufanya vurugu na kusema kuwa vyombo vya dola havichezewi na kuwataka wasije wakailaumu Serikali na kutowaachia watoto wao kuingia mtegoni, wasije kufanya vuru, wala maandamano.

Alisema kuwa mambo mengi ya vurugu wanayokusudia kufanya CUF wanayajua na wana ushahidi nayo na huku akieleza kuwa ipo siku watayatoa. "Chokochoko kachokoe pweza...CCM haichokolewi iko imara na ukifanya mchezo itakushughulikia",alisema Balozi Seif.


Alisema kuwa Oktoba 25  mwaka huu ni siku ya ushindi wa CCM hivyo kila mmoja aende mapema kupiga kura na kuwahakikishia wananchi kuwa siku ya uchaguzi ulinzi wa kutosha utakuwepo kwa ajili yao na watalindwa wakati wote.

Nae Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha alisema kuwa Mamlaka kamili ya Zanzinar yalipatikanwa tokea mwaka 1964 chini ya Marehemu Mzee Abeid Karume na hakuna mtu yeyote wala kikundi chochote cha watu ambacho kina uwezo wa kufanya hivyo hivi leo.

Alisema kuwa wanachokusudia kukifanya chama hicho kwa kutaka Zanzibar iwe mwanachama wa Umoja wa Mataifa, iwe na safaru yake, Wizara yake ya mambo ya nje yake ni jambo la kushangazwa kwani taifa lolote duniani haliwezi kuwa na viti viwili katika umoja wa Mataifa wala haiwezekani kuwa na sarafu mbili wala Wizara mbili za Mambo ya nje ndani ya taifa moja.

Shamsi aliendelea kuwashangazwa na CUF kutaka kuanzisha Mamlaka kamili na kueleza kuwa  chama hicho na kile cha CHADEMA msiimamo wao unafanana lakini dhamira zinatofautiana kwani lengo lao ni kuvunja Muungano kwa kutumia lugha ya ulaghai.

Alisema kuwa dhamira ya CHADEMA ni kuwarubuni CUF ili kuwaunga mkono na kuwa na mgombea mmoja wa Jamhuri ya Muungano na la kusikitisha zaidi ni kuwa CHADEMA kimefanikiwa, kuvidhoofisha vyama vya CUF na NSSR MAGEUZI. Pia alieleza kuwa CCM itaendelea kuunga mkono sera ya Serikali mbili.

Alieleza kuwa CCM inaamini kuwa Sera ya Serikali mbili ndio yenye uwezo wa kuongoza serikali, na kusisitiza kuwa Sera ya Serikali tatu haina uwezo wa kuulinda Muungano wala kuyalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Kwa upande wa Muungano alisema kuwa Wazanzibari wamekuwa wakinufaika na Muungano na kueleza kuwa Tanzania Bara wapo Wazanzibari wanaopata huduma kadhaa za maisha ya mwanaadamu ikiwemo ardhi, maji safi na salama na huduma  nyenginezo bila ya bughudha.

Shamsi alishangazwa na wale wote wanaosema kuwa Muungano hauna maana na kueleza kuwa ipo haja ya kutafuta mada nyengine na sio hiyo.

Akieleza juu ya vitendo vinavyofanywa na viongozi wa CUF, alisema kuwa wapo wanachama na viongozi wanapita kwenye Majimbo kununua vitambulisho vya kupigia kura na kueleza kuwa Sheria ya uchaguzi inasema kuwa mwananchi yeyote wa Zanzibar aliesajiliwa kwenye Daftari, haijalishi kuwa shahada yake, imepotea ama imenunuliwa au imeibiwa, ana haki ya kupiga kura.

Hivyo aliiomba Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kila Mzanzibari mwenye Shahada na asie na shahada wakati jina lake limo kwenye Daftari la kupiga kura ipewe fursa hiyo.

Nae Bi Amina Salum Ali aliwataka wananchi wa Kaskaznini kutobabaishwa na maneno ya wapinzani huku akieleza miongoni mwa mafanikio yaliopatikana katika Mkoa huo ikiwa ni pamoja na uimarishwaji wa miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyengine za kijamii.

Aidha, aliendelea kueleza kufarajika kwake na mipango ya Dk. Shein ya kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Zanzibar inalima na kuzalisha mchele wake wenyewe.

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir ambaye pia ni mgombea Uwakilisgi Jimbo la Tumbatu,alisema kuwa WanaCCM wanasubiri siku ya tarehe 25 Oktoba mwaka huu kukirejesha madarakani chama hicho.

Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Haji Juma Haji, alisikitishwa na kauli za chama cha CUF zinazoelezwa katika mikutano yao kuwa Zanzibar itaongozwa na wale walioondoshwa mwaka 1964 pamoja na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali hiyo itaingia madarakani na wale wote waliochukuliwa mashamba yao wanawarudishiwa mashamba yao kwani yamechukuliwa kwa dhulma.

Alieleza kuwa wanaCCM wanaamini kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa huru, haki na amani, na kusema kuwa vitendo vinavyofanywa na CUF katika Mkoa huo hawaridhiki kwani wameanza kuchana picha za wagombea wa CCM na kuwataka vijana wa Mkoa wa Kaskazini wasikubali kutumiwa na CUF kufanya hivyo.

Alisisitiza kuwa Mkoa wa Kaskazini ushindi hauna mbadala, huku akishangazwa wale wanaoparamia miti na kuanza kuchana picha za wagombea wa  CCM"Waanaparamia miti kwaru kwaru utazani kima wanagombana na picha zisizosema waje kugombana na mimi Haji Juma nnosema',alisema  Haji.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

11 comments:

  1. msituletee ujinga wenu hapa, mshazowea kupitiwa mlango wa nyuma na Tanganyika sasa hivi hamsikii wala hamuoni, mara hii tutamtizama na huyo Maalim kama atawarejesha hao masultani ndo tutamjuwa kama mbaya, lakini nyinyi basi tena miaka yote hiyo hamna moja, utumbo mtupu musituletee siasa zenu za chuki hapa.

    ReplyDelete
  2. Nyinyi CCM hamutaki mamlaka kamili kwa sababu hamuwezi kujiongoza wenyewe ndio sababu kubwa, lini mulijiongoza kwani? siku zote munaongozwa na Tanganyika.

    ReplyDelete
  3. Mimi naona maelezo haya rasmi yanatokana Ikulu. Ikulu ni chombo cha serikali sio CCM. Inakuwaje CCM waweze kuitumia medium hii kwa kampeni. Jee hii ni sahihi. Hii ni haki kwa wapinzani wa Dr. Sheni?
    Kuweni waadilifu Ikulu katika kutimiza wajibu wenu.

    ReplyDelete
  4. Hongera Balozi wape vidonge vyao, wataisoma number. sultan harudi ng'o

    ReplyDelete
  5. Hongera Balozi wape vidonge vyao, wataisoma number. sultan harudi ng'o

    ReplyDelete
  6. Ama kweli ccm mmeshashindwa! Bora mnyamaze kimya kuliko huu utumbo wenu! Au ndio tonge inakaribia kukatika!

    ReplyDelete
  7. Ama kweli ccm mmeshindwa! Huu ni utumbo gani? Eleza sera zako nini utawapatia wazanzibari baada miaka 50 ambapo hukuweza kufanya lolote! Hiki ni kizazi kipya hakidanganyiki! Mnayo yale2 ya kale! Basi ya kale hayapo tena! Yatafutieni matumbo yenu tonge nyengine.

    ReplyDelete
  8. Ovyoo pumba tupu hamna sera WaZanzibari tumeamka sio wale wa utawala wa Nyerere sisi.....Halafu ikulu ya SMZ ndio imekuwa inaweka Press Relese ya Utumbo huu....musituletee ujinga wenu hapa hapa hii ZANZIBAR ni nchi ya WaZanzibari, Sio Nchi ya CCM hii...

    ReplyDelete
  9. Ujinga mtupu sultani gani atarudi Zanzibar kwa hali iliopo sasa aache kula tende zake aje kula ukoko wa meno

    ReplyDelete
  10. Press release ya ccm inatolewa na Ikulu? Huu ni upuuzi wa grade 1

    ReplyDelete
  11. Ukiangalia kwenye hii habari utaona kuna statements mbili ambazo zinapingana baina ya Balozi Seif na Shamsi Nahoda! Balozi Seif anasema

    "Alisema kuwa CUF hawana hoja na kushangazwa na kauli inayotoa kuwa Zanzibar haina Mamlaka kamili wakati tayari Zanzibar inayo mamlaka Kamili ila nia ya chama hicho ni kurudisha uongozi wa Kifalme." Na Shamsi Nahoda anasema "Alisema kuwa wanachokusudia kukifanya chama hicho kwa kutaka Zanzibar iwe mwanachama wa Umoja wa Mataifa, iwe na safaru yake, Wizara yake ya mambo ya nje yake ni jambo la kushangazwa kwani taifa lolote duniani haliwezi kuwa na viti viwili katika umoja wa Mataifa wala haiwezekani kuwa na sarafu mbili wala Wizara mbili za Mambo ya nje ndani ya taifa moja.
    Sasa tumsikilize yupo? ??? Contradiction! !!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.