Na Shemsia Khamis, PEMBA
MFANYAKAZI mmoja wa Kampuni ya ‘Rock Tronic’ kutoka Tanzania bara, inayotengeneza barabara ya Meli tano –Konde Kaskazini Pemba, Pita Mikael Msakati (39), amenusurika kufa baada ya kuunguwa mvuke wa lami wakati wanaiingiza katika gari.
Tukio hilo limetokea jana kwareni Vitongoji wilaya ya Chake chake majira ya saa 5:00 mchana, wakati majeruhi huyo akiwa na wenzake wanne wakifanya kazi hiyo.
Majeruhi huyo, alikumbwa na mkasa huo akiwa katika majukumu yake ya kazi, mara baada ya gari waliyokuwa wakijaza lami kujaa mkusanyiko wa gesi na kupasua paipu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja ya wafanya kazi hao Paulo Adam Mbano alisema, gari waliyokuwa wakijaza lami ilijaa gesi na ndipo ilipotoka nje na kumuathiri mwenzao.
Alisema, tatizo hilo limekuwa likijitokeza mara nyingi katika kazi hiyo, lakini jana lilikuwa kubwa na ndio kusababisha mfanyakazi mwenzao kuunguwa.
‘’Idadi yetu tulikuwa wanne, lakini mwenzetu Pita ndio ameunguwa sana na mwengine alipata majara kidogo na wawili walinusurika kabisa’’, alisema mfanyakazi.
Akuzungumza na mwandishi wa habri hizi, majeruhi wa tukio hilo alisema, alipokewa vizuri katika Hospitali ya Chake chake na kupatiwa matibabu ipasavyo na sasa anaendelea vizuri ukilinganisha na hapo awali.
Alisema, tukio kama hilo limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika kazi zao, lakini hii ni mara ya mwanzo kukumbwa na mkasa huo.
Akithibitisha kumpokea majeruhi huyo Daktari dhamana wa Hospitali ya Chake chake dk. Yussuf Hamad Idd alisema, alifikishwa hapo akiwa ameunguwa mikono, miguu, tumbo na sehemu ya kichwa.
‘’Tulimpatia matibabu kama ilivyo ada na hivi sasa yupo hospitali amelazwa anaendelea na matibabu na hali yake sio mbaya kama hapo awali’’, alieleza dk. Yussuf.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni hiyo Said Bakar alisema, Kampuni ina mpango wa kumsafirisha na kumpeleka Hospitali ya Machami iliopo mkoa wa Kilimanjaro Tanzania bara.
Afisa mdhamini Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano kisiwani Pemba Hamad Ahmed Baucha alisema, wamepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa, kwani mfanyakazi huyo ni miongoni mwa wataalamu wa mambo ya lami katika barabara hiyo.
Alisema, Wizara itashirikiana kwa kila hali, ili kuhakikisha majeruhi anapatiwa matibabu ipasavyo na kurejea katika hali yake ya uzima kama awali.
Hata hivyo, Mdhamini alisema ni vyema kwa vibarua wanaofanya kazi kama hizo, kuwa na nguo madhubuti sambamba na kuwa makini muda wote, ili kuepusha athari kama hizo.
Hili mi tukio la kwanza kwa mtu kuungua mvuke wa unaofanana na wa moto katika miaka ya hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment