Habari za Punde

Konda aliempiga mwanafunzi kufikishwa mahakamani

Na Shemsia Khamis, PEMBA

JESHI la Polisi mkoa wa kusini Pemba, linatarajia kumfikisha mahakamani wakati wowote konda wa gari ya abiria inayofanyakazi Chake –Vitongoji, Mohamed Amir (25), kwa tuhuma za kumdhalilisha mwanafunzi wa kike (20) wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji.
Kondakta huyo anadaiwa kuwa alimpiga mwanafunzi huyo akiwa abiria wake, baada ya kutofautiana kwa shilingi 100, ambapo mwanafunzi alikuwa na shilingi 200 wakati kondakta huyo akitaka apewe shilingi 300.
Kamanda wa Polisi mkoni humo, Juma Yussuf Ali aliliambia gezeti hili kuwa, awali Jeshi la polisi limekuwa likimuhojia kondakta huyo pamoja na abiria wake (mwanafunzi), ambapo baada ya upelelezi kukamilika ni kufikisha mahakamani.
Alisema kuwa alichokifanya kondakta huyo ni kinyume na sheria za usalama barabarani na hata sheria ya mwenendo wa jinai, hivyo kazi ya kumuhoji ikikamilika hatua itakayofuata ni kulifikisha jalada la kesi ya kwa Mkurugenzi wa mashitaka kwa hatua.


 “Konda kwa hili kama ni kweli, basi alipaswa kutumia ustaarabu wa hali ya juu, ili kuweza kuepusha migogoro kama hii bila ya sababu ya msingi’’, alisema Kamanda.
Hata hivyo alisema kesi kama za udhalilisha hazipaswi kufumbiwa macho na vyombo vya sheria, ndio maana watendaji wake wamekuwa wakifuatilia kwa karibu matendo ya aina hiyo ili kujenga heshima kwa mtu ndani taifa hili.
 Kwa upande wake, muathirika wa tukio hilo (20) alisema alikumbwa na mkasa huo, mara baada ya kumpa konda nauli shilingi 200 badala ya 300 aliotaka, na ndipo walipoanza kuzozana kwa maneno na kisha kumpa kichapo.
Alieleza, alipofika sehemu ya kuteremka gari wakati anakwenda chuoani, ndipo alipoanza kumpiga vibao na kisha kumchania nguo zake, kumuangusha chini na kupoteza fahamu, ambapo baadae kuondokta aliondoka mbio na gari yake.
“Nilichukuwa muda hapo, na baadae nikanyanyuka na kuamua kuelekea kituo cha Polisi Madungu, kwa ajili ya kuripoti mkasa huu ulionitokea’’, alisema mlalamikaji.
Alifahamisha, baada ya kufika kituoni na kueleza mkasa, ndipo alipokwenda chukuliwa konda huyo na Polisi na kusuluhishwa na kisha kupewa shilingi 80,000 na kuamua kuzikataa.
Mlezi wa mwanafunzi huyo, alisema waliamua kuzikataa fedha hizo, kutokana na kuwa haitokuwa adabu kwa konda huyo na wengine wenye tabia kama hiyo ya kudhalilisha abiria hasa wanafunzi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katibu wa Jumuiya ya usafirishaji mkoa mkoa wa kusini Pemba (PESTA), Hafidha Mbarouk Salum alisema wamepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa.
Alieleza, tayari wameshawaita wahusika wote wa tukio na endapo watathibitisha kosa, wataandika barua na kuipeleka wizara husika, kwa ajili ya kufanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kuwapokonya leseni ya gari na kufuta ruti ya njia.
Hata hivyo, aliwataka madereva na konda kuwa wastahamilivu muda wote wa kazi kutokana na kuwa wanafanyakazi na watu tofauti, ili kuweza kuepusha migogoro isiyoyalazima.
Hili ni tukio la kwanza kwa mwaka huu, kuripotia la mwanafunzi kupigwa na konda, baada ya kutokea kwa mzozano wa nauli akiwa anakwenda chuoni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.