Habari za Punde

Mwili wa Waziri Celine Kombani waagwa rasmi kwa heshima za kiserikali

 Viongozi Wakuu wa Serikali za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongoza Umma wa Watanzania katika kutoa heshima ya mwisho kwa Mwili wa Marehemu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Marehemu Celina Ompeshi Kombani Karimjee Jijini Dar es salaam.Wa kwanza kutoka kushoto kuelekea kulia ni Makamu wa Rais wa  SMT Dr. Moh’d Gharib Bilal, Mke wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Katibu Mkuu Kiongozi wa SMT Balozi Ombeni Sefue.
 Familia ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Marehemu Celina Ompeshi Kombani wakiwa katika majonzi makubwa wakati wa kuuaga rasmi Mwili wa Mpendwa wao Karimjee  Jijini Dar es salaam.

  Jeneza la Marehemu Waziri Celine Kombani likiwekwa juu ya jukwaa tayari kutoa nafasi kwa Viongozi wa Kiserikali, Vyama vya Siasa, Taasisi za Kijamii na wana familia kuuaga rasmi katika viwanja vya Karimjee Mjini Dar es salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha salamu za Pole za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa kuuaga Mwili wa Marehemu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Marehemu Celina Ompeshi Kombani Karimjee Jijini Dar es salaam.

Picha na –OMPR –ZNZ.


Na Othman Khamis Ame, OMPR

Mwili wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma Celine Ompesh Kombani aliyefariki Dunia Alhamisi iliyopita katika Hospitali ya  Andra Prash Apolo ya Nchini India umeagwa rasmi kwa Heshima zote za Kiserikali.

Marehemu Waziri Celine Ompesh Kombani  alianza kuumwa Tarehe 26 Agosti mwaka huu ambapo Tarehe Mosi Septemba alipelekwa Nchini India kwa matibabu zaidi na kugundulika kuwa  na maradhi ya Saratani ya Kongosho iliyoathjiri ini lake.

Heshima ya kuuaga rasmi Kiserikali Mwili wa Marehemu Celine  ulioletwa kutoka Nchini India Juzi Mchana na kupokelewa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, marafiki na wana familia zilifanyika katika viwanja vya Karimejee Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d  Gharib Bilal aliuongoza Umma wa Watanzania katika kuuaga mwili wa Marehemu Celine  Ompesh Kombani  ambao baadaye utapelekwa  shambani kwake Lukole Jimboni Ulanga Mkoani Morogoro kwa Mazishi.


Kwa Upande wa Zanzibar  maombolezo hayo yaliongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyeambatana pia na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi  pamoja na Wanasiasa.

Mh. Celina Ompesh Kombani alizaliwa Tarehe 19 Juni Mwaka 1959 katika Kijiji cha Kisewe Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro akiwa Mtoto wa Pili miongoni mwa  Watoto 16 wa Mzee Ompesh  Kombani.

Alianza kupata elimu yake ya Msingi kuanzia mwaka 1968 hadi mwaka 1974 katika Skuli ya Kwiro Mahenge na baadaye kuendelea na elimu ya Sekondari kuanzia mwaka 1975 hadi 1978 kwenye skuli ya Sekondari ya Kilakala Mkoani Morogoro.

Marehhemu Celine Ompesh Kombani aliendelea na masomo ya Kidato cha Tano hadi cha sita katika Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora akiunganisha na Elimu ya juu katika chuo cha Uongozi  wa fedha cha IDM Mzumbe na kupata Stashahada ya Uongozi na Utawala na baadaye Shahada ya Juu ya Uzamili katika Chuo hicho cha Uongozi wa Fedha IDM Mzumbe.

Mwaka 1985 Marehemu Celine Ompesh Kombani aliajiriwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro  akiwa Afisa Utumishi  nafasi iliyomuwezesha kupanda Madaraka na kuteuliwa kuwa Meneja wa Rasilimali Watu katika Kiwanda kilichopo Morogoro.

Katika uhai wake Marehemu Celine aliwahi kuwa Afisa Utawala wa Chuo cha Kilimo Morogoro, Kiongozi wa Halaiki ya Vijana wa Chipukizi wa Chama cha TANU, Mwenyekiti wa Tawi la CCM Kilosa pamoja na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Morogoro.

Katika nyanja ya Kisiasa Marehemu Celine Ompesh Kombani alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ulanga kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 nafasi iliyomuwezesha kuteuliwa kushika nyadhifa mbali mbali za juu za Uongozi Serikalini.

Marehemu Celine aliwahi kuwa Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Katiba na Sheria   pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma nafasi aliyodumu nayo hadi kufariki kwake.

Wakitoa salamu za maombolezo ya Makundi mbali mbali, Wawakilishi wa Makundi hayo ikiwemo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bunge la Jamuhuri ya Muungano  wa Tanzania, Taasisi za Kijamii walimuelezea Marehemu Celine Ompesh Kombani kuwa alikuwa Mtu wa Watu.

Walisema Marehemu Celine alikuwa Kiongozi mahiri aliyekubali na kuridhia kuwa karibu na Taasisi na Watu wa makundi ya aina yote bila ya kujali itikadi, jinsia au Dini ya mtu.

Mapema akiongoza sala maalum ya kumuombea safari njema Marehemu Celine Ompesh Kombani Mchungaji Wilfred Mmary alisema Muungu muweza na asili ya kila kitu amekausha  pumzi ya Mpendwa Celine akifanya hivyo bila kosa bali  ni kutekeleza utukufu wake kwa viumbe vilivyo chini ya himaya yake.

Mbele ninaendelea nnazidi kutembea. Maombi uyasikie. Bwana umpambe. Ebwana  uniinue ili nipande milima yote.  Ni shairi alilolikariri mchungaji Wilfred ambalo alisema lilikuwa likiimbwa  na kumjumuisha Pia Marehemu Celine  wakati wa Ibada zao za misa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania { NEC } kupitia Mkurugenzi wake Bwana Kailina Ramadhan imeahirisha uchaguzi wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro kufuatia Kifo cha Waziri Celine  Ompesh Kombani aliyekuwa miongoni mwa wagombea nafasi ya Ubunge  wa Jimbo la Ulanga kupitia chama Tawala Cha CCM.

Marehemu Waziri Celina Ompesh Kombani ameacha Mume, Watoto Watano pamoja na Wajukuu Wanne. Muungu iweke roho ya Marehemu Celine  Ompesh Kombani mahali anapostahiki kwa mujibu wa amali yake. Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.