Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea taarifa za kuwepo Mahujaji wawili kutoka Tanzania ambao wamelazwa katika mojawapo ya hospitali nchini Saudi Arabia baada ya kujeruhiwa kutokana na tukio la mkanyagano wa Mahujaji lililotokea eneo la Mina, Makkah, tarehe 24 Septemba, 2015.
Mahujaji hao ambao wanaendelea kupata matibabu na hali zao zikiendelea vizuri ni Bi. Hidaya Mchomvu naBi. Mahjabin Taslim Khan.
Pia kwa mujibu wa taarifa za Ubalozi Hujaji mwingine anayejulikana kwa jina la Mustafa Ali Mchira amelazwa katika Hospitali ya Ansari Madina katika chumba cha wagonjwa mahututi. Taarifa zinaeleza kuwa Bw. Mchira alipata ugonjwa tangu alipowasili Saudi Arabia na hivyo ugonjwa wake hauhusiani na ajali iliyotokea tarehe 24 Septemba, 2015.
Vilevile, Serikali ya Saudi Arabia imeanza kutoa taarifa za alama za vidole za Mahujaji waliopata ajali. Hivyo, Ubalozi unazipitia na kuzihakiki taarifa hizo ambazo zitasaidia kuwabaini Mahujaji wetu waliokufa katika ajali hiyo.
Kutambulika kwa Mahujaji hao waliolazwa, kunatokana na jitihada zilizofanywa na Ubalozi kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na Vikundi vya Mahujaji za kutembelea Hospitali zote zilizopo Makkah, Mina, Arafat, Muzdalifa, Jeddah na Taif kwa ajili ya kuwatafuta Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia au kulazwa katika hospitali hizo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam.
01 Oktoba, 2015
No comments:
Post a Comment