DK. SHEIN: NICHAGUENI TENA TUENDELEE KUSHIRIKIANA KWA
KUONGEZA KASI YA KUIJENGA ZANZIBAR
Mgombea
wa nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein amewataka wananchi kumpa tena fursa ya kuongoza ili waendelee
kushirikiana kuijenga Zanzibar.
Amesema
katika kipindi cha miaka mitano kinachomalizika sasa Zanzibar imepiga hatua
kubwa kimaendeleo kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
hivyo kumchagua tena yeye na chama chake kuongoza ni fursa nyingine kwa
wananchi wa Zanzibar kuendeleza kasi ya maendeleo ya nchi yao.
Katika
mkutano wa kampeni uliofanyika huko Paje katika jimbo la uchaguzi la Paje,Mkoa
wa Kusini Unguja, mgombea huyo wa CCM aliueleza umati mkubwa wa wananchi ambao
haujawahi kutokea kuwa ahadi alizozitoa kwa jimbo hilo katika mkutano wa
kampeni kama huo mwaka 2010 zimetekelezwa na kuahidi kuongeza kasi ya
utekelezaji wa Ilani mpya ya chama hicho ya mwaka 2015-2020.
“Tumetekeleza
Ilani yetu kama tulivyopanga katika sekta ya afya, elimu, maji, umeme na sekta
ya utalii”na kuongeza kuwa kwa sekta ya barabara utekelezaji umeanza na
utakamilishwa katika kipindi kijacho.
Alifafanua
kuwa baada ya kukamilisha kuifanya hospitali ya Makunduchi kuwa ya wilaya,
Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya katika mkoa huo kwa kuiimarisha
hospitali ya Kivunge na kituo cha afya cha Paje kwa kivipatia vifaa na
wataalamu wa afya.
“Kazi
ya kuipandisha hospitali ya Makunduchi kuwa ya wilaya imekamilika kwa kuiwekea
vifaa vipya na kuwapatia madaktari wakiwemo kutoka nje ya nchi na tunatarajia
kuongeza majengo mengine mapya kuiwezesha hospitali hiyo kuwahudumia watu wengi
zaidi” alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa hivi sasa hata wananchi wa mjini
wanafika katika hospitali hiyo kufuata huduma.
Aliongeza
kuwa Serikali hivi karibuni ilifungua kituo kipya cha afya huko Kajengwa
Makunduchi ikiwa ni sehemu utekelezaji wa mpango wa Serikali wa uimarishaji wa
huduma za afya nchini.
Dk.
Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa katika kipindi kijacho Serikali itajenga
dakhalia katika skuli ya sekondari Paje Mtule ambayo ni skuli mpya ya kisasa
ambayo imejengwa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2010 -2015 ya
kuimarisha elimu nchini.
Katika
kuendelea kuimarisha elimu, Dk. Shein ameahidi katika kipindi cha miaka mitano
ijayo kuzipatia skuli zote za sekondari kompyuta ili ziweze kwenda na
mabadiliko ya sayansi na tekinolojia.
Kuhusu
ahadi ya kusambaza umeme vijijini, Dk. Shein alieleza kuwa utekelezaji wake umezidi asilimia mia na kwa
upande wa Paje ni maeneo machache yaliyobaki na kuahidi kukamilishwa muda mfupi
ujao baada Shirika la Umeme
Zanzibar (ZECO) kwa kuweka transfoma mpya.
Mgombea
huyo wa CCM anatarajiwa kwenda Pemba kuendelea na kampeni zake kesho.
No comments:
Post a Comment