STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29 Septemba, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Mgombea
Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema
suala la mafuta kutolewa katika mambo ya muungano ni matokeo ya jitihada za
pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na viongozi wake hivyo asitokee mtu au chama kikalitumia suala
hilo kama lake binafsi.
“Hakuna
haja ya mbwembwe wala kujisifu wote katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano tulishirikiana na kushauriana pamoja kwa muda
mrefu hadi kufikia hatua ya kupitisha sheria ya mafuta katika kikao cha Bunge
cha mwezi Julai 2015” Dk. Shein alisema.
Akizungumza
katika mkutano wa kampeni huko Paje leo katika jimbo la uchaguzi la Paje, Mkoa
wa Kusini Unguja, Dk. Shein amesema wako baadhi ya wanasiasa Zanzibar
wanalitumia suala hilo kama mtaji wa kisiasa kwa kuwaeleza wananchi kuwa hatua
iliyofikia sasa ni jitihada zao binafsi.
Katika
mkutano huo ambao ulivunja rekodi za mahudhurio tangu kufanyika mkutano wa
uzinduzi wa kamepeni, Dk. Shein amesema suala hilo limekuwa likipotoshwa kwa
makusudi kwa manufaa ya kisiasa hasa wakati huu wa kampeni.
“ningewaelewa
wenzangu hawa kama wangewaeleza wananchi kuwa hatua iliyofikiwa ni jitihada za
serikali yetu ambao wao ni washirika katika serikali lakini kusema wao ndio
waliofanikisha jambo hili inasikitisha na si jambo la kiungwana” Dk. Shein
alieleza na kuongeza kuwa kama ni sifa angeweza kujisifu yeye kwani ndie
aliyekuwa msimamizi mkuu pamoja na Rais Kikwete.
Alisema
yeye amefanya ziara katika nchi za Uholanzi na Ras El Khaima ambako alifanya
mazungumzo na kutia saini makubaliano ya awali ya ushirikiano katika kuendeleza
sekta hiyo pamoja na kufanya mazungumzo na makampuni mengi yenye azma ya kuja
kushiriki katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi.
Dk.
Shein alibainisha kuwa baada ya kuwepo makampuni ya kutafuta mafuta Tanzania
mwaka 2002 wakati huo akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alimtuma aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati huo Edgar Maokola Majogo kuzungumza
na Waziri mwenzake wa Zanzibar wakati huo Burhan Saadat kuhusu suala hilo
uchimbaji wa mafuta.
“Majibu
ya mashauriano hayo yalikuwa ni kuwa suala hilo lisiharakishwe kwa kuwa
linahitaji mashauriano zaidi” Dk. Shein alisimulia na ndipo mazungumzo
yalipoanza.
Mgombea
huyo wa CCM aliwaeleza wananchi kuwa
jitihada za kuliondoa suala la mafuta
katika mambo ya muungano lilijadiliwa katika Bunge la Katiba lakini baada ya
kuwa mchakato huo haukukamilika yeye na Rais wa Jamhuri ya Muungano
walilipeleka suala hilo kwa wanasheria wakuu ili kutumia bunge kulikamilisha na
ndivyo lilivyofanyika.
“Ilikuwa
ni busara yetu viongozi kulipelekea suala hili kwa wanasheria wetu wakuu baadae
tukalijadili katika vikao vyetu hadi sheria kupitishwa bungeni” Dk. Shein
alisisitiza.
Hata
hivyo aliongeza kuwa ni jambo la kushangaza watu hao wanaojinasibu kuwa
wamefanikisha suala hilo ndio hao hao waliopinga suala hilo na kukimbia bungeni
wakati sheria ya mafuta ilipokuwa ikipitishwa.
Akibainisha
zaidi Dk. Shein kuwa wakati hayo yakiendelea huku Serikali ya Zanzibar ilikuwa
ikitayarisha sera yake na kudokeza kuwa imekamilika pamoja na kwamba rasimu ya
sheria iko tayari ikisubiri kupitishwa katika Baraza la Wawakilishi ili kazi ya
kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ianze kwa kasi.
Aliwataka
wananchi wasihadaike na maneno ya viongozi hao kuwa uchimbaji huo utaanza mara
moja na kuwatahadharisha kuwa hadi kuyachimba mafuta itachukua sio chini ya
miaka mitano.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015,
Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment