Habari za Punde

360 wafariki kwa ajali za barabarani Zanzibar: Ripoti za haki za binadamu

Na Haji Nassor, Pemba
WATU 360 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na ajali 4,291 za barabarani, zilizotokea Unguja na Pemba, kuanzia kipindi cha mwaka 2008 hadi mwezi disemba mwaka 2014.
Kwa mujibu wa ripoti za haki za binadamu za miaka saba iliopita, zinaonyesha kuwa, katika kipindi hicho watu wengine 3,195 walijeruhiwa baada ya kutokezea ajali hizo.
Ripoti hizio zinazotayarishwa kila mwaka na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), zinaonyesha kuwa kila mwaka, matukio ya vifo vya ajali barabarani yanaongezeka.
Ripoti ya mwaka 2008 imeonyesha kuwa, jumla ya watu 48 walipoteza maisha na 409 walijeruhiwa baada ya kutokezea ajli za barabarani, ambapo mwaka uliofuata (2009), iliongezeka watu sita (6) na kufikia 54, ingawa mwaka 2010, kulipungua watu wawili wawili sawa na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na watu 50 waliofariki.
Aidha taarifa za ripoti hizo za haki za binadamu, zinaonyesha mwaka mwengine uliowaacha wazanzibari na simanzi kubwa ni 2011, baada ya kuripotiwa idadi hiyo, na 440 kujeruhiwa, ingawa miaka miwili iliofuta kulipungua na kuwepo watu 39 na 29 kwa mwaka 2013, huku mwaka 2014 ikipanda mara dufu na kufikia 88, sawa na majeruhi 547.
Zanzibar ambayo kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012, inaidadi ya watu 1,303,569 ambapo kutokana na watu 360 waliopoteza maisha pekee kwa sababu za barabarani kwa kipindi cha miaka saba iliopita, ni sawa na kwamba mwaka mmoja kulikua na jali moja kila siku.

Aidha kutokana na idadi hiyo ya vifo, nazo ajali 4,291 za barabarani ziliripotiwa kwenye ripoti hizo, kuanzia kipindi cha miaka saba iliopita, na mwaka jana ndio kulikoripotiwa ajali nyingi, kwa kufikia 845, huku mwaka 2010 zikifikia 692.
Mwaka mwengine ulioripotiwa ajali nyingi za barabarani ni 2011 kwa kuripotiwa 615, ukifuatiwa na mwaka 2009 ajali 583, wakati mwaka 2008 zikijumuishwa ajali 536, ikikaribiana na mwaka 2013 kulikoripitiwa ajali 534 na majeruhi 503 wa Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, chanzo cha kujitokeza kwa ajali hizo ni kuwepo kwa mchanganyiko wa matumizi ya barabara, baina watembea kwa miguu, waendesha vyombo vya magurudumu mawili na gari za kawaida.
Sababu nyengine ni ubovu na uchakavu wa barabara katika maeneo kadhaa ya Zanzibar, uwembamba wa barabara zenyewe, sheria za usalama barabarani kutochukua nafasi yake na kukosekana kwa usalama mzuri sambamba na uendeshaji wa uzembe.
Dereva wa gari Chake chake-Mkoani Juma Mohamed ‘J’ alisema yeye anaona sababu kubwa na ufinyu wa barabara ambao hauhimili tena ongezeko la vyombo vya moto kisiwani Pemba.
Nae Ali Mjaka Hashim, alisema inawezekana pia harufu ya rushwa iliopo kwa baadhi ya wasimamizi wa sheria barabarani ndio zinazotoa fursa kwa madereva kuendesha mwendo kasi ambapo hata akisababisha ajali hana hakika ya kuadhibiwa.
“Madereva hawafungwi na wala hawana adhabu kali wanapofanya makosa ya barabarani hata kama wamesababisha kifo, ndio maana ongezeko la ajali na vifo lipo’’,alifafanua.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wameshauri kuendelea kutolewa kwa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha vyombo vya moto na watembea kwa miguu ili kupunguza ajali zisizokuwa za lazima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.