STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
1.12.2015

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametembelea mradi wa
maji Makunduchi na kuwataka wananchi wa kijiji hicho kuendelea kuiamini
Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuukamilisha mradi
huo na kuwapatia huduma ya uhakika ya maji safi na salama katika kipindi kifupi
kijacho.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi waliofika katika eneo la
Mradi huo huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, mara baada ya kutembelea mradi wa ubadilishaji wa tangi pamoja na
kisima kipya kilichochimbwa katika eneo hilo la Mradi.
Katika maelezo yake
Dk. Shein aliwaeleza wananchi waliohudhuria tukio hilo kuwa Serikali yao ya
Mapinduzi ya Zanzibar ipo na inaendelea na kazi za kuwahudumia wananchi wote na
kusisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa
kupatikana huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.
Dk. Shein alisema kuwa
mradi huo unaotarajiwa kuzinduliwa katika sherehe za Mapinduzi utaweza kuongeza
upatikanaji wa maji safi na salama na kuwaondoshea kabisa tatizo la huduma ya
maji safi na salama wananchi wa maeneo hayo.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa visima vitatu ambavyo vitapeleka maji katika tangi hilo kubwa
lililobadilishwa kikiwemo kisima kipya kiliopo karibu ya tangi hilo ambacho
kinatarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja ijayo, kisima kilichochimbwa kupitia
mradi wa Ras el Khaimah na kile kilichochimbwa Mnywambiji huko Kibuteni
vikiunganishwa kwa pamoja vitatoa maji ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya
wananchi.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa wafanyakazi na uongozi wa Mamlaka
ya Maji Zanzibar, (ZAWA) pamoja na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati,
viongozi wa Jimbo na wananchi wote
waliounga mkono na kuonesha ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo ili
kuhakikisha unakamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe.
Ramadhan Abdalla Shaaban alisisitiza kuwa si muda mrefu wananchi wa maeneo hayo
watafaidika na huduma ya maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi huo
wa maji Makunduchi.
Waziri Shaaban alibainisha
kuwa kazi ya ulazaji wa mabomba kutoka
kisima kipya cha pango la Mnywambiji kilichochimbwa huko Kibuteni nayo
iko mbioni kumalizika ambapo kwa hivi sasa imebaki sehemu ndogo tu ya kuvuga
barabara ya Makunduchi na kuingia tangini.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji
wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Dk. Mustafa Ali Garu alisema kuwa visima
hivyo vitatu vitakapokamilika vitaweza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa
asilimia zaidi ya 90 kwa wananchi wa Makunduchi.
Alifafanua kuwa kisima
cha Makunduchi kitaanza kutoa maji wiki ijayo wakati kile cha Kibuteni kitaanza
kutoa maji baada ya kukamilika uwekaji wa umeme wa jua hivi karibuni.
Alisema kuwa Mradi huo
umeweza kutekelezwa kwa mashirikiano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Uongozi wa Jimbo, Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation pamoja na wananchi.
Mkurugenzi Garu
alisema kuwa mradi huo umeweza kupitia katika miongo mbali mbali ambao
uliansihwa katika miaka ya 1960 kwa msaada kutoka Serikali ya Watu wa China na
mnamo mwaka 2000 ukaimarishwa zaidi kwa kuwekwa tangi la sandarusi ambapo awamu
hii limejengwa tangi jipya la chuma.
Alieleza kuwa tayari
kazi za uwekaji wa tangi hilo jipya zimeshafanywa na hivi sasa imeshakamilika
na limeanza kutumika kwa kutiwa maji ambayo husambazwa kwa wananchi.
Dk. Garu alisema kuwa
kukamilika kwa mradi huo baada ya kukamilika kwa visima hivyo vitatu kutasaidia
kutoa zaidi ya lita laki moja ambazo zitasambazwa na kuwasaidia wananchi wa
Makunduchi na kulifanya tatizo la maji kuwa historia kijijini hapo.
Sambamba na hayo, Garu
alifafanua kuwa kisima hicho pia, kitapeka huduma hiyo ya maji kwa wananchi wa
Mtende.
Nao wananchi wa
Makunduchi walitoa salamu zao za shukurani na pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kuendeleza juhudi za kuwapelekea
huduma muhimu za kimaendeleo, kijamii na kiuchumi katika vijiji vyao huku
wakiahidi kuendelea kumuunga mkono.
Akitoa salamu hizo za
shukurani Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dk. Idriss Muslim Hija alieleza kuwa
kuna kila sababu za kuendelea kuungwa mkono juhudi hizo za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wa Makunduchi wanatoa shukurani za dhati kwa
juhudi zinazofanywa na Serikali yao.
Viongozi mbali mbali
wakiwemo Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wananchi pamoja na viongozi
wa vyama vya siasa walihudhuria katika ziara hiyo.
Rajab Mkasaba.
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment