Habari za Punde

Mashamba 7000 yatambuliwa Pemba, hakuna aliepewa hati

Na Haji Nassor, Pemba
WANANCHI wanaomilika mashamba 7003, katika shehia tisa za wilaya nne Kisiwani Pemba zilizoanza kwa majiribio, tayari zimeshakamilisha zoezi la utambuzi wa ardhi, na sasa wanaendelea na hatua nyengine za kisheria, ili wakabidhiwe hati za umiliki.
Zoezi hili lililoanza mwaka 2012, lengo lake ni kuhakikisha kuwa kila mmiliki wa ardhi, anapatiwa hati maalum ya umiliki ambayo pamoja na mambo mengine, itamuwezesha kuikodisha baada ya kuingizwa kwenye daftari maalumu.
Kwa wilaya ya Chakechake, tayari wananchi wenye mashamba 2,467 yameshatambuliwa, ambapo wilaya ya Mkoani kuna mashamba 2,231 na wilaya ya Wete kwenye shehia tatu kama wilaya nyengine, kuna mashamba 2,305 yaliokwisha tambuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya ardhi na usajili kisiwani Pemba, shehia ambayo wananchi wake wamehamasika na kujitokeza kwa wingi ni Selemu wilaya Wete, ambapo kuna mashamba ya wananchi 1000.
Shehia nyengine inayoongoza kwa wamiliki wa mashamba hayo kukubali kujitokeza na kisha mahsamba yao kutambuliwa ni Chokocho wilaya ya Mkoani, kuna mashamba 997, ikifuatiwa kwa karibu na shehia ya Mkoroshoni yenye mashamba 950.

Aidha taarifa hiyo ikafafanua kuwa, shehia nyengine ambazo mashamba yameshatambuliwa ni Uweleni 726, Ngombeni 508, Kipangani 615, Msingini Chake chake 590 na Wara wilaya ya Chakechake mashamba ya wananchi 927.
Mohamed Salim Afisa Mtambuzi wa Ardhi Pemba, alisema zoezi hilo ambalo ni kwa shehia zote za Pemba, kwanza zoezi hilo limeanza kwa kutimiza masharti ya sheria namba 10 ya mwaka 1990 inayozungumzia usajili wa ardhi.
Amewatoa hofu wananchi kwamba zoezi hilo, wala halina lengo hapo baadae, kwamba wananchi watatozwa kodi kupitia ardhi zao kama wengine wanavyofikiria.
Aidha Afisa huyo, alifahamisha kuwa wananchi wala wasiwe na hofu na wasiwasi kwamba ardhi zao watapokonywa na serikali, bali hapo baadae ni kukabidhiwa hati za umiliki ambazo zitawawezesha kuwa na uhakika wa umiliki.
“Mwisho wa zoezi hili ni kuhakikisha kila mwananchi anapewa hati ya umiliki, maana itakuwa ardhi yake sasa inatumbulika na anaweza kuitumia hata kuombea mikopo na kuikodisha’’,alifafanua.
Kuhusu kwamba wananchi wameshakabidhiwa hati za umilikiwa wa ardhi au laa, Mkuu wa Idara ya Ardhi Pemba Rashid Suleiman, hakuwa na jawabu rasmi la kumuelezwa mwandishi wetu.
“Ngoja maana mimi sijui kwamba kuna wananchi wameshapewa hati au la, maana huyu mkuu wa kitengo hayupo na mini sina taarifa zozote”,alisema.
 “Zoezi hili ni la kisheria na linataratibu zake hivyo lazima wakati ukifika wananchi hawa ambao tayari mashamba yao wameshatambuliwa watakabidhiwa hati, lakini sijui kwamba washaopewa au laa’’,alifafanua Mkuu huyo.
Kwa mujibu wa sheria, ili ardhi iweze kusajiliwa lazima iwe na vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuthibitisha, kuridhia na kusajiliwa (approval/registration).
Kigezo chengine ni kutangaazwa kwa eneo litakalofanyiwa zoezi la usajili na Afisa Mtambuzi wa ardhi, kufanyika kwa uhamasishaji wa eneo lililotangaazwa kufanyiwa usajili pamoja na kukusanywa malalamiko kutoka kwa wamiliki wa ardhi , nyumba (claim collection).
Baadhi ya wananchi hao ambao tayari mashamba yao yameshatubuliwa kisheria, waliomba Idara husika kuharakisha upatikanaji wa hati za umiliki.
Wamesema  imekuwa ikuchukua muda mrefu, kutoka kumalizika kwa zoezi la utambuzi hadi kufikia kupewa hati, jambo wakati mwengine huwapa wasiwasi.
Aidha wananchi ambao shehia zao hawajfikiwa na zoezi hilo, wa shehia ya Wawi wamesema huwenda zoezi hilo likasababisha wasiowamiliki rasmi wa mashamba wakajulikana .
Ali Haji Massoud, alisema katika miaka ya hivi karibuni kumejitokeza migogoroa kadhaa ya ardhi ya ndugu, ambapo anaamini zoezi hilo litasaidia kupunguza.

Zoezi la utambuzi wa ardhi na kisha wananchi kupewa hati maalumu za umiliki baada ya kuingizwa kwenye daftari maalumu, kwa sasa limeanza katika shehia tisa kwa majiaribio kutoka wilaya za Chake chake, Mkoani an Wete.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.