HUTUBA YA
RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA
MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA
MAADHIMISHO
YA SHEREHE ZA MIAKA 52 YA
MAPINDUZI
YA ZANZIBAR, AMAAN STADIUM
TAREHE 12
JANUARI, 2016
Mheshimiwa Dk. John
Pombe Magufuli;
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,
Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan;
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Majaliwa
Kassim Majaliwa;
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Maalim
Seif Sharif Hamad;
Makamu wa Kwanza wa
Rais, Zanzibar,
Mheshimiwa Balozi
Seif Ali Iddi;
Makamu wa Pili wa
Rais, Zanzibar,
Mheshimiwa Mzee Ali
Hassan Mwinyi;
Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Benjamin
William Mkapa,
Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete;
Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dk.
Salmin Amour Juma;
Rais Mstaafu wa
Zanzibar,
Mheshimiwa Dk. Amani
Abeid Karume;
Rais Mstaafu wa
Zanzibar,
Waheshimiwa Mawaziri
wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar,
Mheshimiwa Job
Ndugai;
Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Pandu
Ameir Kificho;
Spika wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar,
Mheshimiwa Othman
Chande Mohamed;
Jaji Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Omar
Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa
Zanzibar,
Waheshimiwa Mabalozi
na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,
Mheshimiwa Abdalla
Mwinyi Khamis;
Mkuu wa Mkoa wa
Mjini Magharibi,
Viongozi mbali mbali
wa Serikali na Vyama vya Siasa,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu
Aleikum,
Awali ya yote, napenda nianze kwa
kumshukuru Mola wetu Mtukufu mwenye kustahiki kushukuriwa na viumbe vyote kwa
kutujaalia uhai na afya njema tukaweza kukutana katika hadhara hii muhimu kwa
historia na harakati za maendeleo ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano waTanzania
kwa jumla. Leo tarehe 12 Januari, 2016
tunaadhimisha kilele cha sherehe za miaka 52 tangu yalipofanyika na kufanikiwa
kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964.
Mwenyezi Mungu awape malazi mema waasisi
na viongozi wetu wa Mapinduzi waliokwishatutangulia mbele ya haki na walio hai,
Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu ili tuzidi kunufaika na hekima
zao. Mwenyezi Mungu aijaaliye nchi yetu
amani, umoja, mshikamano zaidi na atupe mafanikio katika utekelezaji wa mipango
yetu ya maendeleo na kutuongezea ustawi wa jamii yetu.
Ndugu
Wananchi,
Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar,
napenda nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli; Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiongoza Awamu ya Tano ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuchaguliwa
kwenu, ni kielelezo cha imani waliyonayo wananchi kwenu na kwa Chama cha
Mapinduzi. Natoa shukurani zangu za dhati kwenu, kwa kuja kuungana nasi katika
sherehe hizi za maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tunakukaribisheni kwa furaha kubwa pamoja na
viongozi wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mliohudhuria.
Kadhalika, napenda nitoe shukurani zangu
za dhati kwa mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, taasisi mbali mbali,
wananchi na wageni waalikwa wote kwa kuhudhuria kwa wingi katika sherehe hizi
muhimu na adhimu ambazo zimefana sana. Kuwepo
kwetu hapa siku hii ya kilele na mahudhurio makubwa kunadhihirisha kwamba
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 yanathaminiwa sana na
yataendelea kudumishwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ndugu
Wananchi,
Leo ni siku adhimu na muhimu kwa
Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla ambapo miaka 52 iliyopita waliikata
minyororo ya utawala wa kikoloni na kisultani ambao ulidumu kwa miaka 132.
Wananchi wanyonge walioongozwa na Chama cha Afro Shirazi walijitolea muhanga
kufanya Mapinduzi dhidi ya wakoloni, mabwanyenye na mabepari waliokuwa
wakiendeleza vitendo vya udhalilishaji, dhulma, unyonyaji na ubaguzi kwa
wananchi.
Madhila waliyotendewa wananchi yalihusu
masuala yote muhimu ya maisha yakiwemo kubaguliwa katika elimu, matibabu,
makaazi na matumizi ya ardhi na ubaguzi wa kukoseshwa haki za kiraia katika
nchi yao wenyewe. Haya yote leo yanabaki
kuwa ni historia baada ya Waasisi wa Mapinduzi wakiongozwa na Jemedari wake Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume na Chama cha ASP kufanya Mapinduzi tarehe 12 Januari,
1964. Huo ndio mwanzo wa utawala wa wanyonge wa Zanzibar na kupata uhuru wao wa
kweli, unaozingatia misingi ya usawa, utu na kuturejeshea heshima ya
wafanyakazi na wakulima nchini mwetu iliyopotea kwa kutawaliwa.
Leo tunaposherehekea miaka 52 ya
Mapinduzi, vile vile, tunasherehekea umoja wetu unaotokana na nchi mbili
zilizokuwa huru, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Muungano wetu umetokana na dhamira ya dhati ya vyama vyetu vya ukombozi
vya ASP na TANU na sasa CCM pamoja na uongozi bora na thabiti wa Waasisi wa
nchi yetu, hayati Mwalim Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani
Karume.
Ndugu
Wananchi,
Kwa hakika tuna wajibu wa kuwashukuru
na kuwaombea dua Waasisi wa Mapinduzi kwani wao ndio msingi wa mafanikio
makubwa wa maendeleo tuliyoyapata. Katika kipindi chote cha miaka 52, wananchi
wote kwa nyakati tafauti wamefaidika na matunda ya Mapinduzi kutokana na
malengo yake na mipango ya maendeleo iliyowekwa.
Kwa hivyo, maadhimisho ya sherehe hizi
yanatukumbusha umuhimu wa kuendelea kuyaheshimu, kuyatetea, kuyalinda na
kuyadumisha Mapinduzi yetu, kwa faida ya kila mmoja wetu. Katika kuyathamini na
kuyaenzi Mapinduzi yetu, Serikali imeamua kujenga mnara maalum wa kumbukumbu ya
Mapinduzi katika eneo la Michenzani, Mwembekisonge, uliozinduliwa mwaka jana. Naomba wananchi mwende mkautembelee mnara wa
aina yake huu pale mtakapopata nafasi ambapo pia mtapata nafasi ya kuelezwa historia
ya Mapinduzi iliyotayarishwa katika vyumba maalum.
Ndugu
Wananchi,
Jitihada za Serikali, wananchi na
washirika wetu wa maendeleo zimetuwezesha kuitekeleza mipango mikuu ya maendeleo
katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya
2020, MKUZA Awamu ya Pili na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010-2015
tuliyoitekeleza kwa kiwango kinachokadiriwa kufikia asilimia 90 pamoja na
Malengo ya Milenia. Maelezo
nitakayoyatoa yanadhihirisha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2015.
Ndugu
Wananchi,
Katika
mwaka 2015, Tume ya Mipango ya Zanzibar imeratibu mapitio ya Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II) unaomaliza muda wake mwezi wa Juni
2016. Rasimu ya mwanzo ya mkakati mpya imefikia hatua ya kuchangiwa maoni na
wahusika mbali mbali na inategemewa kuanza kutumika rasmi kuanzia bajeti ya
mwaka 2016 /2017.
Vile vile, Serikali imefuta Sheria
namba 1 ya mwaka 1999 ya miradi ya maridhiano na kutunga Sheria mpya ya
mashirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) namba 8 ya mwaka
2015. Ni matumaini ya Serikali kwamba wawekezaji binafsi wataitumia fursa ya
mashirikiano baina ya sekta hizo mbili, kupitia sheria mpya, kwa lengo la
kuongeza tija na ufanisi.
Ndugu
Wananchi,
Kutokana
na umuhimu wa utafiti, Serikali kupitia Tume ya Mipango kwa kushirikiana na
COSTECH inatayarisha Mpango wa Utafiti wa Zanzibar wenye kushirikisha sekta
zote. Rasimu ya awali ya mwongozo wa utekelezaji wa tafiti imetolewa ili kazi
ya utafiti ifanyike kitaalamu kwa lengo la kupata taarifa sahihi na kuondoa
kero za wananchi.
Katika
mwaka 2014, Serikali iliandaa programu maalum za utekelezaji wa “Matokeo kwa
Ustawi” kwa kupitia mfumo wa maabara katika sekta ya Utalii, uimarishaji wa
biashara na upatikanaji wa Rasilimali Fedha.
Utekelezaji wa programu hizi umeonesha mafanikio ya kutia moyo. Kwa
sasa, Tume iko katika hatua za matayarisho ya maabara ya Elimu na Afya kwa
kushirikiana na taasisi zinazohusika.
Maabara hizo zinatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Ndugu
Wananchi,
Licha ya kuendelea kuwepo kwa matukio
mbali mbali yanayoathiri kasi ya ukuaji
wa uchumi wa dunia, uchumi wetu umeendelea kuimarika katika kila mwaka. Mwaka 2014 Pato halisi la Taifa lilikua na
kufikia asilimia 7.0. Hali hii imechangiwa zaidi na kuimarika kwa sekta
ya viwanda na sekta ya huduma kwa kuongezeka
kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini kutokana na kuwepo kwa vivutio
vya utalii na amani na utulivu. Kadhalika,
Pato la Mtu binafsi limeongezeka hadi kufikia TZS 1,552,000 (USD 939) mwaka 2014
ikilinganishwa na TZS 1,384,000 (USD 866) mwaka 2013 sawa na ongezeko la
asilimia 12.1. Kwa mujibu wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015, pato la mtu binafsi lilitakiwa lifikie TZS
884,000 ifikapo mwaka 2015. Ni dhahiri kwamba pato la mtu binafsi limepindukia
kiwango kilichokadiriwa.
Ndugu
Wananchi,
Katika kipindi cha robo mwaka ya kwanza
ya mwaka 2015, kasi ya ukuaji wa uchumi
imefikia asilimia 6.1 na katika robo ya pili ya mwaka 2015 imefikia
asilimia 7.0. Kuendelea kuimarika kwa
hali ya uchumi kwa robo mwaka ya kwanza na ya pili kwa mwaka 2015 kumetokana na
kuimarika kwa sekta ya viwanda, sekta ndogo ya malazi, huduma za chakula,
huduma za fedha, ufugaji, bima pamoja na ukuaji wa sekta ndogo ya ujenzi.
Katika mwaka 2015, kasi ya mfumko wa
bei za bidhaa na huduma nchini imeendelea kuwa ya tarakimu moja kutoka asilimia
5.6 mwaka 2014 kufikia asilimia 5.7 mwaka 2015.
Serikali inaendelea na juhudi za kudhibiti kasi ya mfumko wa bei nchini
kwa kupunguza ushuru wa bidhaa muhimu zinazoingizwa nchini na kuwasaidia
wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa beif nafuu ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Ndugu
Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeongeza
ufanisi katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti uvujaji wa mapato
hayo. Katika kipindi cha miezi sita ya
kwanza ya mwaka wa fedha 2015/2016, mapato ya ndani yalifikia TZS Bilioni 188.4
ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka 2014/2015 ambapo TZS Bilioni
172.5 zilikusanywa, sawa na ongezeko la mapato
la asilimia 9.2. Vile vile, Serikali
inaendelea na juhudi za kuimarisha mapato ikiwemo kupunguza misamaha ya kodi
katika baadhi ya miradi ya uwekezaji na kufanya marekebisho ya viwango vya ada
mbali mbali. Kadhalika, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha kodi mpya ya miundombinu, ili kuhakikisha
tunakuwa na fedha za kuiendeleza na kuitunza miundombinu yetu.
Ndugu
Wananchi,
Serikali iliendelea kuwashajiisha
wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta zote kuu za kiuchumi na
kijamii. Katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2015, jumla ya miradi 31 yenye
thamani ya Dola za Marekani Milioni 316.0 imeidhinishwa katika sekta mbali
mbali katika miradi hio, miradi mingi ni ya utalii. Miradi hii itakapomalizika
itatoa nafasi za ajira 2,500.
Juhudi kubwa zilifanywa zilizopelekea kuanzishwa
kwa utekelezaji wa kuyaendeleza Maeneo Huru ya Uchumi kwa vitendo. Mradi wa
Ujenzi wa Mji Mpya wa Fumba umeanza, ambapo kiwanda kikubwa cha maziwa kimejengwa na kimeanza kazi Julai, 2014. Mji huo utajumuisha ujenzi wa nyumba 650
zitakazouzwa kwa watu mbali mbali.
Ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa kuanza Februari mwaka huu. Kadhalika, bandari ndogo itakayotoa huduma
kwa wananchi na wageni itajengwa katika eneo hilo. Serikali, kwa kushirikiana
na Kampuni ya “Union Property Developer” na “Coastal Dredging” hivi sasa
inaendelea na ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara mpya zenye upana wa mita
15, mita 30 pamoja na barabara kuu ya mita 60.
Ndugu
Wananchi,
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,
Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa kibiashara pamoja na hoteli kubwa za kisasa,
nyumba za kuishi, uwanja wa ndege mdogo na uwanja wa kimataifa wa “golf ” wa
kisasa vitajengwa. Kampuni ya “Pennyroyal
ya Gibralter” imetenga jumla ya Dola za Kimarekani milioni 800 kwa ajili ya
mradi huu. Kampuni hiyo hivi sasa inaendelea
na ujenzi barabara ya kisasa inayotoka Mkwajuni kupitia Kijini hadi Mbuyutende
na imefikia hatua nzuri.
Katika kuliendeleza eneo la Bwawani
mnamo mwezi wa Novemba 2015, Serikali ilitiliana saini Mkataba na Kampuni ya
“Quality Group Limited” ambayo itaanzisha mradi mkubwa wa kuendeleza Hoteli ya
Bwawani na maeneo yaliyoizunguka. Kampuni
hiyo imetenga Dola za Marekani zipatazo Milioni 200 zitakazotumika kwa ajili ya
kuifanyia matengenezo makubwa Hoteli ya Bwawani, ili ifikie kiwango cha nyota
tano. Kadhalika, kampuni hiyo ya
“Quality Group Limited” itajenga majengo ya biashara na kituo cha mikutano ya
Kimataifa katika eneo hilo la Bwawani.
Aidha, Serikali imeidhinisha mradi wa
uimarishaji wa Hoteli ya “Mtoni Marine”, wenye lengo la kutengeneza ufukwe maalum
kwa ajili ya mapumziko ya wageni na wenyeji.
Sambamba na uimarishaji huo, utaanzishwa mji mdogo wa kisiwa kwa lengo
la kuikuza sekta ya utalii.
Ndugu
Wananchi,
Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
Zanzibar (ZSSF) nao umeshajiika kuwekeza katika ujenzi wa majengo ya kisasa,
ili kubadilisha taswira ya Zanzibar. Katika mwaka huu wa fedha, 2015/2016, ZSSF
imeanza kutekeleza Mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo la Mbweni –
Unguja. Mradi huu unajumuisha ujenzi wa
jumla ya majengo 18 ya ghorofa 7 kila moja na yatakapomalizika, jumla ya
nyumba (flats) 252 zitapatikana. Mradi huu unatarajiwa kumalizika katika kipindi
cha miaka mitatu ijayo.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka 2015, suala la kuimarisha
mazingira ya biashara lilipewa umuhimu mkubwa. Serikali ilichukua hatua ya
kuhakikisha kuwa bidhaa za chakula zinakuwepo nchini wakati wote. Takwimu
zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 hakukuwa na upungufu wa bidhaa
hizo. Serikali imeanzisha Baraza la Kusimamia Utoaji wa Leseni kwa lengo la
kuweka mfumo mzuri na ulio bora katika utoaji wa leseni na vibali vya biashara.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ililinunua
jumla ya tani 2,826.5 za karafuu 2,826.5 zenye thamani ya TZS bilioni 39.5
kutoka kwa wakulima katika mwaka
2014/2015, hadi kufikia tarehe 4 Januari, 2016, Serikali ilinunua jumla ya tani
3,235.1 zenye thamani ya TZS bilioni 45.3.
Kwa upande wa mauzo, katika mwaka
2014/2015, Serikali iliuza nchi za nje jumla ya tani 2,766.2 za karafuu zenye
thamani ya TZS bilioni 53.3. Kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia tarehe 31
Disemba, 2015, Serikali imeuza karafuu nchi za nje tani 2,122.0 zenye thamani
ya TZS bilioni 36.0. Msimu wa karafuu wa mwaka huu bado unaendelea
na wakulima wanaendelea kuuza karafuu zao ZSTC na matarajio ya Serikali ni kununua
tani 5,500 za karafuu.
Kadhalika, katika kipindi cha mwaka
2014/2015, Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya TZS milioni 342.3 kwa
wakulima 126 wa karafuu wa Unguja na Pemba. Mikopo hiyo imewasaidia kununua
pembejeo na vitendea kazi. Nachukua
nafasi hii kuwapongeza wakulima wa Unguja na Pemba kwa juhudi zao
wanazozichukua katika kuliendeleza zao la karafuu kwa kushirikiana na Serikali.
Aidha kwa lengo la kuliendeleza zao la
karafuu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizindua Mfuko wa Maendeleo ya
Karafuu Zanzibar ambao Shirika la ZSTC limeweza kulipa fidia kwa walioanguka
kwenye mikarafuu jumla ya TZS milioni 60 na kutoa mikopo.
Ndugu
Wananchi,
Juhudi za kufufua viwanda zilipata
mafanikio zaidi katika mwaka 2015 ikilinganishwa na miaka iliyopita. Bidhaa
zilizozalishwa viwandani kwa mwaka 2015 zikiwemo maziwa, sukari, maji ya kunywa,
unga wa ngano, juisi, sabuni, bidhaa za
nguo na viungo zilikuwa na thamani ya TZS bilioni 136.0, ikiwa ni ongezeko la
asilimia 5.51 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo bidhaa zilizozalishwa
nchini zilikuwa na thamani ya TZS bilioni 128.9. Kuimarika kwa viwanda vyetu kutaongeza ajira
kwa wananchi na kuwapunguzia umasikini.
Ndugu
Wananchi,
Serikali imepanga na kutekeleza
mikakati mbali mbali ya kuiendeleza sekta ya utalii ambayo hivi sasa ndiyo
sekta kiongozi kwa uchumi wetu. Wawekezaji wameshajiishwa katika ujenzi wa
hoteli ambapo hoteli ya “Park Hyatt” ilifunguliwa hivi karibuni. Kamisheni ya
Utalii imejitangaza katika masoko mapya ya huko China na India. Kamisheni hio imefungua Ofisi ya Uwakala huko
Mumbai, India, kwa lengo la kuimarisha utalii. Katika kuimarisha huduma za utalii na upatikanaji
wa ajira, hatua zimechukuliwa kwa kuanzisha mafunzo ya fani mbali mbali za
utalii yanayotolewa katika kiwango cha Stashahada katika Chuo Cha Maruhubi na
Shahada na Stashahada katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Katika mwaka wa
mafunzo uliomalizika wanafunzi 1028 wamemaliza yao kwenye vyuo hivyo. Katika mwaka ujao tunatarajia Chuo cha Utalii
Maruhubi kitaunganishwa na SUZA.
Katika mwaka 2015, watlii waliendelea
kuitembelea Zanzibar kutokana na vivutio viliopo, pamoja na kuwepo amani na
utulivu. Jumla ya watalii 254,699 waliitembelea Zanzibar katika kipindi cha
Januari-Novemba, 2015. Wito wangu kwa wananchi ni kuwa tuendelee
kushirikiana katika kulifanikisha lengo letu la Utalii kwa Wote, ili mafanikio
haya tunayoyaona yapatikane zaidi na yazidi kuimarisha uchumi wetu.
Ndugu
Wananchi,
Jitihada kubwa imefanywa na Serikali
katika kuimarisha sekta ya Kilimo kwa lengo la kuhakikisha kuwa uhakika wa
chakula na lishe unakuwepo. Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya asilimia 75 kwa
wakulima ya gharama za pembejeo za kilimo na huduma za matrekta kwa Unguja na
Pemba. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016, tayari tani 750 za mbolea na
lita 15,000 za dawa ya kuulia magugu zimenunuliwa kwa lengo kuwapa wakulima,
ili kuimarisha kilimo.
Kuhusu kilimo cha mpunga cha
umwagiliaji maji, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya Utekelezaji wa Mradi
wa Ujenzi wa Miundombinu ya umwagiliaji maji ambao ukimalizika utaongeza uzalishaji
wa mpunga kutoka kiwango cha sasa cha wastani wa tani 30,000 kwa mwaka hadi
kufikia tani 45,000 kwa mwaka. Shughuli
za utafiti katika Taasisi ya Kilimo Kizimbani zimeimarishwa. Kuhusu Chuo cha Kilimo cha Kizimbani, jumla
ya wahitimu 93 wamemaliza masomo yao Stashahada na Cheti katika mwaka 2015 na
tunatarajia wahitimu hawa wataajiriwa, ili kuongeza nguvu shughuli za ugani na
ufugaji.
Kwa upande wa uendelezaji wa maliasili
zetu, Serikali inaendelea kusimamia ulinzi na udhibiti wa misitu yetu ikiwemo
msitu wa Jozani Unguja na msitu wa Ngezi Pemba na misitu mingine ya asili kwa
kushirikiana na wananchi. Juhudi
zitaendelea kufanywa kuwahamasisha wananchi juu ya ufugaji nyuki wa kisasa.
Ndugu
Wananchi,
Jitihada kubwa zilifanywa katika
kuiendeleza sekta ya uvuvi. Katika mwaka
2015, kiwango cha samaki waliovuliwa kilifikia tani 31,439.0 zenye thamani ya TZS
bilioni 123.80 ikilinganishwa na tani 30,108.6 zenye thamani ya TZS bilioni
116.3 zilizovuliwa mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 6. Uzalishaji wa zao la mwani umeongezeka kutoka
tani 13,301 mwaka 2014 hadi kufikia tani 15,076 mwaka 2015. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 13.
Hivi karibuni Serikali inatarajia
kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya
samaki huko Beit el Ras kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA). Kadhalika,
Serikali imetiliana saini makubaliano ya awali na Kampuni ya Hairu kutoka
Sri-Lanka ambayo itawekeza katika kiwanda cha kutengeneza boti zenye urefu wa
mita 6, na mita 9 kwa ajili ya wavuvi wadogo na mita 18 zitakazofika bahari
kuu. Vile vile, kampuni hiyo itaweka mitambo
ya kusindika samaki na mazao mengine ya baharini.
Kadhalika, Serikali inategemea kuanzisha
mradi wa ujenzi wa diko la kisasa Malindi katika mwezi wa Novemba, 2016. Mradi huu unafadhaliwa na Serikali ya Japan
na unategemewa kugharimu Dola za Kimarekani milioni 9.3 na unatarajiwa
kukamilika katika kipindi cha miaka miwili.
Madhamuni makubwa ya mradi huu ni kuwawezesha watumiaji wa diko la
Malindi kuuza na kununua samaki wao wakiwa katika kiwango bora, kuwaongezea
tija wavuvi, wachuuzi, madalali na wafanyabiashara wadogo wa diko hilo pamoja
na kuweka mazingira mazuri ya kuweka vyombo vya uvuvi bandari.
Ndugu
Wananchi,
Kuhusu sekta ya ufugaji, juhudi kubwa zimefanywa
ya kuwaendeleza wafugaji wetu kupitia Programu mbali mbali. Juhudi hizo
zimeleta hamasa katika ufugaji wa kisasa na kuongeza idadi ya wafugaji wa
ng’ombe na mbuzi wa maziwa kutoka wafugaji 9,795 mwaka 2014 hadi kufikia 10,082
mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 2.9. Juhudi hizi zimepelekea kuwepo kwa
ongezeko la uzalishaji wa nyama na maziwa.
Kwa lengo la kuwaendeleza wafugaji, jumla
ya wafugaji 16,819 walitembelewa na kupatiwa mafunzo ya kitaalamu ya ufugaji
bora wa ngo’mbe, mbuzi, kuku na mifugo mingine.
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 84 ya lengo la kuwafikia wafugaji 20,000.
Vile vile, wawekezaji wa ndani wameshajiishwa, ili wawekeze katika vikundi
vidogo vidogo vya kuongeza thamani bidhaa za mifugo. Aidha, kwa lengo la kukabiliana na maradhi
mbali mbali ya mifugo, Serikali
inaendelea kuziimarisha huduma za uchunguzi wa maradhi ya mifugo kwa kuongeza
wataalamu, vifaa na kuimarisha miundombinu ya maabara huko Maruhubi pamoja na
kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo vituo vya karantini na vituo
vya uzalishaji.
Ndugu
Wananchi,
Katika kukabiliana na changamoto za
kimazingira, Serikali imeandaa na kupitisha sheria mpya ya usimamizi wa
mazingira Zanzibar Nambari 3 ya mwaka 2015.
Lengo kuu la sheria hiyo ni kuimarisha uhifadhi wa mazingira
nchini. Aidha, kupitia sheria hiyo,
Serikali imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) ili kuyashughulikia
masuala muhimu yanayohusu mazingira na kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu
anazingatia masharti ya sheria ya mazingira.
Jitihada zinaendelea kuchukuliwa na
Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kukabiliana na
athari za kimazingira pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti vitendo
vya uharibifu wa mazingira vinavyosababishwa na shughuli za ujenzi, ukataji wa
miti ovyo, utupaji wa taka za plastiki ngumu na vifaa vya kielektroniki. Katika
kukabiliana na uharibifu wa mazingira jumla ya mikoko milioni 50 sawa na hekta
20 zimepandwa katika maeneo tisa ya Unguja na Pemba ili kuhuisha maeneo
yaliyokatwa mikoko.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu miundombinu, katika mwaka 2015 Serikali imekamilisha ujenzi wa
barabara za lami mbili ambazo ni barabara ya Konde hadi Wete (km.15) na kutoka
Wete hadi Konde (km.15). Ujenzi wa
barabara za lami sasa unaendelea katika barabara ya Ole hadi Kengeja huko Pemba (km. 35). Kwa
barabara za Unguja ujenzi unaendelea kwa barabara za Jendele kupitia Cheju hadi
Kaebona (km. 11.7) na Koani hadi Jumbi (km. 6.3) na Mwanakwerekwe hadi Fuoni (km. 4). Kadhalika, Serikali inaendelea kuifanyia
matengenezo makubwa ya barabara ya Ole hadi Konde kuanzia eneo la Meli 5 hadi
Chwale (km. 13) huko Pemba kwa kufumuliwa na kutiwa lami upya.
Katika mwaka wa fedha 2015/2016,
Serikali kwa upande wa Unguja ina lengo la kujenga barabara ya Bububu kupitia Mahonda
hadi Mkokotoni (km30), barabara ya Matemwe-Mbuyutende-Muyuni (km 11.5), Pale
hadi Kiongele (km 5), Mkwajuni-Kijini-Mbuyutende (km 9), barabara kutoka Fuoni hadi Kombeni (km 7). Kwa upande wa Pemba itajengwa upya barabara ya Wete hadi Chake
Chake (km 22.1). Wito wangu kwa wananchi
ni kuendelea kuzitunza barabara zetu na kutoa ushirikiano kwa Serikali na
wakandarasi wanaojenga barabara zetu.
Ndugu
Wananchi,
Kuhusu ujenzi wa bandari mpya ya
Mpigaduri, Serikali imekamilisha matayarisho yote ya bandari hiyo katika mwaka
2015. Ujenzi wa bandari hii unategemewa
kuanza katika robo ya kwanza ya mwaka 2016.
Aidha, katika mwaka 2015, Serikali imejenga gati ndogo katika Kisiwa cha
Tumbatu inayotarajiwa kumalizika Februari, 2016 na imekamilisha matengenezo ya
jengo la abiria katika bandari kuu ya Malindi.
Katika azma ya kuimarisha usafiri wa
baharini, Serikali ilitengenezesha meli mpya MV Mapinduzi II katika kampuni ya
Daewoo ya Jamhuri ya Korea. Meli hio
iliwasili nchini tarehe 2 Disemba, 2015.
Meli hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo tani 200, imeanza
ratiba zake tarehe 8 Januari, 2016 kwa safari ya kwenda Pemba. Vile vile, Serikali imeamua kununua meli
nyengine mpya ya mafuta mwaka huu.
Ndugu
Wananchi,
Katika hatua za kuimarisha usafiri wa
anga, Serikali imechukua hatua madhubuti ya kukamilisha ujenzi wa jengo jipya
la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume. Katika
mwaka 2015, tuliukamilisha na kuuzindua mradi wa ujenzi wa maegesho ya ndege na
njia za kupitia ndege katika kiwanja hicho.
Aidha, Kiwanja cha Ndege cha Pemba kimeimarishwa
kwa kutiwa taa za kuongozea ndege za kisasa.
Mradi huo umekamilia na kuzinduliwa tarehe 7 Januari, 2016. Hatua inayofuata sasa ni ujenzi wa jengo jipya la abiria la kisasa, kuongeza
urefu wa njia ya kurukia na kutulia ndege (Runway) kutoka urefu wa sasa 1.5km
hadi kufikia 2.5km. Katika kutekeleza mpango huu, Serikali tayari imekubaliana
na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) katika utekelezaji wa mradi huo.
Ndugu
Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeendelea na kazi ya usambazaji wa umeme vijijini. Katika kipindi cha Januari hadi Novemba,
2015, kazi kubwa ya uwekaji wa laini za umeme imefanywa, ambapo kilomita 47.25 za laini ndogo na
kilomita 31.85 za laini kubwa ya umeme zimewekwa Unguja na Pemba. Kazi ya kupeleka umeme katika visiwa vya Makoongwe
na Kisiwapanza huko Pemba imekamilika. Nalipongeza
Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) kwa kukamilisha kazi ya kuvusha umeme chini
ya bahari na kuupeleka kwenye visiwa hivi kwa wakati uliopangwa. Kisiwa cha Shamiani kilichopo katika Wilaya
ya Mkoani kinatarajiwa kupatiwa umeme
katika mwaka huu wa fedha, 2015/2016.
Ndugu
Wananchi,
Vile vile, katika jitihada za
kushughulikia utafutaji wa mafuta na gesi, Serikali tayari imekamilisha Rasimu
ya Sera ya Mafuta na Gesi. Kuhusu Sheria
ya Mafuta na Gesi asilia, rasimu yake ipo katika hatua za mwisho za matayarisho
na inatarajiwa kukamilika baada ya muda si mrefu. Nachukua nafasi hii kwa kumpongeza kwa
dhati Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuhakikisha kwamba kabla ya kuondoka
madarakani, suala la Zanzibar kusimamia mafuta na gesi asilia wenyewe, linapatiwa ufumbuzi. Sheria ya Bunge
ya 2015 ilitungwa ambapo sasa Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuchimba mafuta na
gesi yake kwa kutunga sheria yake
wenyewe itakayosimamia nishati hii pamoja na faida zake zote. Hatua hii tuliyoifikia ni kubwa kwa ajili ya
maendeleo ya Zanzibar.
Ndugu
Wananchi,
Jitihada kubwa zimefanywa na Serikali
kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuimarisha elimu. Idadi ya skuli za maandalizi zimeongezeka na
zimefikia 270 katika mwaka 2015, skuli
za msingi zimeongezeka kutoka skuli 359 mwaka 2014 hadi skuli 370 mwaka 2015 na
skuli za sekondari zimeongezeka na kufikia skuli 263 mwaka 2015 kutoka skuli
210 mwaka 2014.
Serikali kwa kushirikiana na Washirika
wa Maendeleo ina mpango wa kujenga skuli za msingi mpya 11 katika mwaka huu wa
fedha wa 2015/2016. Kati ya skuli hizi, skuli 9 ni za ghorofa, maandalizi ya
ujenzi wa skuli hizi yameshaanza ambapo fedha za mradi huo zitatokana na Mfuko
wa OPEC.
Aidha, vituo vipya vya mafunzo ya amali
vitajengwa kuanzia mwaka huu huko Makunduchi katika Mkoa wa Kusini Unguja na
Mtambwe kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika,
ili kuwapa fursa vijana kujifunza kazi za amali zikiwemo ufundi wa aina mbali
mbali.
Ndugu
Wananchi,
Elimu ya juu inayotolewa na vyuo vikuu
viliopo Zanzibar inaendelea kuimarishwa kwa kuongezwa Idara mpya na vitivo vya
vyuo hivyo. Idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya Zanzibar imefikia 5,923,
hadi kufikia mwezi wa Novemba mwaka 2015. Aidha, kwa kushirikiana na Serikali
ya Falme ya Saudi Arabia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mpango wa
kujenga Chuo Kikuu kipya katika eneo la Dole. Idadi ya wanafunzi wanaopata
mikopo katika vyuo vya ndani na nje ya Tanzania sasa imefikia 3,016 ambapo
jumla ya TZS bilioni 9.3 zilitengwa mwaka jana kukidhi mikopo hiyo. Hadi sasa wanafunzi 1,016 wameanza kurejesha
mikopo yao kati ya wanafunzi 3,800 waliohitimu masomo yao.
Ndugu
Wananchi,
Jitihada kubwa zimefanywa katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kupitia miradi na
programu mbali mbali za maji mijini na vijijini. Hali ya upatilkanaji wa maji safi na salama
imefikia wastani wa asilimia 87 mijini na asilimia 70 katika vijiji, katika
mwaka 2015. Lengo la Serikali ni
kuimarisha upatikanaji wa huduma hizo hadi kufikia asilimia 97 katika miji na
asilimia 85 katika vijiji ifikapo mwaka 2020.
Aidha, tunatarajia kulipatia ufumbuzi,
tatizo la maji safi na salama katika Manispaa ya mji wa Zanzibar kufuatia
kutiwa saini Mkataba wa Mradi wa Maji Mjini tarehe 29 Disemba, 2015
unaogharimu Dola za Kimarekani milioni
21. Mradi huo unatarajiwa kumalizika
katika miezi 18 ijayo.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka 2015 jitihada zetu za
kuiendeleza Hospitali ya Mnazi mmoja kuwa ya Rufaa zimefanikiwa sana. Ujenzi wa jengo la utibabu wa watoto na wagonjwa
wenye matatizo ya figo unaendelea vizuri ambapo tarehe 5 Januari, 2016 umewekewa
jiwe la msingi pamoja na jengo lilokuwa la kiwanda cha madawa limeanza
kufanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya huduma za wajawazito na watoto. Majengo
haya mawili yanagharamiwa na Serikali ya Norway, Uholanzi pamoja na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Kazi za kuzipandisha daraja hospitali
ya Koteji ya Makunduchi na Kivunge zinaendelea vizuri. Kwa utoaji wa huduma, hospitali ya Makunduchi
na Kivunge tayari zimefikia hatua nzuri cha kiwango cha hospitali za wilaya na kwa
hospitali za Micheweni na Vitongoji kazi hio nayo inaendelea vizuri.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka wa 2015, hospitali ya
Abdalla Mzee Pemba imeanza kujengwa upya kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China. Utakapokamilika ujenzi wa
hospitali hii itakuwa ni ya kisasa yenye uwezo wa kutoa huduma zote za utibabu
na uchunguzi wa maradhi na itakuwa na
hadhi ya hospitali ya rufaa ya Mkoa.
Kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa
dawa, Serikali imeongeza bajeti ya dawa
kutoka TZS bilioni moja kwa mwaka
2013/2014 hadi kufikia TZS bilioni 4.3 kwa mwaka 2015/2016. Gharama za
kuchangia huduma za uchunguzi wa maradhi
kwa kutumia “X-Ray”, “CT-Scan” na “Ultra Sound”, zimeondolewa hivi sasa zinatolewa bila ya malipo kwa
wananchi wote.
Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika
kupunguza vifo vya mama na watoto kutokana na kinamama kujifungulia hospitalini
na kuenea kwa huduma za uzazi vijijini. Katika mwaka 2014, kiwango cha kinamama
waliojifungulia hospitali kimefikia asilimia 67.8 ikilinganishwa na asilimia
56.1 ya mwaka 2013. Aidha, kutokana na jitihada za kuwasomesha madaktari tumepata
mafanikio ya kutia moyo katika
kuimarisha utoaji wa huduma kwa uwiano wa daktari kwa wananchi wanaohudumiwa. Kwa sasa uwiano wa daktari na idadi ya watu
anaowahudumia ni daktari mmoja kwa watu 8,885 (1:8885), kutoka kiwango cha
daktari mmoja kwa watu 9,708 (1:9708) mwaka jana.
Ndugu
Wananchi,
Serikali imefanya jitihada kubwa katika
kuimarisha huduma za kinga na tiba.
Katika kipindi cha mwaka 2015, Serikali iliweka mkazo maalum katika kuyakinga
na kuyadhibiti maradhi ya kuambukiza na yasio ya kuambukiza ambayo yameendelea
kuwa tatizo kwa watu wa Zanzibar.
Vita dhidi ya Malaria vimeendelezwa na kiwango
cha malaria bado kipo chini ya asilimia moja.
Kazi ya usambazaji na ushajiishaji wa matumizi sahihi ya vyandarua,
ufukizaji wa dawa na kuulia mbu majumbani pamoja na uchunguzi na tiba kwa
wagonjwa wa Malaria inaendelezwa. Katika kupambana na Malaria, kati ya Julai
2014 hadi Machi 2015, jumla ya vyandarua 114,394 sawa na asilimia 51 ya makisio
ya mwaka uliomalizika vimegawiwa. Aidha, jumla ya nyumba 70,368 zilikusudiwa
kupigwa dawa ambapo utekelezaji halisi ni nyumba 66,497 sawa na asilimia 94.5
ya makisio. Kuhusu uchunguzi wa vimelea
vya Malaria, jumla ya watu 172,972 walichunguzwa ambapo watu 1,648 sawa na
asilimia 0.9 waligundulika kuwa na vimelea vya maradhi ya malaria.
Kuhusu tatizo la kipindupindu ambalo
lilianza mwishoni mwa mwaka 2015 zilifanyika jitihada kubwa katika kuyadhibiti
maradhi hayo. Jumla ya wagonjwa 843
waliripotiwa kupata kipindupindu, Unguja na Pemba. Kwa bahati mbaya wapo wachache miongoni mwao
waliofariki. Hali ya maradhi ya
kipindupindu imedhibitiwa na kasi yake
imepungua sana. Naupongeza uongozi wa
Wizara ya Afya kwa kazi nzuri ulioifanya.
Nawaomba wananchi waendelee kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya
kuhusu maradhi haya.
Ndugu
Wananchi,
Katika sekta ya habari, jitihada
zimeendelea kuchukuliwa katika
kuimarisha shughuli za Shirika la Utangazaji la Zanzibar pamoja na Gazeti la
Zanzibar Leo. Kupitia Shirika la
Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Serikali imetekeleza vyema wajibu wake wa kuielimisha
jamii na kuipa habari na burudani.
Matangazo ya radio na televisheni za ZBC yameendelea kurushwa hewani kwa
saa 24. Chaneli 2 za ZBC-TV (ZBC na
ZBC2) zimeendelea kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika kutengeneza vipindi vya
kienyeji katika nyanja tafauti. Matangazo ya radio ya ZBC yameimarishwa na
kusikika katika masafa ya kati na masafa ya mbali na kurudisha tena chaneli ya
“Spice FM Radio”.
Kadhalika, Shirika la Magazeti la
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar limeendelea kuimarisha huduma zake za
kuwapasha habari za matukio mbali mbali wananchi na kuwashajiisha katika
kushiriki masuala ya maendeleo kupitia gazeti la Zanzibar Leo linalotolewa kila
siku. Aidha, kupitia gazeti la Zaspoti;
wananchi hupata habari mahsusi za michezo na utamaduni kutoka ndani na nje ya nchi. Gazeti la Zanzibar Leo linazidi kupanua wigo kwa
kuuzwa Unguja na Pemba pamoja na mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara.
Ndugu
Wananchi,
Jengo jipya la Chuo cha Uandishi wa Habari
linakamilishwa ujenzi wake ulioanza Juni 2015 katika eneo la Kilimani na
unatarajiwa kumalizika hivi karibuni. Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hili litatoa
fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kujifunza taaluma hiyo.
Aidha, Serikali iliahidi kujenga Studio
ya kisasa ya muziki na filamu kwa ajili ya wasanii wa Zanzibar katika jengo lilokuwa
la Sauti ya Tanzania Zanzibar liliopo Rahaleo.
Ahadi hio imetekelezwa baada ya
jengo hilo kukarabatiwa na vifaa vya studio vipya kununuliwa. Studio hio ilizinduliwa rasmi tarehe 8
Januari, 2016. Studio hiyo itatumiwa na wasanii kufanya kazi zao kwa ufanisi
mkubwa. Vile vile, Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari na Tamasha la Filamu la
Nchi za Jahazi (ZIFF) yameendelea kufanyika na yanaendelea kutoa mchango mkubwa
katika kutoa ajira kwa vijana pamoja na
kuchochea kukua kwa sekta ya utalii nchini.
Kuhusu sekta ya michezo, Serikali iliadhimisha
kwa mafanikio makubwa siku ya mazoezi inayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe
mosi Januari kwa lengo la kuhamasisha umuhimu wa kufanya mazoezi, kwa madhumuni
ya kuzitunza afya zetu. Ni jambo la kufurahisha kwamba mahudhurio ya mwaka huu
ya wanamichezo yalitia fora. Aidha, mashindano ya riadha ya wilaya zote za
Zanzibar yalifanywa kwa juhudi kubwa ili kuimarisha michezo maskulini. Kadhalika, katika kuiimarisha miundombinu ya
michezo, kazi ya uwekaji wa mpira wa kukimbilia katika uwanja wa Gombani iliyoanza
mwaka 2015 inatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Vile vile, kazi ya ujenzi wa uwanja mpya wa
Mao-tse-tung itaanza rasmi mwezi Februari, 2016 na inatarajiwa kukamilika mwaka
ujao.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka 2015 Serikali imeendelea kuchukua
hatua ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kwa kadri hali ya ukuaji wa uchumi
wetu inavyoruhusu. Katika mwaka huo wa 2015, Serikali ilifanya marekebisho ya
mishahara kwa watumishi wenye uzoefu na elimu ya kiwango cha Stashahada ambao
utumishi wao umefikia zaidi ya miaka 15. Zoezi la kuwapanga watumishi wote wa
Serikali kulingana na madaraja yao limekwishaanza kwa hatua za awali za
kukusanya taarifa, ili kazi hiyo ifanywe kwa uangalifu mkubwa na kupata
ufanisi.
Serikali imeendelea kuchukua hatua ya
kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kupambana na
umaskini. Kupitia Mfuko wa Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi, hadi kufikia mwezi Novemba 2015, jumla ya mikopo 286 yenye thamani
ya TZS milioni 436.2 imetolewa. Mikopo hiyo imewanufaisha wananchi wapatao
8,976. Kuanzia Januari hadi Novemba,
2015, jumla ya TZS milioni 397.2 zilikusanywa ikiwa ni marejesho ya mikopo hio.
Aidha, Serikali ilisajili taasisi 4 za Wakala binafsi za ajira na kuongeza idadi
ya taasisi hizo kufikia 8. Jumla ya vijana 240 wamepata ajira kupitia mawakala
hao wa ajira.
Ndugu
Wananchi,
Kwa lengo la kuwasaidia vijana
kuondokana na tatizo la ajira, Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi imeongeza fedha za dhamana katika Benki ya CRDB kutoka TZS milioni 100
hadi TZS milioni 150 katika mwaka 2015. Kutokana na hatua hiyo, Benki ya CRDB
imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya TZS milioni 975.3 kwa vijana 2,952.
Ndugu
Wananchi,
Miongoni mwa shabaha ya Mapinduzi ya
mwaka 1964 ilikuwa ni kuwapatia wazee waliokuwa
hawana uwezo, matunzo mazuri ya maisha yao kwa kuwapatia nyumba bora za kuishi
na huduma nyengine. Hii ndio sababu
iliyopelekea mara tu baada ya kufuzu kwa Mapinduzi, Serikali ilijenga nyumba za
wazee za Sebleni, Selemu na sehemu ya
Limbani na kuwaweka wazee ambao wamepatiwa huduma za malazi, matibabu na fedha
za matumizi. Katika mwaka 2015, Serikali
imelipa jumla TZS milioni 14.3 kila mwezi kwa wazee wanaotunzwa katika nyumba
za Sebleni, Welezo Limbani na Makundeni.
Kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa
maisha wazee wastaafu, Serikali inaendelea na matayarisho ya uanzishwaji wa
Mpango wa Pensheni Jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70 na
kuendelea. Zoezi la usajili linaendelea ambapo
tayari jumla ya wazee 22,443 waliostaafu Serikalini na waliokuwa hawajafanya
kazi Serikalini wamekwishasajiliwa. Utaratibu wa kuanza kuwalipa wazee hao kupitia
mpango huu kiasi cha TZS 20,000 kwa mwezi, kitatolewa kuanzia mwezi Aprili
mwaka huu wa 2016. Kwa wale waliostaafu Serikalini wataendelea kupata pensheni
yao ya kisheria.
Ndugu
Wananchi,
Kuhusu watu wenye ulemavu, Serikali
imechukua hatua za kuhakikisha wanapatiwa haki zao na kuwekewa mazingira mazuri
yanayozingatia mahitaji yao pamoja na kushirikishwa katika masuala mbali mbali
ya kijamii na kitaifa. Watoto wenye
ulemavu wanapatiwa haki yao ya elimu katika skuli zetu kwenye mpango wa elimu
mjumuisho. Ujenzi wa majengo ya huduma
umeendelea kufanywa kwa kuzingatia watu wenye mahitaji maalum.
Kadhalika, jitihada zimefanywa na
Serikali katika kuwashirikisha kinamama katika masuala ya maendeleo pamoja na
kulinda haki zao kwa kupiga vita vitendo vyote vya udhalilishaji wanawake na
watoto ambapo Serikali ilianzisha kampeni hiyo mwaka jana. Kampeni hii inaendelea vizuri ingawa
changamoto bado zipo. Wito wangu kwenu ni kuwa sote tushirikiane katika kuifanikisha
Kampeni hii.
Ndugu
Wananchi,
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana
katika sekta zote nilizozielezea katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wa
2015, vile vile, tulipata mafanikio makubwa katika taasisi za sheria na utawala
bora. Ni katika kipindi hiki ambapo
Sheria ya Maadili ya Viongozi imetungwa na ipo tayari kutumika. Vile vile,
katika kipindi hiki Serikali ilikabiliwa na changamoto kadhaa, katika
utekelezaji wa mipango yake. Baadhi ya
changamoto hizo zimeanza kushughulikiwa na nyengine zinafanyiwa kazi.
Ndugu
Wananchi,
Nyote mtakumbuka kwamba, nchi yetu
iliingia katika Uchaguzi Mkuu tarehe 25 Oktoba, 2015 ambapo wananchi wa pande
zote mbili za Muungano walipata fursa ya
kuwachagua Viongozi wao.
Uchaguzi wa Viongozi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania uliosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania umemalizika na sote tunafahamu kwamba, Chama cha Mapinduzi
kimepata ushindi mkubwa. Kwa mara
nyengine tena nampongeza Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wake wa Rais.
Aidha, nawapongeza wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
madiwani waliochaguliwa kwa upande wa CCM.
Kwa upande wa Zanzibar, Tume ya
Uchaguzi iliufuta uchaguzi wa Zanzibar
tarehe 28 Oktoba, 2015, baada ya kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa
kama zilivyoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Kadhalika, uamuzi huo wa Tume ulitangazwa
katika Gazeti Rasmi la Serikali la tarehe 6 Novemba, 2015 kwamba Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar imeyafuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa
tarehe 25 Oktoba, 2015 na kwamba uamuzi wa Tume wa tarehe nyengine ya kurudiwa
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utatangazwa baadae.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi Namba 11
ya mwaka 1984, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndio yenye jukumu la kusimamia na
kuendesha uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Kwa
hivyo, nawaomba wananchi waendelee kuishi kwa amani na kupendana huku
tukisubiri Tume ya Uchaguzi Zanzibar itangaze tarehe nyengine ya kurudia
uchaguzi.
Aidha, katika suala zima la hali ya
kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu, viongozi
wenu tulishauriana tukutane ili tufanye mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia
ya amani, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano. Hatimaye
tulikubaliana tuanze mazungumzo hayo. Mazungumzo haya yanatuhusisha viongozi
sita, tuliopo madarakani na waliostaafu mimi nikiwa Mwenyekiti. Mazungumzo hayo
bado yanaendelea. Taarifa ya pamoja ya mazungumzo hayo itatolewa na wajumbe
tunaofanya mazungumzo mara tu mazungumzo hayo yatakapokamilika. Katika kipindi hiki bado nawaomba wananchi
waendelee kuwa wavumilivu na wastahamilivu na waendelee na shughuli zao za
maisha za kila siku kwa amani.
Ndugu
Wananchi,
Kudumishwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar
ambayo leo yametimiza miaka 52, lazima kwende sambamba na kudumishwa na
kuendelezwa kwa Muungano wa Tanzania ambao ifikapo tarehe 26 Aprili mwaka huu
wa 2016, utatimiza miaka 52 tangu kuasisiwa kwake. Muungano wa Tanzania ni kielelezo muhimu cha
umoja wa Watanzania na udugu wa damu uliopo tangu kale na dahari kwa wananchi
wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kipindi chote tangu
kuasisiwa kwake tarehe 26 Aprili, 1964, wananchi wameendelea kunufaika
kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kujitokeza changamoto ambazo zimekuwa
zikifanyiwa kazi kwa ufanisi mkubwa na Kamati ya pamoja katika Ofisi ya Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Nne.
Napenda nimhakikishie Mheshimiwa John
Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania na wote
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Awamu ya Saba, itaendelea kuwa muumini wa dhati wa Muungano wa Tanzania na
kuendelea kuyatekeleza kwa vitendo kwa malengo yale yale ya Waasisi wetu, Marehemu baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Ndugu
Wananchi,
Mafanikio tunayoyapata yanatokana na
kuwepo kwa hali ya amani na utulivu nchini.
Natumia fursa hii kusisitiza kauli yangu niliyoitoa tarehe 26 Juni, 2015
katika hotuba yangu ya kulivunja Baraza la Nane la Wawakilishi, kwamba ni
jukumu la viongozi wote wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa madhehebu ya dini,
viongozi wengine katika jamii na wananchi wote kutekeleza wajibu wetu na
kuhakikisha tunadumisha amani na utulivu na kufuata sheria. Sote tuna wajibu mkubwa wa kuitii Katiba ya
Zanzibar na Sheria zake na kutambua kuwa ni msingi muhimu wa kulinda na
kuendeleza amani na utulivu wetu.
Katika kipindi chote cha Uongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya saba, nimeridhishwa sana na kazi
nzuri inayofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kusimamia amani na usalama nchini. Napenda niwahakikishie wananchi wote kuwa
Serikali zetu zote mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuchukua hatua madhubuti katika
kuhakikisha kuwa amani, utulivu na usalama vinaendelea kudumishwa nchini.
Nchi yetu inaongozwa kwa Katiba na Sheria na hivyo hakuna mtu au taasisi
yoyote iliyo juu ya Katiba na Sheria.
Kwa mnasaba huo, suala la kutii Sheria na Katiba ya nchi halina mbadala
wala mjadala.
Ndugu
Wananchi,
Kwa niaba yenu natoa shukurani kwa nchi
rafiki, mashirika ya Kimataifa na washirika wetu wote wa maendeleo kwa
kushirikiana nasi katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo. Napenda nikiri kuwa mafanikio tuliyoyapata,
yametokana na jitihada zetu za pamoja katika utekelezaji wa mipango yetu ya
maendeleo kwa kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii. Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inathamini ushirikiano wetu na itauendeleza kwa lengo la
kupiga hatua zaidi za maendeleo.
Natoa shukurani zangu tena kwa Viongozi
wote waliohudhuria katika sherehe hizi wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Natoa shukurani
Maalum kwa Wasaidizi wangu; Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad
na Mhe. Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kwa kunisaidia kuiongoza
Zanzibar kwa mafanikio. Aidha, nawashukuru Mawaziri wote, Makatibu Wakuu,
Wakurugenzi, Viongozi mbali mbali wa Serikali na Wafanyakazi wote kwa jitihada
zao katika kuwatumikia wananchi.
Ndugu
Wananchi,
Nakamilisha hotuba yangu kwa kutoa
shukurani na kuipongeza Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa inayoongozwa na
Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kazi nzuri iliyofanywa
ya kuyafanikisha maadhimisho ya mwaka huu.
Navipongeza kwa dhati Vikosi vyote vya Ulinzi kwa gwaride zuri lenye
ukakamavu. Nawashukuru washiriki wote wa
Maandamano na vikundi vya sanaa na burudani vilivyotumbuiza na kuongeza hamasa
katika siku hii ya kilele. Kadhalika, natoa shukurani zangu kwa waandishi wa habari
na wamiliki wa vyombo vya habari kwa kuzitangaza sherehe zetu kwa ufanisi mkubwa
tangu tulipoanza tarehe 3 Januari, 2016.
Natoa shukurani zangu maalum kwenu wananchi
nyote kwa kushiriki kwa wingi katika matukio mbali mbali tokea tulipoanza
Sherehe za Maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi na leo katika siku hii ya
kilele. Aidha, nakushukuruni kwa
kuonesha umoja na mshikamano na kushereheka Sherehe hizi kwa amani, hamasa
kubwa na uzalendo. Hiki ni kielelezo
muhimu kwamba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla tunayaenzi na tunayadumisha
Mapinduzi kama ni msingi muhimu wa uhuru wetu na maendeleo ya nchi yetu.
Tuendelee kusimamia amani, umoja na mshikamano ambazo ni nguzo muhimu kwa
maendeleo yetu. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe nguvu za kuitekeleza mipango yetu
ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Nakutakieni kheri na baraka
za mwaka mpya wa 2016.
MAPINDUZI
DAIMA
MUNGU
IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU
IBARIKI TANZANIA
MUNGU
IBARIKI AFRIKA.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment