Habari za Punde

Ujenzi wa nyumba za ZSSF unaendelea vizuri Mbweni

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Nyumba za Mkopo unaotekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF }hapo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.Wa kwanza kutoka kushoto  ni Msanifu Majengo anayesimamia Mradi huo Bwana Mahsen Mahd  na Waziri wa Fedha Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee  na kushoto ya Balozi Seif ni Meneja Mipango,Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Nd. Khalifa Muumin Hilal  na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud.

Balozi Seif akiangalia ramani ya Nyumba zinakavyojengwa akiwa pamoja na Waziri wa Fedha Kushoto yake Mh. Omar Yussuf Mzee, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Nd. Abdulwakil Haji Hafidh na Meneja Mipango,Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Nd. Khalifa Muumin Hilal.

 Muonekano wa Ramani ya mandhari ya nyumba zitakavyokuwa baada ya ujenzi wake.
 Baadhi ya Majengo yaGhorofa yatakavyosimama baada ya kukamilika kwa ujenzi wake hapo Mbqweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.


 Baadhi ya Majengo yaGhorofa yatakavyosimama baada ya kukamilika kwa ujenzi wake hapo Mbqweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
  Harakati za ujenzi kwa hatua ya Msingi { Jamvi } inaendelea kwa kasi hapo Mbweni unaoendeshwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar      { ZSSF }.

Wahandisi wa ujenzi wa Nyumba za Mkopo za ZSSF Mbweni wanaonekana wakiwa katika harakati za kusuka nondo kwa ajili ya kumwaga zege kwa hatua ya kukamilisha  Msingi wa Mjengo ya awamu ya kwanza.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Harakati za ujenzi wa  Nyumba za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } zilizoanza Mwezi Septemba mwaka uliopita  kwa lengo la kuwakopesha wanachama wake pamoja na wananchi watakaohitaji kununua Nyumba hizo zinaendelea vyema katika eneo la Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Wazo la kuanzishwa kwa mradi huo lililobuniwa karibu miaka minne iliyopita  lilianza kutoa matumaini  ndani ya ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya katika Jimbo la Seattle Nchini Marekani  mwishoni mwa mwaka 2013 alipoambatana na Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar  kwa nia ya kuutangaza mradi huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Nd. Abdulwakil Haji Hafidh alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika eneo la Mradi huo kujionea maendeleo ya ujenzi wake.

Nd. Abdulwakil alisema mradi huo utakaokuwa na Mabloki 18 ya Majengo ya Ghorofa Saba zenye Fleti 252 utajengwa kwa awamu tatu tofauti  zinazotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni Arubaini na Sita { 46,000,000,000/- } hadi kukamilika kwake.

Alisema wajenzi wa mradi huo Kampuni ya Dezo Civil Construction yenye Makao Makuu yake Jijini Dar es salaam  wameanza na awamu ya kwanza itakayohusisha  Mabloki Matano yenye Nyumba 70 ambapo  wahitaji wa nyumba hizo tayari wameanza hatua ya kujitokeza kwa kuwasilisha maombi yao kwa Uongozi wa ZSSF.

Nd. Abdulwakil alimfahamisha Balozi Seif kwamba mipango  maalum imeshaandaliwa ya  jinsi nyumba hizo zitakavyotoa huduma ambapo alisema zipo zikakazouziwa wanachama na wateja moja kwa moja, nyengine zitakodishwa kwa wateja ambao baadaye watakuwa na uwezo wa kuzinunua.

Alisema utaratibu mwengine utaandaliwa ili kuwapa fursa wanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii wenye kipato kidogo kukopeshwa nyumba hizo kupitia udhamini wa Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } ambapo mteja anaweza kutumia kiinua mgongo chake kwa kulipia nyumba atakayoihitaji.

“ Ujenzi wetu tumeupanga kuutekeleza kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza tutajenga Bloki Tano, ile ya Pili pia tutajenga Bloki Tano na ya mwisho tutamalizia kwa Bloki Nane “. Alisema Mkurugenzi huyo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.

Naye Meneja Mipango,Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Nd. Khalifa Muumin Hilal  alisema huduma zote zinazohitajika kuzipata mwanaadamu zitawekwa kwenye majengo hayo ili kumuondoshea usumbufu Mwanachama wao.

Nd. Muumin alisema Majengo hayo yatajumuisha  Maduka ya bidhaa mbali mbali, sehemu za burdani ya watoto wa familia zitakazoishi sehemu hiyo pamoja na eneo maalum litakalotengwa kwa ajili ya maegesho ya vyombo vya moto sambamba  na eneo la michezo tofauti.

Alisema ukumbi wa Kisasa utakaokuwa na uwezo wa kuhudumia watu mia 500 kwa wakati mmoja pia utajengwa katika eneo hilo ili utoe  huduma kwa Taasisi na mashirika mbali mbali yatakayohitaji ukumbi kwa ajili ya Mikutano yao ya  Kitaifa ama  Kimataifa .

Kwa upande wake Msanifu Majengo anayesimamia Mradi huo Bwana Mahsen Mahd alifafanua kwamba ujenzi wa majengo hayo unazingatia taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwashirikisha wataalamu wa Taasisi za ujenzi pamoja na watendaji wa Baraza la Manispaa.

Bwana Mahd alisema usanifu wa majengo yote yatakayojengwa katika eneo hilo utakwenda sambamba na vigezo vinavyokubalika  na kutumiwa katika majengo ya Kimataifa.

Akielezea matumaini yake kutokana na hatua nzuri ya maendeleo ya mradi huo wa Nyumba  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushauri Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya  Jamii Zanzibar kuhakikisha kwamba  viwango vya nyumba zinazojengwa vinakuwa na fursa pana ya kuwafaidisha wanachama wa Mfuko huo wenye Vipato tofauti.

Balozi Seif alisema hatua hiyo itasaidia kuleta faraja kwa wanachama wa ngazi zote watakaokuwa na nia ya kutaka kununua, kukodi au kukopeshwa nyumba hizo kwa mujibu wa uwezo aliokuwa nao  muhusika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar kwa uamuzi uliochukuwa wa kuwekeza katika miradi ya Jamii ambayo itasaidia kustawisha maisha ya kila siku ya wananchi.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.