Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Jumla ya Wananchi 1,572 wa Vijiji vya Michamvi Pingwe na
Michamvi Kae wanatarajiwa kupata Maji safi na salama
baada ya kukamilika kwa Mradi wa kuchuja Maji Chunvi
kuwa Maji matamu.
Kukamilika kwa mradi huo kutawapunguzia Kero wananchi
wa Vijiji vya Michamvi ambao kwa miaka mingi
wamekumbwa na tatizo hilo bila ya msaada wowote.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Uwezeshaji, ustawi wa
Jamii,Vijana Wanawake na Watoto Zanzibar Zainab Omar
Mohammed wakati akiweka Jiwe la Msingi la Mradi huo
huko Michamvi wilaya ya Kusini Unguja.
Amesema uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Mradi huo na
kupata maji matamu ambayo yatawasaidia wananchi hao ni
moja kati ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kwa lengo la kuwaondoshea shida ya upatikanaji
wa maji wananchi wake.
“Malengo makubwa ya jitihada hizo ni kuwaondoshea kero
Wananchi ya kukosekana kwa huduma hiyo ya maji safi ili
waweze kushughulikia zaidi kazi za uzalishaji mali na
maendeleo kwa lengo kuimarisha kipato chao” amesema
Waziri Zainab.
Ameongeza kuwa eneo la Michamvi ni moja kati ya maeneo
yanayokabiliwa na upatikanaji wa maji safi na salama na
kwamba baada ya muda mfupi wananchi wataondokana na
kero hiyo.
Akitoa taarifa juu ya Mradi huo Naibu Katibu mkuu Wizara
ya Ardhi, Makaazi,Maji na Nishati Mustafa Jumbe amesema
Mradi umetekelezwa na kugharamiwa kati ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya UST kutoka Ujerumani
ambapo jumla ya Shilingi Millioni 475 za Kitanzania
zinatarajiwa kutumika.
Amefafanua kuwa Kampuni ya UST imechangia Milioni 395
ambapo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi kwa
kushirikiana na Wananchi wamechagia Millioni 80.
Jumbe amezitaja kazi zitakazofanyika kuwa ni pamoja na
uchimbaji wa kisima,utiaji wa pampu,ujenzi wa kibanda cha
kuwekea mitambo na ununuzi wa mitambo ya kusafishia
maji chumvi kuwa matamu.
Akitoa nasaha Mkuu wa Wilaya ya Kusini Jabir Khamis
Makame amewaomba wananchi wa Michamvi kuuenzi Mradi
huo ili uweze kuwaletea matunda yaliyokusudiwa.
Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Kuchuja maji Chumvi
kuwa Maji matamu ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya
Zanzibar ambayo lengo lake ni kuwakombo Wananchi na
Umasikini ikiwemo kuwaletea maji safi na salama katika
maeneo yao.
No comments:
Post a Comment