Habari za Punde

Jumuiya ya Maradhi ya Saratani Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Saratani Duniani kwa Mkutano na Waandishi wa Habari.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi ya saratani Zanzibar Dkt. Msafiri  Marijani akizungumza na waandishi wa habari katika  Ofisi ya Jumuiya hiyo Mpendae ikiwa ni maadhimisho ya siku ya saratani duniani, kushotoni kwake ni Mkurugenzi wa Utumishi na uendeshaji Wizaraya ya Afya,
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi ya saratani  Zanzibar  kwenye maadhimisho ya siku ya saratani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Utumishi na uendeshaji Wizaraya ya Afya Zanzibar ndugu Omar Mwinyi Kondo akizungumza na waandishi katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani yaliyofanyika Ofisi ya Jumuiya Mpendae.
Viongozi ya Maradhi ya Saratani wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani ndugu Omar Mwinyi Kondo (kati) mwenye suti na baadhi ya viongozi na waandishi wa habari waliohudhuria.
     Picha na Makame Mshenga Maelezo 


Na. Ramadhani Ali /Maelezo Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi ya Saratani Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani ameitanabahisha  jamii kwamba maradhi ya saratani  yamekuwa janga linalosumbua  dunia  nzima kwa sasa na kila mmoja anawajibu wa kusaidia katika   kukabiliana na maradhi hayo sugu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Jumuiya hiyo Mpendae nje kidogo ya Mjini Zanzibar,  ikiwa ni maadhimisho ya siku ya saratani duniani, Dkt. Marijani amesema  mtu anaweza kujikinga na maradhi hayo iwapo hatua za mapema  zitachukuliwa.

Amezitaja hatua zinazopaswa kuchukuliwa  na  wananchi  katika kukabiliana na saratani kuwa ni kujenga  mwamko wa kuchunguza afya  mara kwa mara ili kugundua mapema iwapo  mtu anazo dalili za maradhi hayo.

Amesema hatua nyengine ni kuacha kutumia bidhaa zinazotokana na tumbaku, ulevi wa kupindukia, kupunguza matumizi ya mafuta kwenye  chakula, kutumia zaidi  vyakula vya matunda na mbogamboga na kujenga tabia ya kufanya mazoezi kila siku.

Dkt. marijani amewakumbusha wananchi kuwa saratani ni uvimbe mpya kwenye mwili na baada ya muda mfupi  huzalisha chembechembe  zinazosababisha athari kubwa na kama haikuwahiwa mapema inasababisha donda kubwa na kuwa halitibiki tena.

“Saratani  inaweza kuzuilika   iwapo itawahiwa mapema, tuongezeni nguvu kukabiliana nayo  vyenginevyo inaweza kuathiri wananchi wengi kwani gharama ya matibabu yake ni kubwa na wagonjwa  wengi  hushindwa na kupoteza maisha,” alisisitiza Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Amesema saratani ya matiti na shingo ya kizazi  ndizo  zinaongoza kwa   wanawake   Zanzibar na saratani ya tenzi dume inaongoza kwa  upande wa wanaume.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya  maradhi ya Saratani Zanzibar,  ambae ni Daktari bingwa  wa uchunguzi wa saratani, amewaeleza waandishi wa habari kwamba mpaka hivi sasa hakuna takwimu rasmi za wagonjwa wa maradhi hayo Zanzibar lakini Hospitali ya Ocean Road ya Dar es salaam imekuwa ikipokea wagonjwa 1,000 kila mwaka kutoka Zanzibar  mbali na wagonwa wengine wanaopelekwa nje ya nchi  na wanaobakia majumbani kupatiwa dawa mbadala.

Amesema kutokana na kadhia hiyo  mwaka 2013 ilianzishwa Jumuiya ya kupambana na saratani  Zanzibar ikiwa na lengo la kutoa elimu  kwa jamii  juu ya njia za kujikinga na kuishauri serikali njia zinazofaa kupunguza ongezeko la maradhi hayo.

Ameitaka Serikali kuongeza wataalamu  na dawa za kupunguza maumivu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja na hospitali  nyengine za Zanzibar  kwani zimekuwa hazitoshi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji Wizara ya Afya Ndugu Omar Mwinyi Kondo amewapongeza wanachama wa Jumuiya hiyo kwa juhudi kubwa wanayochukua kuelimisha jamii kujikinga na saratani.

Amewahakikishia viongozi wa Jumuiya hiyo kwamba Serikali itaanzisha utaratibu  rasmi wa kuwasajili wagonjwa wa saratani na kuongeza huduma za matibabu Hospitali kuu ya Mnazimmoja hasa dawa za kupunguza maumivu na wataalamu.

ujumbe wa mwaka huu katika siku ya saratani duniani ni mimi na wewe tunaweza kujikinga na saratani. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.