Habari za Punde

TPB Yakabidhi Shule Vyoo vya Thamani ya Tsh. Milioni 4.7

 Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua vyoo vyenye matundu 14, vitakavyohudumia wanafunzi 850 katika shule ya Msingi ya Makambi, Songea Mkoa wa Ruvuma, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 4.7 kulia ni Meneja wa Oparesheni wa tawi la Songea, Simon Mlelwa.
 Wanafuzni wakishangilia kupata vyoo
 Noves akibadilishana mawazo na baadhi ya walimu na wazazi
 Sehemuya vyoo hivyo

 Wanafunzi wa shule ya msingi ya Makambi iliyopo Kata ya Ndilima Litembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakifurahia vyoo vya kisasa vilivyojengwa na Benki ya Posta Tanzania.



Na Mwandishi wetu, Songea
BENKI ya posta Tanzania, TPB, imekabidhi vyoo vyenye thamani ya shilingi milioni 4.7 kwa shule ya msingi Makambi iliyoko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akikabidhi vyoo hivyo vyenye matundu 14 vilivyojengwa na benki hiyo ili kusaidia kuondokana na upungufu wa vyoo kwenye shule hiyo mwishoni mwa wiki, Meneja mahusiano na mawasiliano wa TPB, Noves Moses, alisema msaada huu wa benki ni sehemu ya mchango kwa jamii katika kuboresha miundombinu ya shule na hivyo kufikia lengo la kutoa elimu bora hapa nchini.
Kwa kutambua juhudi za Rais za kutoa elimu bure kwa wanafunzi kote nchini, ambapo kumekuwepo na ongezeko kubwa sana la wanafunzi, benki ya posta inayofuraha kuunga mkono juhudi za Mh.Rais na msaada huu wa vyoo utasaidia kuweka mazingira bora ya utoaji elimu lakini pia mahudhurio ya wanafunzi, alisema Noves.
Alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wadau wa elimu kulichukulia suala la elimu bure kama kigezo cha kutokuchangia sekta hiyo na baadala yake wanadai ni kazi ya serikali pekee jambo ambalo siyo sahihi katika uboreshaji elimu.

“Suala la elimu bure lisiwe kigezo cha wadau kushindwa kuichangia sekta hiyo kwani kufanya hivyo kunapelekea baadhi ya shule kushindwa kuwa na mazingira mazuri ya watoto kujisomea pamoja na walimu wao kutokuwa na morali ya kufundisha” alisema Meneja huyo wa mahusiano na mawasiliano.
Noves alisema kuwa Benki ya Posta Tanzania inafanya kazi kwa kiwango kikubwa na serikali hivyo imetoa misaada mbalimbali ya kijamii hasa kwa upande wa afya na elimu huku katika upande wa elimu wamechangia madawati na ujenzi wa vyoo bora vya kisasa kwenye shule mbalimbali hapa nchini .
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Kanisius Ngongi awali akitoa taarifa ya shule hiyo kabla ya kukabidhiwa vyoo hivyo alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 850 na matundu ya vyoo yapo 14 na kuwa vyoo vyote vina maji ya kutosha.
Ngongi aliipongeza benki hiyo alisema kuwa shule hiyo kwa sasa imeshabadilika, mazingira yamekuwa bora kwa upande wa vyoo vya wanafunzi ambavyo kwa sasa hakuna shule ndani ya Manispaa hiyo yenye vyoo kama hivyo.
Mwalimu Ngongi alisema kuwa licha ya vyoo vya wanafunzi kuwa bora lakini bado kuna changamoto ya vyoo vya walimu maana vyoo walivyokuwa wakivitumia vimeshapoteza ubora wake na kuwafanya walimu hao kupata shida mahala pa kujisitili hivyo amewaomba wadau mbalimbali waweze kuchangia kama Benki ya Posta inavyojitolea.
Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua vyoo vyenye matundu 14, vitakavyohudumia wanafunzi 850 katika shule ya Msingi ya Makambi, Songea Mkoa wa Ruvuma, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 4.7 kulia ni Meneja wa Oparesheni wa tawi la Songea, Simon Mlelwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.