Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Viongozi wa Umoja wa Rufaa za Wananchi Tanzania

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Umoja wa Rufaa za Wananchi Tanzania Ukiongozwa na Bwana John Shibuda.

 Balozi Seif akifafanua jambo mbele ya Mwenyekiti wa Umoja wa Rufaa za Wananchi wa Tanzania Bwana John Shibuda aliyeuongoza ujumbe wa Umoja huo kufanya ziara ya siku mbili Zanzibar.
Mjumbe wa Umoja wa Rufaa za Wananchi Tanzania kutoka Chama cha UDP  Bwana John Momos Cheyo wa kwanza kutoka kulia akielezea malengo la Umoja huo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Viongozi wa Umoja wa Rufaa za Wananchi Tanzania umewaomba Wazanzibari kwenda kukamilisha haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura kwa kuwachagua Viongozi  wanaowataka kuwaletea maendeleo kwenye uchaguzi Mkuu wa marejeo wa Zanzibar unaotarajiwa kufanyia Jumapili ya Tarehe 20 mwezi huu.

Kauli hiyo imetolewa na Ujumbe wa Viongozi  saba  wanaotoka vyama vidogo vidogo vya Kisasa  Nchini Tanzania vilivyokuwa havimo kwenye  Umoja wa Ukawa ukiongozwa na Mheshimiwa John Shibuda wakati walipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Shibuda alisema kinachohitajika wakati huu kwa Taifa ni kuona watanzania wanaendelea kuishi kwa amani na ushirikiano utakaotoa nafasi pana kwa Wananchi wake kujikita zaidi katika uzalishaji mali badala ya kuhubiri Siasa.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vikosi vyake vya ulinzi kwa kulinda amani ya Zanzibar.


Bwana Shibuda aliwataka Wanachama wa vyama vya siasa, Viongozi pamoja na Wananchi kukamilisha zoezi la kupiga kura kwa amani na usalama ili lengo la kurejewa uchaguzi huo likamilike na kuleta mafanikio makubwa.

Alitahadharisha kwamba si vyema  wakati wa uchaguzi wakajitokea baadhi ya watu kutaka kuchezea matokeo ya kura jambo ambalo ni hatari na matokeo yake ni kwamba gharama za kuja kulinda vurugu ni ndogo.

Naye Mjumbe wa Umoja huo wa Rufaa za Wananchi  Tanzania Bwana John Momos Cheo alisema upigaji kura ya marejeo Jumapili ijayo ndio njia pekee itakayotoa mwanga kwa Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar kuamua wapi wanataka kuelekea katika mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

Akitoa shukrani zake  kwa Ujumbe huo wa Umoja wa Rufaa za Wananchi Tanzania, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Tume huru ya Uchaguzi Zanzibar { ZEC } haikufanya makosa kufuta uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Tarehe 25 Oktoba mwaka 2015.

Balozi Seif alisema yapo mambo tisa yaliyoainishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Bwana Jecha Salum Jecha ambayo yalichangia kuvuruga zoezi zima la uchaguzi na kufikia hatua ya kufuta uchjaguzi pamoja na matokeo yake yote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Ujumbe wa Viongozi hao wa Umoja wa Rufaa za Wananchi Tanzania kwamba Serikali itaendelea kusimamia amani ili kuona zoezi hilo  la uchaguzi linakamilika kwa utulivu.

Balozi Seif alisema jukumu hilo la Serikali limelenga kuona Maisha ya kila siku yanatoa nafasi kwa Wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kimaisha kama kawaida.

Ujumbe huo wa Umoja wa Rufaa za Wananchi uliofanya ziara ya siku mbili Zanzibar umejumuisha Viongozi wa Kisiasa wa vyama visivyokuwa ndani ya Ukawa vya UPDP, SAU, UDP na ADATADEA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.