Habari za Punde

DPP, ayarejesha mafaili ya uchomaji moto Polisi, hadi wakamilishe uchunguzi

Haji Nassor na Hassan Khamis, Pemba
JUMLA ya majalada tisa ya tuhumza za uchomaji moto nyumba, majengo ya chama na serikali, yanayowahushishwa watuhumiwa 29, wa mikoa miwili ya Pemba, yamerejeshwa na Afisi ya Mkurigenzi wa Mashitaki, kwa Jeshi la Polisi, hadi watakapokamlisha ushahidi wa mashauri hayo.
Awali Jeshi la Polisi Mkoani wa Kaskazini Pemba, baada ya kuwasaka na kuwatia mbaroni washukiwa 21 wa makosa hayo, juzi Machi14, waliwafikisha mbele ya afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka tayari kwa ajili ya kufungiliwa kesi, ingawa hilo halifanikiwa.
Kama ilivyo kwa Mkoa wa kaskazini Pemba, pia Jeshi la Polisi kusini Pemba, nalo liliwafikisha mbele ya Afisi ya Mkurugenzi wa mashitaka watumiwa nane (8) wakiwa na majalada manne, tayari kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka ingawa jawabu ilikuwa sawa sawa.
Akizungumza kwa njia ya simu mwanasheria dhamana wa afisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Pemba Al-baghir Yakout Juma, akiri kuwa, afisi yake ilipokea majalada hayo tisa, matano yakiwa ya Mkoa wa kaskazini yenye washukiwa 21, na manne ya Mkoa wa kusini yakiwa na washukiwa nane (8) ingawa kisha waliyarejesha tena Jeshi la Polisi kwa upelelezi.
Baghiri alisema, jeshi la Polisi linapopata kesi za jinai wasiwe na haraka ya kutaka kufunguliwa kwa kesi na kisha watuhumiwa kupelekwa rumande, ni vyema wakakamilisha upepelezi ili kesi ziwe na uhakika wa kufanikiwa zinapofunguliwa.

“Unajua mwandishi, hii dhana ya upelelezi kwanza, inafaida kubwa na wala wananchi na Jeshi la Polisi, wasitutafsiri vibaya, na kuona kama vile hatutaki kuwatia hatiani makosaji wa makosa ya jinai, la hasha”,alifafanua.
Hivyo ameliomba Jeshi hilo kuharakisha upelelezi huo, na kisha kuyafikisha majalada hayo afisini kwao, na kama ikionekana kuna kesi, watawafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.
“Unajua kesi za jinai sio kama papai kwamba baada ya muda linaharaibika, sasa wafanye upelelezi tu hata miaka mingapi, ijayo wakimaliza, tunashirikiana na kuwapandisha mahakamani’’,alifafanua.
Kwa upande wake Mkuu wa upelelezi wa mkoasa ya jinai Mkoa wa kaskazini Pemba, afande Issa Juma Suleiman alikiri kupokea agizo hilo kutoka kwa afisi ya DPP, na tayari wapelelezi wameshaanza kuingia mitaani kukusanya ushahidi.
“Ni kweli tumepokea agizo hilo, na sasa hatuna budi kufanya upelelezi na tukikamilisha kama tataribu zinavyotaka tunakwenda nao tena watuhumiwa hawa mahakamani’’,aliweka wazi.
Alipoulizwa kwamba kwa sasa watuhumiwa hao wako wapi, alijibu bado wanawashikilia na kwa sasa wanaanda barua maalumu, ili kuiomba mahakama kuwapa mamlaka ya kuwanao hadi hapo baadae.
“Sisi tunauwezo wa kuiomba mahakama kwamba hawa watuhumiwa tuendelee kuwashikilia hadi hapo baadae, au kuwaachia kwa dhamana, lakini idadi ya siku ya kuwa nao watasema mahakama baada ya kuwaomba hiyo idhini’’,alifafanua.
Watuhumiwa wa uchomaji wa tawi la CCM, nyumba za makaazi ya watu, kituo cha afya Kiuyu kufikishwa mahakamani na shauri lao kushindwa kufunguliwa ni Maulid Said (22), Haji Hamada Haji (35), Mohamed Rashid Ali (36), Ali Hamad Ali (40), Iddi Khamis Suleiman (46), Nassor Khatib nassor, (25) wote wakaazi wa Makangale.
Wengine ni Omar Hamad Othaman (60), Mussa Ali Ali (25) na  Khamis Juma Khamis (46) ambae nae ni mkaazi wa kijiji hicho ambapo wote kwa pamoja wanashutumiwa kwa uchomaji nyumba moto tukio lililotea usiku wa kuamkia Machi 12 mwaka huu Makangale.
Wengine ambao walikishwa mahakamani juzi bila ya shauri lao kufunguliwa kwa madai kama hayo, Haji Bakari Mtwana (51) na  Awesu Shamte Said (57) wote wakazi wa Msuka, Makame Suleiman Makame (35), Ali Bakari Mtwana (35) wote wakaazi wa Makangale.
Kundi jengine la watuhumiwa wanaohusishwa na makosa ya uchomaji moto kati ya hao 21 ni Ramadhan Hamad Faki (56), Mohamed Said Mbarouk (24), Yussuf Juma Omar ambao wote ni wakaazi wa kijiji cha Msuka.
Aidha Jeshi hilo la Polisi limeshafinikiwa kuwanasa watuhumiwa wengine watatu wa uchomaji moto nyumba mbili za shehia ya Kangagani akiwemo Kombo Hassan Salim (20), Khamis Hamad Haji (26) na Khalfan Bakar Hamad (20) ambao wote ni wakaazi wa shehia hiyo.
Wengine wawili ambao nao jalada lao lilirejeshwa tena Jeshi la Polisi kwa upelelezi wa kina  ambao wanakabiliwa na tuhuma za kutia moto kituo cha afya cha Kiuyu, ni Hassan Mikidadi Hamad (30) na Ali Mikidadi (25) wote wakaazi wa Kiuyu Minuwgini wilaya ya Wete.
Wakati huo huo nalo Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba, linaendelea kuwahoji washukiwa nane wa kutokana na matukio manne ya uchomaji moto yaliotokezea wilaya za Mkoani na Chakechake likiwemo tawi la CCM Tibirinzi na nyumba ya Naibu sheha wa shehia ya Ziwani bibi Maza Borauzima Nduti,
Mkuu wa upelelezi wa mkoasa ya jinai Mkoa wa kusini Pemba Ali Hamada, alisema awali waliwashikilia watuhumiwa 10, ingawa wawili wameshawaachia baada ya upelelezi kuonyesha hawahusikia na matukio hayo manne.
“Wawi tumewaachia kwanza, na hawa wanane twaendelea kuwa hoji na baadae tukihisi wanahusika na matukuo hayo, basi tutawafikisha Mahakamani kwa hatua za kisheria’’,alifafanua.

Juzi usiku wa kuamkia Machi 12 mwaka huu Kisiwa cha Pemba kilikumbwa na matukio manane ya uchomaji maoto, ikiwa ni pamoja na nyumba za wananchi, matawi ya na maskani ya CCM pamoja na kituo cha afya Kiuyu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.