Na Othman Khamis OMPR.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na jitihada kuongeza idadi ya Wanawake katika vyuo na Taasisi ya Elimu ya juu Nchini ili kiwango cha wanawake wenye elimu ya juu kikue kila mwaka hasa katika elimu ya sayansi na ufundi.
Ongezeko hilo litakwenda sambamba na kipaumbele cha kuwapatia mokopo ya elimu ya juu pamoja nakuanzishwa program mbali mbali za kuwainua kielimu watoto wa kike hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Dunia zinazofikia kilele chake kila ifikapo Tarehe 8 Mwezi Machi ya kila Mwaka ambazo zimefanyika katika viwanja vya Kituo cha Simulizi Asili, Tamaduni na lugha za Afrika { Eacrotanal } Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ni ukweli usiofichika kwamba wanawake kutokana na umakini na umahiri mkubwa walionao ni dhahiri kwamba wakipatiwa fursa na haki zao kikamilifu ikiwemo elimu wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo ya Taifa.
Alisema wanawake wanaokadiriwa kufikia asilimia 51.6 % ya watu wote wa Zanzibar kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2012 wanawake ndio wanaotunza na kuziendeleza familia, lakini wengi wao hawana uwezo wa kutosha wa kuzihudumia familia zao.
Balozi Seif alitoa wito kwa Taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwasimamia vyema wanawake ili kuwajengea uwezo utakaosaidia akinamama hao kubeba jukumu lao la kuhudumia familia, lakini pia kuleta maendeleo ya Taifa kwa jumla.
Alisisitiza umuhimu wa changamoto ya umiliki wa rasilmali unaowakumba wanawake wengi kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili waweze kuwa na uhakika kwa kuziendesha familia zao zinazowalazimu.
Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba wanawake walio wengi hawapati fursa ya umiliki wa rasilmali zao kutokana na mfumo dume uliojengeka ndani ya jamii ukiwemo ule wa uelewa mdogo wa wanawake wa kutambua haki zao na kuzifuatilia.
“ Suala ya umiliki mdogo wa rasilmali kwa wanawake ambayo ndio nyenzo muhimu ya kujikomboa kimaisha ni miongoni mwa changamoto zinazozorotesha maendeleo yao katika Nyanja zote ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukuwa juhudi za kubuni mbinu, mikakati na kuandaa fursa mbali mbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Alisema zipo Taasisi zilizoundwa na kuanzishwa zikijikita katika kuhamasisha na kuwajengea uwezo wanawake katika nyanja mbali mbali ikiwemo ujasiriamali, uongozi, umiliki wa rasilmali ndogo na kubwa katika jamii lengo likiwa ni kuwawezesha wanawake kuthubutu kumiliki rasilmali zilizoizunguuka Jamii.
Akizungumzia tatizo la udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba zaidi wanawake na Watoto Balozi Seif Serikali Kuu imedhamiria kupambana na kadhia hiyo ya udhalilishaji inayolitia aibu Taifa na kufikia hatua ya kuanzisha kampeni kubwa ya kupambana na maovu hayo karibu mwaka mmoja uliopita.
Balozi Seif alieleza kuwa upo udhaifu unaojitokeza wakati wa mapambano dhidi ya udhalilishaji ambao iwapo Viongozi, watendaji wa Taasisi zinazosimamia sheria pamoja na Wananchi hawakushirikiana pamoja, majambazi wa matendo hayo wataendelea kutamba na jamii itafikia hatua ya kudhania kama hakuna Serikali.
Alionya kwamba tabia ya kufichiana vitendo vya udhalilishaji pamoja na kusuluhisha makosa hayo inayofanywa na baadhi wabakaji ndani ya familia na mwanya wa kupoteza vielelezo unakosesha ushahidi uliokamilika wa kuwatia hatiani madhalimu wa maovu hayo.
Alifahamisha kwamba ushirikiano wa pamoja kati ya taasisi zote na jamii kwa jumla ndio utakaochangia kumaliza tatizo hilo la udhalilishaji wa kijinsia wa wanawake na watoto hapa Zanzibar na kulirejeshea heshima yake ya Kihistoria Taifa hili.
Katika risala yao wanawake hao iliyosomwa na Bibi Hadia Mohammed Ramadhan alisema wanawake Nchini hawaridhiki na utendaji wa watumishi wa Mahakama, Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka ambao umekuwa ukiwakosesha amani na furaha ya maisha.
Bibi Hadia alisema usalama wa wanawake na watoto hivi sasa uko mashakani kutokana na kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia unaendelea kufanywa na baadhi ya watu Mitaani bila ya kuwa na hofu yoyote.
Alisema tabia ya waovu hai imezidi kupanda batra kutokana na maamuzi ya watumishi wa taasisi hizo kushindwa kutoa maamuzi yanayoleta faraja kwa watoto na wanawake waliodhalilishwa katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Wakitoa salamu kwenye kilele cha maadhimisho hayo ya siku ya wanawake Duniani Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu {UNFPA }Dr.Natalia Kamem, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake { UN WOMEN } Lucy Tesha pamoja na Yule wa Shirika la kuhudumia Watoto { Save the Children } Bwana Rashid Mohammed Hashim wameahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kuwajengea uwezo Wanawake.
Wawakilishi hao walisema haki ya kila mtu haitegemei jinsia yake bali ni uwezo wake katika kuihudumia jamii iliyomzunguuka na kinachohitajika kwa Mataifa na Taasisi za Kijamii ni kuhakikisha zinatoa huduma sawa hasa zile za elimu kwa watu wote na kuacha tabia ya kiuendeleza mfumo dume uliozoeleka.
Walisema ushiriki wa wanawake katika maeneo ya uzalishaji, ajira pamoja na kazi za ujasiriamali ndio njia pekee itakayoifanya dunia inaendelea kuwa na amani na utulivu.
Katika maadhimisho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Mikopo yenye Thamani ya shilingi Milioni 31,125,000/- kwa vikundi 13 vya ujasiriamali vya wanawake kutoka Mikoa yote ya Unguja.
Vikundi hivyo ni pamoja na Kijicho cha Chura kutoka Mkele, Hima Hima Gulioni, Hatuyumbi Sebleni, Hakuna Kulala Group Sogea, Nia Njema Kidimni,Wasafi Group, Mola Tubariki Tazari, Heri Tufanikiwe Kidombo, Gamba Mpya, Nungwi Imara, Kidimni Cooperative, Tuaminiane Kimebe Samaki pamoja na Muungu yupo cha Welezo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata fursa ya kukagua maonyesho ya wajasiriamali wanawake kutoka vikundi tofauti vya miradi ya uzalishaji vya Wilaya za Unguja.
Balozi Seif alionyesha kuridhika na kazi kubwa inayotekelezwa na akina mama hao katika suala zima la kujiletea maendeleo yao kwa kupiga vita ukali wa maisha pamoja na kupunguza umaskini.
Ujumbe wa mwaka huu wa siku ya wanawake Duniani unasema “ Hakikisha usawa wa kijinsia kwa kuchukuwa hatua madhubuti ”. Ujumbe unaofanyiwa kazi na Mataifa wanachama ya Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa mazingira halisi ya Nchi husika.
Kwa upande wa Zanzibar, wanawake na washirika wake wameamua kuadhimisha siku hii ya wanawake Duniani kwa kuhimiza suala la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kwa kupitia Ujumbe unaosema. “ Wanawake ni wenza katika kukuza uchumi. Toa fursa sawa wamiliki rasilmali ”.
No comments:
Post a Comment