Habari za Punde

Wananchi Pemba Waaswa Kusajilini Ardhi Kuepusha Migogoro : ZLSC

Na Haji Nassor, Pemba
WANANCHI wa shehia ya Mihogoni Jimbo la Tumbe wilaya ya Micheweni Pemba, wametakiwa kusajili ardhi zao wakati utakapofika, ili kuzipandisha hadhi ardhi hizo na kujiepusha na migogoro ya umiliki.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, alipokua akijibu hoja za wananchi wa shehia hiyo, kwenye mkutano wa kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi hao.
Alisema suala la kusajili ardhi lipo kwa mujibu wa sheria, na wala halina hiari, bali wananchi hawana budi kujipanga kutekeleza zoezi hilo kwenye maeneo yao wakati utakapofika.
Mratibu huyo, alisema ardhi iliosajili huwa na thamani kubwa, maana humuwezesha mmiliki na hasa baada ya kukabidhiwa hati, kuingia kwenye mikopo mikubwa.
“Jamani suala la kusajili ardhi lipo kwenye sheria kwa muda mrefu sasa, na sisi wananchi wala tusiwe na mtazamo mbaya kwa serikali yetu, bali kila mmoja ahakikishe wakati ukifika anasajili’’,alisema.
Kwa upande wao Maafisa Mipango Kituo hicho, Khalfan Amour Mohamed na Mohamed Hassan Ali, waliwataka wananchi hao kuendelea kuwatumia wasiaidizi wa sheria waliopo majimboni ili kupata msaada wa kisheria bila ya malipo.
Khalfan, alisema wananchi wanapokumbwa na siuntafahamu ya masuala ya kisheria kabla ya kusafiri kwenda afisini kwao, kukaa pamoja na wasaidizi wa sheria masheha ili kuona wanapata ufumbuzi.
Nae Mohamed Hassan, alisema suala la ufahamu wa sheria linamuwajibia mwananchi mwenyewe, ambapo Kituo chao kipo kwa ajili ya kusaidia katika hilo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria kwenye mkutano, walisema wanawasiwasi kwamba hata wanapozifahamu sheria hado suala la kupata haki limekuwa zito.
Omar Kombo, alisema kwa mfano suala la vyeti vya kuzaliwa limekua zito kuanzia kwa masheha hadi wilayani, jambo ambalo wanadhani wanafanyia kwa makusudi.
“Mimi naamini wananchi hasa walioko vijijini wamekuwa wakifanyiwa hujma kwa makusdi, kwa vile tu wanaonekana wanaupungufu wa masuala ya elimu ya uraia’’,alifafanua Hussein Faki.
Akifunga mkutano huo sheha wa shehia ya Mihogoni Jimbo la Tumbe Salim Said Salim, alikipongeza Kituo cha Huduma za Sheria ZLSC kwa uamuzi wa kuwafuata wananchi kuwapa msaada wa kisheria.

Kituo hicho, kimekuwa na utaratibu wa kila wiki mara moja, kwenda katika vijiji kuwapa wananchi msaada wa kisheria bila ya malipo, ambapo tayari wananchi wa shehia za Ng’ambwa, Matale, Mjini wingwi na Mihogoni wamshafikiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.