Habari za Punde

Balozi Seif ashiriki kikao cha kuteua Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Mahonda

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Masheha, Madiwani, Wazee wanaoheshimika wa Jimbo la Mahonda katika Kikao cha Kuteua Kamati ya Maendeleo ya Jimbo hilo kilichofanyika Ofisi ya CCM Jimbo hilo iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B”.

  Baadhi ya Viongozi wa Jimbo la Mahonda waliokutana kuunda Kamati ya Maendeleo ya Jimbo hilo utakaoratibu Mfuko wa Jimbo unaolenga kuunga mkono nguvu za Wananchi kwenye miradi waliyoianzisha.
Balozi Seif akisisitiza jambo wakati akifafanua kifungu cha Sheria cha Baraza la Wawakilishi kilichoanzishwa cha kuanzishwa kwa mfuko wa jimbo ya mwaka 2012.

Picha na –OMPR – ZNZ.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ai Iddi alisema kwamba nia ya Serikali Kuu ya kuanzisha kwa mfuko wa Jimbo ni kusaidia nguvu za Wananchi katika kuunga mkono Miradi ya Kijamii na uchumi waliyoianzisha katika majimbo yao.

Alisema masharti makuu ya mfuko huo ni uwepo wa Kamati ya Maendeleo  itayoundwa rasmi kwa mujibu wa sheria ya Baraza la Wawakilishi Kifungu cha 9 cha kuwanzishwa kwa Mfuko wa Jimbo chini ya Uwenyekiti wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo linalohusika.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo katika Kikao Maalum alichokiitisha kuchaguwa wajumbe Tisa wa kuunda Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Mahonda Kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kiduni Wilaya ya Kaskazini “B”.


Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini nguvu na kazi kubwa inayofanywa na Wananchi wake wanaofikia hatua ya kuanzisha miradi ya kiuchumi, maendeleo na ile ya Kijamii ili kujikomboa na ukali wa maisha sambamba na kupunguza umaskini.

Alisema juhudi hizo za Wananchi ndizo zilizopelekea Serikali Kuu kupitia chombo chake cha kutunga Sheria yaani Baraza la Wawakilishi kuunda sheria ya kuanzishwa kwa mfuko wa Jimbo unaopatiwa fedha zinazolengwa kuunga mkono jitihada za Wananchi hao.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda alifafanua kwamba Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jimbo watakuwa na wajibu wa kutembelea miradi iliyoanzishwa na Wananchi katika Wadi na Shehia zao na baadae kuiwasilisha katika Kamati yao ya Maendeleo.

Alisema mfumo huo umewekwa ili kuipa nafasi Kamati kutafakari na kuichambua miradi iliyowasilishwa ili kupata fursa ya kutoa baraka zake kwa kuidhinisha mradi wa Wananchi utakaostahiki kuungwa mkono kupitia fedha za mfuko wa Jimbo.

Akizungumzia suala la Kipindupindu lililoikumba Taifa hivi sasa Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ili kuepukana na maradhi hayo ya kuambukiza, jamii lazima ikubali kubadilika katika kukabiliana na janga hilo kwa kuweka mazingira bora kwenye maeneo wanayoishi.

Aliwaagiza Viongozi wa Majimbo, Wadi na Shehia kuwatahadharisha Wananchi wa maeneo yao wakati wanapohisi mabadiliko ya afya zao kwa kuharisha au kutapika waharakishe kukimbilia kwenye vituo vya afya ili wapatiwe huduma za haraka kwa lengo la kujikinga na mripuko wa maradhi ya kuambukiza hasa Kipindupindu.

Balozi Seif alitanabahisha kwamba maradhi ya Kipindupindu yaliyochukuwa muda mrefu katika Historia ya maradhi hayo  hapa Zanzibar kwa kudumu takriban Miezi Saba sasa tayari yameshagusa Wilaya zote na kuathiri kila familia hapa Nchini.

“ Kipindipundu hivi sasa tayari kimeshagusa takriban Wilaya zote Nchini. Na kwa mujibu wa takwimu za siku mbili zilizopita kwenye Kituo cha Afya cha Chumbuni pekee kimepokea  na kulaza wagonjwa 88 hali ambayo jamii ndio yenye jukumu la kuyaondosha maradhi hayo ”. Alisema Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda.

Aliwapongeza Viongozi wa Jimbo la Mahonda pamoja na wale wa Wilaya nzima ya Kaskazini “B” kwa umakini wao wa kusimamia uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni katika njia ya amani na utulivu.

Alisema hatua hiyo imetoa sura nzuri kiasi kwamba Viongozi wa Kitaifa wamepata faraja na mwanzo mzuri wa kuanza kuwatumikia Wananchi wao kwa kuwaletea maendeleo kama walivyoahidi wakati wakitangaza Sera na Ilani zao.

Katika Mkutano huo Viongozi hao ambao ni Madiwani Masheha, Wazee mashuhuri pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” walipata fursa ya kuwachagua wajumbe Tisa watakaounda Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Mahonda.

Kwa mujibu wa sheria  na Taratibu zilivyoagiza za Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa ni pamoja na Masheha Wawili, Madiwani Wawili, Wazee Wawili wanaoheshimika katika Jimbo, Mtu Mmoja wa Mahitaji Maalum pamoja na Mmoja anayewakilisha asasi za Kiraia zilizomo ndani ya Jimbo Husika.

Hata hivyo Katibu atakayekuwa mtendaji muandamizi wa Kamati hiyo anatarajiwa kuchaguliwa katika mkutano wa kwanza utakaoitishwa wa Kamati hiyo kwa kushirikisha uongozi wa Halmashauri ya Wilaya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.