Habari za Punde

Wilaya ya Wete yaongoza kwenye matendo ya ukatili wa kijinsia

Na Haji Nassor, Pemba   
          
AMA kweli….. hawakukosea wahenga walivyonena ‘umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’’.

Ukitaka maana yake, fikiria, kaa chini, tikisa akili na chemsha bongo lazima utapata jawabu.

Sio tatizo… kama hayo yote huyawezi, nifuate, njoo, nisome aya kwa aya, na kisha mstari mmoja baada ya mwengine, utajua tu.

Naanza kukufahamisha kwa dhati, hebu jaribu kumuua chawa kwa kutumia kidole chako chochote kile kimoja, jaribu basi…..anza..twendee…haya muuwe…aaa umeshindwa.

Sasa changanya vidole vyako viwili na sasa muuwe chawa…haya twende mbona imewezekana, maana hapo vidole vyako vilishirikiana na pale awali ulivitenganisha.

Kauli hii imefanikiwa sana Zanzibar na hasa kisiwani Pemba, baada ya viongozi wa shehia, waratibu wao wa wanawake na watoto, Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA ofisi ya Zanzibar kushirikiana.

TAMWA imekuwa haipati usingizi, kutokana na jamii ya Zanzibar na hasa wanawake na watoto, kukumbwa na majanga ya ukatili wa kijinsia, ingawa linapigwa vita lakini…..


Ndio maana, TAMWA ikamua kuchanganya nguvu na wenzao wa serikali ya Denmark, na kufanikiwa kupata mradi uliodumu kwa miaka miaka miwili, yaania kuanzia 2012 hadi mwezi Septemba mwaka 2014.
Kwa kisiwa cha Pemba, mradi huu ulijitupa shehia sita za wilaya ya Wete, ambapo pia iligundulika ndio shehia ambazo matendo ya ukatili wa kijnsia kwa wanawake na watoto yamekithiri.

Hapo TAMWA ikaanza kwa mafunzo, semina za hapa na pale, mbinu za kuibua matendo hayo, na vikao vya kila mara, vilivyowashirikisha masheha waratibu wao, maofisa kutoka ustawi na hata wizara husika.

“Lengo la TAMWA la kuleta mradi huu kwenye shehia hizi, sio kwa upendeleo wala kwamba chama hicho kinauhusiano na yoyote miongoni mwenu, ni kuwepo juu matendo’’, alisema Mratib wa TAMWA Mzuri Issa akizungumza kwenye vikao.

Yeye anaamini, utakapomalizika mradi huo wa ‘Kukuza Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake GEWE, matendo ya ukatili yawe yameshapungua.

Kabla ya mradi huo, kuanza kwenye shehia za Kinyikani, Kiungoni, Shengejuu, Mchangamdogo, Mjini ole na Kangani kulikuwa kukiripotiwa matendo 80 kwa mwaka.

Wastani wa kila shehia kwa matendo hayo ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, likiwemo la ubakaji kabla ya kuanza kwa mradi wa GEWE, ni 13 kwa mwaka.

Kwa mfano, Sheha wa shehia ya Mchanga mdogo Asaa Makame Said anasema, alikuwa akipokea malalamiko ya ukatili wa kijinsia sita, jambo ambalo lilikuwa linatisha.

“Matendo hayo ya ukatili wa kijinsia ni yale yaliokuwa yakiripotiwa na familia tu kwangu, maana hata mbinu za kuibua ilikua hatuna’’, alisema sheha huyo.

Hali kama hii kabla ya kuingia kwa mradi wa GEWE, ilikuwepo shehia ya Mjini Ole, ambapo Mratibu wa wanawake na watoto, Khadija Henop Maziku alikuwa akipokea matendo 17.

“Kwa kweli kabla ya TAMWA kutuletea mradi wa GEWE, matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto yalikua juu sana, maana hata sisi waratibu na masheha wetu hatukuwa wajanja wa kuyaibua”, anafafanua.

Zipo pia shehia kama za Kinyikani ambapo uchunguuzi umebaina kuwa, kabla ya kuingia na mradi huo, kulikuwa kukiripotiwa matendo 10 ambayo yalikuwa yakiwadhalilisha wanawake na watoto kwa mwka.

Mratibu wa mradi huo kutoka TAMWA, Asha Abdi Makame, yeye katika kipindi cha mwaka 2013 wakati mradi huo ukiwa umeshapata mwaka mmoja, aliwataka masheha kuhakikisha wanapunguza mtendoa hayo kwa kutoa elimu.

Kwa wakati huo, Mratibu huyo, alisema lazima elimu wanayopewa kupitia vikao vyao, wawaelimishe na wananchi wao, maana haitakuwa na maana mradi ukimalizika kama hakuna mafanikio.

Hata Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed  nae alisema anatarajia hasa katika shehia hizo sita, matendo ya udhalilisha baada ya mradi kumaliza yapungue.

Baada ya kazi nzito iliofanywa na TAMWA, kwa kushirikiana na waratibuwa shehia hizo sita, masheha, afisi ya ustawi na hata wizara inayosimamia haki za wanawake na watoto, mradi umeongezwa na wafadhili.

Baada ya wafadhili kuona kwamba mradi huu umesaidia sana katika kuyaibua na kuyatokomeza matendo ya udhalilishaji wa kijinsia kwa kiasi kikubwa, ndipo wakaamua kuuongezea muda, ambopo ulikuwa umemalizika mwaka 2014 na sasa unakwenda hadi Disemba mwaka huu.

Hii itaweza kuongeza nguvu zaidi kwa waratibu wa wanawake na watoto wa shehia, katika kuyaibua matendo hayo, ambapo walifurahi sana na kusema jitihada zitaendelea zaidi katika kuyatokomeza matendo hayo.

Waratibu hao walisema wamefarajika sana kwa mradi huo kuongezewa muda, ambapo utawafanya kujenga nguvu za pamoja katika kuyaondosha matendo ya ukatili wa kijinsia.

Kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika Kiuyu Minungwini, mbele ya watendaji wa TAMWA, masheha hao na waratibu walitakiwa sasa wafanya tathimini juu ya mafanikio na changamoto.

Mwenyekiti wa kikao hicho, sheha wa shehia ya Mjini ole, Khamis Shaaban, aliinyanyua shehia moja baada ya nyengine ili kueleza mbele ya kikao hicho kama kuna mafanikio ya mradi huo wa GEWE awali uliodumu miaka miwili, ambapo sasa umeongezewa muda wa mwaka mmoja.

Mauwa Said Khamis alikuwa wa mwanzo kutoa ripoti yake, ambapo alisema, kwanza mradi umezaa matunda maana hata matendo ya ukatili awali yalikuwa 10, ambapo kwa sasa anapokea matano (5) kwa mwaka.

“Mradi wa GEWE kwenye shehia yangu, nasema umezaa matunda, maana kwa hesabu za asilimia, sasa nnayo 0.41 kutoka asilimia 0.83 ya zamani kwa mwaka, kwa matendo ya ukatili wa kijinsia’’, alisema.

Zamu ya sheha wa shehia ya shengejuu Omra Faki Kombo, ikafika na kutakiwa na kusema lolote na Mwenyekiti, akajilabu, kwa sasa anapokea matendo matatu (3) kutoka saba (7) ya awali.

“Kabla ya kuja mradi huu wa GEWE, hali ilikuwa ikitisha, maana yalikuwa yakiripotiwa tu ni saba, lakini sasa nakaa hata miezi mitano bila ya kujitokeza’’, alifafanua.

Mafanikio makubwa hasa ya kujivunia kwa TAMWA ni kwenye shehia ya Kangagani, ambayo kabla ya kufikiwa na mradi huu, Mratibu wake Awena Salim Kombo alisema yalikua 30.

“Sasa leo tukiwa mradi umeshakamilika kwa mwaka mzima napokea na kuibua matendo 10, sawa na asilimia 0.83, kutoka wastani wa matendo 2 kwa siku’’, alifafanua.

Kwenye shehia pia ya Mchanga mdogo sheha wa shehia hiyo Asaa Makame Said, naye anasema inagwa kwake huwa ni ya kujirudia rudia, lakini mafanikio yapo.

“Kama naangalia mafanikio ya mtendo ya ukatili wa kijinsia, basi kwenye shehia yangu nasema niko pazuri, maana sasa kwa mwaka napata matatu (3), kutoka sita (6) kabla ya GEWE’’, alifafanua.

Afisa ustawi wa Jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed, anasema kama mradi huo wa ‘GEWE’ ungeaanza miaka kumi iliopita, basi hata shehia ya Kiungoni isingelikuwa juu.

“Maana Mratibu wa shehia hiyo Mchanga Said Hamad, anasema sasa anapokea matendo sita (6), ambapo kabla ya mradi yalikuwa 10 kwa mwaka’’, alifafanua

Waratibu hao wanasema, sasa dunia inakoelekea utatuzi wa matendo hayo ni magumu, maana wakosaji kama matendo ya ubkaji huwa ni ndugu na jamaa wa akaribu.

Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Omar Khamis Othuman  yeye anasema jambo lililofanywa na TAMWA kupitia mradi wa GEWE sasa ni kuendelezwa.

“Mimi naamini umoja na nguvu na utengano ni udhaifu, sasa kama kuna mashirika mengine yanayoguswa kama ilivyokuwa TAMWA, basi matendo hayo yatapungua’’, alisema.

Kwa ujumla mradi huo wa awali wa GEWE uliokuwa ukiendeshwa na TAMWA tokea mwaka 2012 na kumalizika mwezi septemba 2014,  kwenye shehia hizo sita za wilaya wete, umezaa matunda maana matendo ya ukatilia yamepungua kutoka 80 hadi 34.

Baadhi ya wananchi wa shehia hizo walisema, elimu imewafikia lakini kwa sasa, baadhi ya mtendo hayo huwa magumu kupungua maana watendaji ni watu wa karibu.

Idda Haji Makame wa shehia ya Mchanga mdogo, yeye anasema kama baba, kaka, au mjomba anambaka mtoto wake, kesi za aina hiyo huwa vigumu kumalizika.

Asha Abdalla Haji wa shehia ya Kangagani yeye, anasema lazima jamii ibadilike, na kuhakikisha wanatoa ushahidi mahakamani ili wakosaji watiwe adabu kwa mujibu wa sheria.

“Sisi wenyewe jamii pia wakati mwengine ni kikwazo kumaliza kesi za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, maana huwa wazito kutoa ushahidi mahakamani’’, alifafanua.

Ingawa masheha na waratibu hao walisema kwa sasa changamoto kubwa ni vyombo vinavyosimamia haki, kutofanyaka kazi zao kwa umakini.

Walipendekeza kuwa sasa vyombo vya sheria na hasa Polisi na Mahakama, kushibishwe taaluma ya kutenda haki ili wakosaji wahukumiwe.

 Mratibu wa Mradi wa GEWE kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania ‘TGNP’ Matha Samwel, yeye anasema suala la kumaliza metendo hayo lazima ushirikiano uwepo.

Aliekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi Valerie Msoka, anasema mradi wa GEWE, umekuwa na mafanikio makubwa kwa jamii katika kujitambua na kuibua vitendo vya Ukatili wa kijinsia.

Lakini anafurahi zaidi kwamba hata vyombo vya habari, vyenyewe vimekuwa weledi wa kutafutana kuibua vitendo hivyo zaidi na hasa baada ya uwepo wa mradi.

Wilaya zilizofanyiwa utafiti huo ni wilaya za Wete Pemba,  Magharibi Unguja, Kusini kwa Unguja, Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Lindi Vijijini (Lindi), Mvomero (Morogoro) na wilaya mbili za Kinondoni na Ilala (Dar es Salaam).

TAMWA inaendelea kuwashauri wakuu wa kata na shehia, kuendelea kupiga vita matendo hayo, hata kama mradi huo umefikia ukiongoni, maana suala la kutimiza wajibu wao halihitaji ufadhili.
                                                 mwisho




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.