Habari za Punde

CCM Zanzibar yataka wahanga wa mafuriko wasaidiwe

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka viongozi wa serikali na chama kuharakisha kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko bila ya kujali tofauti zao za kisiasa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akitembelea maeneo mbali mbali ya Zanzibar yaliyoathiriwa na mafuriko hayo.

Alisema mamia ya watu waliopata mafuriko hayo kwa sasa wanahitaji msaada wa haraka ili waweze kupata mahitaji ya msingi kama walivyo watu wengine.

“CCM itaendelea kuungana na wananchi waliopata athari ya mafuriko kwa kutoa misaada ya hali na mali kwa lengo la kuhakikisha wanapita salama katika kipindi hiki kigumu cha mvua za masika zinaendelea nchini”., alisema Vuai.

Akifafanua zaidi Vuai alisema CCM inakuwa na misimamo ya kisiasa wakati wa upigaji wa kura pekee lakini sio kwenye masuala ya majanga na matatizo ya kitaifa kwani inaamini kuwa majanga hayo yanawakumba wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za kisiasa.

“Misimamo ya chama chetu inajitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi wa kisiasa lakini wakati wa majanga na matatizo ya kitaifa kamna haya tunabaki kuwa wamoja katika kuwasaidia na kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali tofauti zetu za kisiasa.

Kwa niaba ya chama chetu natoa pole na kuwasihi wananchi wote waliokumbwa na mafuriko kuendelea kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki na tunawaahidi kuwa chama na serikali tutaendelea kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo kadri ya uwezo utakavyoruhusu.”, alifafanua Vuai.


Aliwashauri baadhi ya wananchi waliojenga katika maeneo ya mabonde na sehemu za mitaro ya maji ya mvua kuhama kwa haraka katika maeneo hayo kabla hawajapata athari za kuharibikiwa na  makaazi yao.

 Pamoja na hayo, Vuai alifafanua kuwa CCM itaendelea kuzishauri taasisi za serikali zinazohusika na masuala ya makaazi na miundo mbinu ya barabara kutafuta njia mbadala za  kiutaalamu zitakazosaidia kumaliza tatizo la maji ya mvua  kujaa katika baadhi ya mitaa ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana katika ziara hiyo zinaeleza kuwa takriban nyumba 720 zimekubwa na mafuriko kati ya hizo 196 wamehama kabisa makaazi yao baada ya nyumba zao kuharibiwa kabiwa kabisa na mafuriko hayo.

Katika ziara hiyo yenye madhumuni ya kuwapa pole na kutathimini athari ya mafuriko hayo, Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai, aliungana na viongozi mbali mbali wa chama na Serikali wakiwemo Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na Masheha wa maeneo husika.

 Naibu Katibu Mkuu Vuai, alitembelea maeneo 11 yaliyopata majanga hayo yakiwemo Timba, Karakana, Chumbuni, Kihinani, Bububu, Kikwajuni, Kisimajongoo, Kwahani, Matarumbeta, Sebreni, Jang’mbe ya Migombani na Mfenesini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.