Habari za Punde

SMZ kwa Kushirikiana na AFDB Kuimarisha Miundombinu ya Barabara Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifungua Warsha ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri { TSSP } iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibae Beacha Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Kaimu Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Bibi Merry Helen Minja akifafanua hatua zitakazochukuliwa katika hatua za utekelezaji wa Mradi wa mpango wa uimarishaji wa sekta ya usafiri.
Balozi Seif aliyepo kati akti akiwa pamoja na Viongozi wa Warsha ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri iliyofanyika Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Miundombnu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akio, Kaimu Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Bibi Merry Helen Minja na kulia ya balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unaguja Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Khamis Mussa.
Baadhi ya washiriki wa warsha ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri iliyofanyika huko Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Balozi Seif aliyepo kati kati ya waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja washiriki wa warsha ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Viongozi wa warsha ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri mara baada ya kuizindua rasmi hapo Zanzibar Beach Resort.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika { AFDB } inatarajia kujenga  Barabara  Nne zenye urefu wa Kilomita 51.78 katika azma yake ya kuimarisha sekta ya mawasiliano ya usafiri wa ardhini hapa Nchini.

Ujenzi wa Bara bara hizo Nne  za Zanzibar unajumuisha sambamba  na zile za Tanzania Bara  zitakazopata msukumo wa ufadhili kupitia Mfuko huo wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika zote zikiwa na urefu wa Kilomita Mia 462.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo kwenye Warsha  ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri { TSSP } iliyofanyika  Zanzibar Beach  Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kushirikisha wataalamu wa sekta ya usafiri, watendaji wa Serikali pamoja na wawakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Balozi Seif alisema mradi wa Bara hizo ni pamoja na zile za Bububu – Mahonda – hadi Mkokotoni wenye  wenye urefu wa Kilomita 31, Pale – Kiongele Kilomita 4.6, Fuoni – Kombeni  Kilomita 8.6 na Matemwe – Muyuni Kilomita 7.6.

Alisema ushirikiano wa karibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na washirika wa maendeleo umeiwezesha miundombinu ya bara bara  zenye urefu wa Kilomita 90 kuimarika  ndani ya kipindi cha miaka Mitano iliyopita zikiwa katika kiwango kinachokubalika Kimataifa .

Alifahamisha kwamba Serikali kupitia mfuko wa Bara bara Zanzibar {ZRF } iliongeza bajeti  yake kwa ajili ya matengenezo ya Bara bara kutoka shilingi Bilioni 5 mwaka 2011 hadi shilingi Bilioni 7.3 mwaka uliopita wa 2015.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kuanza kwa miradi hiyo ya ujenzi wa Bara bara za Zanzibar kwa upande mwengine kutatoa fursa za ajira  1,500 kwa baadhi ya wananchi hasa Vijana.

Alisema fursa hizo pia zitaibua ajira  za muda zipatazo 3,000 katika kazi za matengenezo ya bara bara zinazoharibika kutokana na matumizi mbali mbali ikiwemo kuharibika kwa mvua.

Balozi Seif aliupongeza Uongozi na Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya usimamizi wa Mwakilishi wake hapa Nchini Dr. Tonia Kandiero kwa juhudi wanazochukuwa katika kusaidia Maendeleo ya Nchi changa hasa zile zilizomo katika ukanda wa jangwa la sahara.

Alisema mbali ya kuunga mkono nguvu za uimarishaji wa sekta ya Bara bara lakini pia Benki hiyo imeonyesha nia yake thabiti ya kusaidia uendelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo na ustawi wa jamii nchini.

Balozi Seif alisema ipo miradi ya Afya, Elimu, Kilimo, Huduma za Maji safi na salama pamoja na mafunzo ya kuijengea Jamii namna ya kuishi katika misingi ya utawala  Bora ambayo imepata msukumo wa Benki hiyo kupitia Mpango wa kuunga mkono Sekta ya Usafiri { TSSP }.

“ Benki ya Maendeleo ya Afrika imeanza kutoa huduma zake  Zanzibar tokea mwaka 1998 kwa kusaidia ujenzi wa Bara  bara Tano zenye urefu wa Kilomita 88.3 ambazo ni Kinyasini – tunguu, Paje – Makunduchi, Mazizini – Fumba na Amani – Dunga ”. Alifafanua Balozi Seif.

Mapema kaimu mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Bibi Merry Helen Minja alisema Taasisi hiyo ya kifedha kwa maendeleo ya Mataifa ya Bara la Afrika imejikita zaidi katika kuona mipango ya Mataifa hayo kama ile ya kupunguza Umaskini { MKUZA na MKUKUTA } inafanikiwa vyema.

Bibi Minja alisema Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri { TSSP } umeanza kubuniwa rasmi Tarehe 26 Novemba mwaka 2015 na kufikia hatua ya kuwekwa saini mkataba wake mnamo tarehe 4 Disemba mwaka 2015.

Kaimu Mwakilishi huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Bibi Merry Helen Minja alifahamisha kwamba mradi mzima wa ujenzi wa bara hizo unatarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 270.95 sawa na shilingi Trilioni 1.3za Kitanzania.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua Mradi  huo wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri { TSSP } Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akio alisema kwamba maendeleo ya Taifa lolote duniani hutegemea kuimarika kwa Sekta ya mawasiliano ya usafiri.

Dr. Malik alisema Wizara anayoisimamia imepewa jukumu la kusimamia jukumu hilo kazi ambayo imekuwa ikipata  mafanikio kutokana na nguvu ya pamoja kati ya Serikali  na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi.

Warsha  hiyo ya siku moja  ya uzinduzi wa  Mradi  wa Mpango wa uimarishaji  wa  Sekta ya Usafiri imejadili mada Nne muhimu miongoni mwake ni pamoja na sheria na taratibu za manunuzi, ujenzi wa bara bara zilizomo ndani  ya mradi huo pamoja na ripoti ya fedha  na ukaguzi wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.