Habari za Punde

Wafanyakazi wa kampuni ya simu ya Zantel wapanda miti kwenye hifadhi ya Masingini kama moja ya jitihada za kutunza mazingira.

 Na Mwandishi Wetu Zanzibar.
Wafanyakazi wa kampuni ya simu ya Zantel leo wameshiriki katika zoezi la kupanda miti kwenye hifadhi ya Masingini iliyopo magharibi mwa kisiwa cha  Unguja kama  moja ya jitihada zake katika kutekeleza mpango wa kutunza na kuhifadhi mazingira visiwani Zanzibar.

Eneo la hifadhi ya msingini lipo mita 120 kutoka usawa wa bahari na ni eneo lenye vyanzo vingi vya maji  ambavyo vinakadiriwa kutoa lita 27,400,000 kwa ajili ya matumizi ya kila siku ya wakazi wa Zanzibar.

Akizungumza wakati wa upandaji miti, Afsa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu ya Zantel,bwana Benoit Janin alisema kupanda miti kutasaidia kuzuia mmomonyoko wa ardhi, kuongeza  rutuba ya udongo na pia kulinda vyanzo vya maji .

‘Kama Kampuni ya simu inayotoa huduma ya mawasiliano kwa wakazi wa visiwani ni lazima tuhakikishe tunatunza na kuhifadhi mazingira kama moja ya  rasilimali muhimu kwa  ajili ya ustawi wa jamii yetu’alisema Bw Janin.

Zoezi hili la kupanda miti limefanyika leo, ikiwa ni wiki moja tu toka uzinduzi wa mtandao wa 4G visiwani hapa, hatua inayoonyesha kuwa kampuni ya Zantel imejipanga katika mpango wa kuhakikisha inalinda na kuhifadhi mazingira kwa kushirikiana na serekali yetu .

Akizungumza baada ya tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar, bwana Sheha Mjaja Juma aliwapongeza wafanyakazi wa kampuni ya simu ya  Zantel kwa kuweza kushiriki kwenye  zoezi hilo  la kutunza na kuhifadhi mazingira.

‘Madhumuni ya zoezi hili la upandaji miti hapa Masingini yamelenga kusaidia jitihada za kutunza na kulinda vyanzo vya maji, msitu pia kuzuia mmonyoko wa ardhi ili kulinda viumbe hai vilivyopo kwenye eneo hilo’ alisema bwana Sheha.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.