Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe,Mathias M.Chikawe alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kuonana na Rais,leo,[Picha na ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe,Mathias M.Chikawe alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao,[Picha na ikulu.]
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 6.5.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesisitiza haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya
Tanzania na Japan hasa kwa kutambua hatua za nchi hiyo za kuendelea kuiiunga
mkono Tanzania katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu
mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe. Mathias Meinrad Chikawe.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alimueleza
Balozi huyo kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri
pamoja na hatua za Japan za kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha
miradi kadhaa hapa nchini.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Japan
imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara
kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha miradi mbali
mbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya maji, umeme, kilimo, afya na miradi
mengineyo.
Alisema kuwa Serikali ya Japan pamoja na
Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa muda mrefu zimekuwa zikiunga mkono
uimarishaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini ambapo kwa upande wa Zanzibar
nchi hiyo imeweza kusaidia mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao
hivi sasa upo katika awamu ya tatu.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali
Japan imeweza kusaidia miradi kadhaa ukiwemo ule wa kusambaza umeme vijijini
hasa katika Mkoa wa Kusini Unguja huku akieleza mpango wa nchi hiyo wa kusaida
ujenzi wa soko la kisasa la samaki huko Malindi mjini Unguja sambamba na usambazaji
wa huduma za umeme ukiwemo ule wa vijijini na miradi mengineyo ya maendeleo.
Dk. Shein, pia, alimueleza Balozi huyo
umuhimu wa kuimarisha sekta ya uwekezaji hasa katika viwanda kwa kutumia uvuvi
wa bahari kuu kwa kuzingatia kuwa ukanda wa bahari unaoizunguka Zanzibar una
samaki wengi wa aina ya jodari ambao ni wazuri na wanapendwa sana duniani.
Aidha, Dk. Shein alieleza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa kilimo
cha mpunga wa umwagiliaji maji ambapo lengo la Serikali kati ya mwaka 2018-2019
ni kuzalisha nusu ya mahitaji ya mchele unaotumika hapa nchini ambao hivi sasa unaagizwa
nje ya nchi.
Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kumueleza
Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuitangaza zaidi Tanzania kiutalii hasa kwa kuweko
vivutio kadhaa kama fukwe nzuri za bahari kwa Zanzibar na mbuga za wanyama kwa
Tanzania Bara.
Nae Balozi mpya wa Tanzania nchini Japan
Mhe. Mathias Meinrad Chikawe alitoa pongezi kwa Dk. Shein pamoja na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kwa kupata uteuzi wake
huo.
Balozi Chikawe alimuhakikikishia Dk.
Shein kuwa katika wadhifa wake huo mpya juhudi za makusudi atazichukua katika
kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Japan na Tanzania
unaimarishwa zaidi sambamba na kuyafanyia kazi maelekezo yote aliopewa na Rais
Dk. Shein.
Kabla ya kupangiwa kituo hicho cha kazi
Balozi Chikawe aliteuliwa kuwa Balozi mnazo tarehe 14 Februari mwaka huu.
Balozi Chikawe aliwahi kuwa Mbunge wa
Jimbo la Nachingwea kati ya mwaka 2005 na 2015, na kwa vipindi tofauti katika
Serikali ya Awamu ya nne alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Utawala Bora ambapo pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Mh. Balozi! Ipo haja ya kutekelezwa kwa vitendo yale yote mazuri mliyokubaliana kuyafanyia kazi na Mh. Rais
ReplyDeleteNdugu yangu Suleiman, hiyo ni kufurahisha nafsi tu, Zanzibar hakuna msaada wa kihivyo, ingawa misaada kwa nchi si jambo jema, misaada wanayopata bara ingekuwa zanzibar tungekuwa mbali, leo pahali kama mwana kwerekwe badala ya kujenga kitu kama skyover, tunafanya upuuzi tuu miaka nenda miaka rudi, Zanzibar kweli khasa hakuna serikali makini miaka yote, mola atusaidie tuu
ReplyDelete