Habari za Punde

Dk Shein akutana na Balozi Mteule nchini Japan

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza  na Balozi  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe,Mathias M.Chikawe  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kuonana na Rais,leo,[Picha na ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na Balozi  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe,Mathias M.Chikawe  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao,[Picha na ikulu.]


 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                           6.5.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan hasa kwa kutambua hatua za nchi hiyo za kuendelea kuiiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe. Mathias Meinrad Chikawe.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri pamoja na hatua za Japan za kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miradi kadhaa hapa nchini.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Japan imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya maji, umeme, kilimo, afya na miradi mengineyo.

Alisema kuwa Serikali ya Japan pamoja na Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa muda mrefu zimekuwa zikiunga mkono uimarishaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini ambapo kwa upande wa Zanzibar nchi hiyo imeweza kusaidia mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao hivi sasa upo katika awamu ya tatu.


Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali Japan imeweza kusaidia miradi kadhaa ukiwemo ule wa kusambaza umeme vijijini hasa katika Mkoa wa Kusini Unguja huku akieleza mpango wa nchi hiyo wa kusaida ujenzi wa soko la kisasa la samaki huko Malindi mjini Unguja sambamba na usambazaji wa huduma za umeme ukiwemo ule wa vijijini na miradi mengineyo ya maendeleo.

Dk. Shein, pia, alimueleza Balozi huyo umuhimu wa kuimarisha sekta ya uwekezaji hasa katika viwanda kwa kutumia uvuvi wa bahari kuu kwa kuzingatia kuwa ukanda wa bahari unaoizunguka Zanzibar una samaki wengi wa aina ya jodari ambao ni wazuri na wanapendwa sana duniani.

Aidha, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji ambapo lengo la Serikali kati ya mwaka 2018-2019 ni kuzalisha nusu ya mahitaji ya mchele unaotumika hapa nchini ambao hivi sasa unaagizwa nje ya nchi.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuitangaza zaidi Tanzania kiutalii hasa kwa kuweko vivutio kadhaa kama fukwe nzuri za bahari kwa Zanzibar na mbuga za wanyama kwa Tanzania Bara.

Nae Balozi mpya wa Tanzania nchini Japan Mhe. Mathias Meinrad Chikawe alitoa pongezi kwa Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kwa kupata uteuzi wake huo.

Balozi Chikawe alimuhakikikishia Dk. Shein kuwa katika wadhifa wake huo mpya juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Japan na Tanzania unaimarishwa zaidi sambamba na kuyafanyia kazi maelekezo yote aliopewa na Rais Dk. Shein.

Kabla ya kupangiwa kituo hicho cha kazi Balozi Chikawe aliteuliwa kuwa Balozi mnazo tarehe 14 Februari mwaka huu.

Balozi Chikawe aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nachingwea kati ya mwaka 2005 na 2015, na kwa vipindi tofauti katika Serikali ya Awamu ya nne alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora ambapo pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

2 comments:

  1. Mh. Balozi! Ipo haja ya kutekelezwa kwa vitendo yale yote mazuri mliyokubaliana kuyafanyia kazi na Mh. Rais

    ReplyDelete
  2. Ndugu yangu Suleiman, hiyo ni kufurahisha nafsi tu, Zanzibar hakuna msaada wa kihivyo, ingawa misaada kwa nchi si jambo jema, misaada wanayopata bara ingekuwa zanzibar tungekuwa mbali, leo pahali kama mwana kwerekwe badala ya kujenga kitu kama skyover, tunafanya upuuzi tuu miaka nenda miaka rudi, Zanzibar kweli khasa hakuna serikali makini miaka yote, mola atusaidie tuu

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.