HOTUBA YA RAIS WA
ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA UFUNGUZI WA MASHINDANO YA MICHEZO YA VYUO
VIKUU NA TAASISI ZA
ELIMU YA JUU ZANZIBAR
(ZAHILFE - GAMES)
UWANJA WA AMAAN ZANZIBAR
TAREHE 21 MEI, 2016
Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Amali, Zanzibar,
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utalii,
Utamaduni na
Michezo, Zanzibar,
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo, Zanzibar,
Waheshimiwa Mawaziri mbali mbali
mliohudhuria,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Shirikisho
la Vyuo
Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu, Zanzibar,
Viongozi mbali mbali wa Serikali
mliohudhuria,
Wakuu wa Vyuo na Skuli mbali mbali
mliohudhuria,
Wanamichezo na Wanafunzi wote,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Aleikum,
Kwanza kabisa, napenda nianze kwa kumshukuru
Mola wetu Mtukufu Subhana Wataala; Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uhai na afya
njema tukaweza kuungana na wanamichezo wenzetu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na
Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar. Pili,
nachukua fursa hii kutoa shukurani za dhati kwa viongozi wa Shirikisho la Vyuo
Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar (ZAHILFE) kupitia Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali kwa kunialika kuja kuungana na wanamichezo wenzangu kwa lengo
la kuyafungua mashindano haya ya Shirikisho la Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu
Zanzibar katika mwaka huu wa 2016. Kwa
hakika nimeupokea mwaliko huu kwa furaha na Ahsanteni Sana.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kukupongezeni kwa dhati
kabisa, kwani mmeamua kutekeleza kwa vitendo madhumuni ya sera ya michezo ya
Zanzibar. Sera ya michezo ya Zanzibar ya
mwaka 2007 imeweka bayana umuhimu wa michezo kwa wanamichezo wote kutoka kwenye
makundi tofauti katika jamii, zikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu na Skuli kwa
jumla. Nimeridhishwa sana na jitihada za
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kusimamia vyema wajibu wa kuandaa
mashindano ya michezo katika taasisi za elimu za ngazi zote. Lengo kubwa likiwa
ni kuchangia jitihada zetu kwa pamoja katika kuwapata wanamichezo bora wa Taifa na kugundua vipaji
vya wachezaji kama ilivyoelekezwa katika sera ya michezo ya Zanzibar. Hongereni Sana.
Mashindano haya ni kielelezo na nyenzo moja
wapo ya kujenga umoja, maelewano na mshikamano wa kitaifa na kimataifa kwa
wanavyuo, wanafunzi wa skuli na jamii kwa jumla. Aidha, kulingana na mabadiliko ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii duniani kote, michezo hivi sasa imepata kipaumbele kikubwa
mbali na ile dhana ya tangu kale ya kuwa michezo ni sehemu moja wapo ya
burudani. Kadhalika, michezo ni ajira
kwa vijana wetu. Naamini mnawajuwa kuwa
hivi sasa vijana kadhaa wa Kitanzania ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya
nchi. Vile vile, michezo kwa kiasi
kikubwa husaidia kuimarisha nidhamu maskulini, vyuoni na katika jamii kwa
jumla. Kwa upande wenu wanafunzi, nidhamu ina umuhimu mkubwa katika kupata
matokeo mazuri kwenye masomo yenu.
Matarajio yetu ni kuwa kupitia michezo, wanafunzi mtakuwa na nidhamu na
mahusiano mazuri kati yenu wenyewe kwa wenyewe pamoja na walimu wenu mnapokua
darasani.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Natambua kuwa nyinyi ni wanafunzi ambao
mnahitaji kuimarisha afya zenu, kukuza taaluma na vipaji vyenu. Hayo ni miongoni mwa matokeo ya kushiriki
michezo. Ili michezo iendelee kukua hapa
nchini ni lazima ukuaji wa vipaji vya michezo uanzie kuandaliwa katika ngazi za
maskuli, vyuoni na hatimae katika jamii yetu.
Kwa mnasaba huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imeamua
kulirudisha vuguvugu la michezo katika
skuli zetu na taasisi za juu za elimu. Katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya
Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tulianzisha Idara mpya ya Michezo na
Utamaduni ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Idara hii imeanzishwa kwa lengo la kutekeleza
Sera ya Taifa ya Michezo katika skuli ili tuibue, tukuze, tuimarishe na
tuendeleze vipaji vya wanafunzi ili kupata wanamichezo bora katika nchi
yetu.
Idara hii imeanza kazi vizuri ambapo mwaka
jana iliwandaa vyema wanafunzi wetu wa Sekondari kwa ajili ya kushiriki
Mashindano ya Shirikisho la Skuli za Sekondari ya Afrika ya Mashariki
(Federation of East African Secondary School Sports Association – FEASSSA )
yaliyofanyika Dar es Salaam. Timu zetu
za mpira wa miguu wanaume pamoja na mpira wa mikono na wavu wanaume zilifanya
vizuri kwa kushika nafasi ya tatu katika makundi yaliyozijumuisha timu za
Kenya, Uganda, Sudan ya Kusini na Rwanda. Kwa upande wa michezo wa riadha, timu
yetu ilishika nafasi ya nne kwa jumla.
Tutafanya kila jitihada ili matokeo ya mwaka jana, yatuongezee kasi na
ari ya kufanya maandalizi bora zaidi ili tupate nafasi bora katika mashindano
yajayo, jambo ambalo linawezekana.
Naelewa kuwa tayari maandalizi ya vijana wetu kwa ajili ya michezo ya
Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yamekwishaanza. Hata hivyo, nataka mfanye maandalizi ya
kupata kushinda na sio kushiriki.
Natoa wito kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali kupitia Idara ya Michezo kushirikiana vyema na Uongozi wa Wizara ya
Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo na vyama vyengine vya michezo katika
kuziandaa timu zetu mbali mbali zinazoiwakilisha nchi yetu ili kuiletea heshima
yetu katika nyanja za michezo, kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Zanzibar ina historia kubwa, ndefu ya kufanya
vizuri katika michezo ya Kimataifa na kwa hivyo ni lazima sote tushirikiane
katika kuirudisha hadhi yetu hiyo ya nchi yetu.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Nataka mkumbuke kuwa, Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, Awamu zote imekuwa ikijitahidi kuendeleza michezo kuanzia kwenye
maskuli. Lengo hili limedhihirika wazi
mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964,
Serikali ilipoanzisha Wizara ya Elimu na Mila. Wakati huo, shughuli zote za
michezo na utamaduni ziliratibiwa na Wizara hiyo na wanafunzi wengi wa enzi
hizo tulishiriki. Mimi na wenzangu wengi
tuliopo hapa ni miongoni mwa waliopata fursa ya kuonesha vipaji vyetu katika
michezo ya riadha na mpira wa miguu, tulipokuwa tukisoma katika skuli za Msingi
na Sekondari. Tuliinukia kwenye michezo
hio na wengine walioendelea kuvuma na kupata sifa kem kem.
Katika Awamu hii ya Saba ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, tumejidhatiti kuendeleza michezo maskulini na vyuo vya
Elimu ya Juu kwa vile msingi hasa wa kupata vipaji hivyo huanzia
maskulini. Wengi mtakumbuka jitihada
zetu, tulipoanzisha mashindano ya mbio za riadha ya Wilaya zote 10 za
Zanzibar. Kwa mara ya kwanza,
niliridhishwa na vipaji vya vijana wetu,
nilivyoviona, kwa wanaume na kwa wanawake. Kutokana na jitihada nilizoziona ndipo
nilipofanya uamuzi wa kuwapa wanamichezo vifaa vya michezo vya aina mbali mbali
Unguja na Pemba, ili viweze kuwasaidia.
Zaidi ya hayo, Serikali imeanza kuchukua hatua za kufundishwa kwa somo
la michezo maskulini ambapo Idara ya Michezo na Utamaduni ilishirikiana na
Taasisi ya Elimu Zanzibar kwa kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha somo la
michezo katika skuli za msingi. Jumla ya
walimu 574 walifaidika na mafunzo hayo.
Vile vile, wanafunzi wameshajiishwa kupenda michezo na kuunda klabu za
michezo maskulini. Hivi sasa tayari
hamasa na vuguvugu la michezo maskulini limeanza kuonekana. Nataka nielezee jinsi nilivyofarijika pale
nilipoona michezo mbali mbali inayochezwa na vijana wetu kwenye kilele cha
Miaka 50 ya Maadhimisho ya Elimu bila ya malipo waliponialika kuwa Mgeni
Rasmi. Aidha, leo hii tunashuhudia
hamasa za michezo ya vijana wetu wa Taasisi za Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu
ya Juu. Sote tujipongeze kwa mafanikio
haya.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza la
Tisa la Wawakilishi, niliyoitoa tarehe 5 Aprili, 2016, nilieleza wazi dhamira
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha
pili tulichokianza. Niliwahakikishia wananchi kuzidisha juhudi katika kuyaendeleza
mafanikio tuliyoyapata katika sekta ya michezo kwa kuyaimarisha mashindano ya
riadha ya Wilaya na kuliimarisha Bonanza la Michezo na vikundi vya mazoezi
tunalolifanya tarehe mosi ya kila mwaka.
Aidha, tutaongeza juhudi katika kuimarisha michezo maskulini na vyuo vya
elimu ya juu ambapo katika kipindi hiki Serikali inadhamiria kulifundisha somo
la michezo katika skuli 6 za sekondari zilizochaguliwa, Unguja 4 na Pemba
2. Kadhalika, ujenzi wa uwanja wa Mao
Tse Tung, utaanza Disemba mwaka huu na utiaji wa tartan katika uwanja wa
Gombani nao unashughulikiwa. Vile vile,
Serikali ina mpango wa kujenga viwanja vya michezo katika kila Wilaya. Hatua nyengine ni kuhamasisha michezo ya
asili ya Zanzibar ikiwemo mashindano ya resi za Ngalawa, Bao, Karata, Mchezo wa
Ng’ombe na kadhalika. Watu wenye ulemavu
nao tutawahamasisha kwa kuwapatia vifaa pamoja na vyama vya michezo
vinavyohusika ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuendeleza michezo.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Katika mashindano tunayoyazindua leo, wasia
wangu kwenu ni kuwa mfuate taratibu na sheria za michezo. Mara nyingi michezo
huwatayarisha na kuwaandaa vijana wenye maadili mazuri, wasikivu, watiifu na
wenye nidhamu kwa jamii nzima, ikizingatiwa kuwa nyinyi ni viongozi wa kesho. Hivyo mnahitajika sana kujijenga na kujipamba
kwa kuwa na maadili na kuwa na nidhamu
nzuri, ili muweze kufanikiwa na kuishi maisha mazuri hapo baadae. Nidhamu
inamuwezesha mtu kufanya kazi zake kwa mpangilio mzuri unaokwenda sambamba na
malengo yanayokusudiwa. Hii itakuwa ndio njia ya uhakika ya kuyafikia malengo
yoyote yale ya kupata elimu bora pamoja na mafanikio mema katika maisha yenu ya
baadae. Nasisitiza umuhimu wa nidhamu
wakati wote wa mashindano haya na katika maisha yenu ya kutafuta elimu na
khatima njema ya maisha yenu hapo baadae.
Kadhalika, natoa wito kwa jamii yetu
izingatie, iendeleze na isimamie dhana halisi ya michezo. Ifahamike wazi kwamba
michezo sio inayowafanya watoto wawe
wacheza na watukutu. Ucheza, utundu na
utukutu kwa mtoto ni matokeo ya mambo mengine.
Lakini, michezo ina mchango mkubwa katika kuongeza ufahamu wa masomo na
kuchangamsha akili ya mwanafunzi katika kukabiliana na masomo yake. Miongoni mwa wanafunzi wanaofanya vizuri
darasani na kufanikiwa katika masomo yao na baadae kwenye maisha wamo pia
walioshiriki michezo. Hili
limethibitishwa na wataalamu. Kwa hivyo,
tusiwazuwie vijana wetu kushiriki katika michezo badala yake tuwashajiishe
waipende na washiriki.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Kabla sijamalizia hotuba yangu, natumia
fursa hii kukukumbusheni kuwa wakati mnapofurahia michezo yenu hii, iwe michezo
salama tangu mwanzo leo hii hadi siku ya
mwisho. Natoa kauli hiyo, nikiimaanisha
furaha yenu hii itaendelea kudumu iwapo tutaendelea kuwa salama na tuwe na tahadhari
kubwa juu ya maradhi ambayo yameikumba nchi yetu yakiwemo maradhi ya
kipindupindu, UKIMWI na matatizo yanayosababishwa na dawa za kulevya. Ni imani yangu kwa sasa kila mmoja wetu
anaelewa vyema jinsi madhara ya maradhi haya
yalivyotusibu katika jamii yetu.
Ni wajibu wetu kila tukipata fursa tuendelee kukumbushana ili tuchukue
hatua za lazima za kukabiliana na maradhi hayo kwa kuwa huchangia katika
kuzirudisha nyuma jitihada zetu za kuleta ustawi bora wa jamii yetu. Maradhi haya yanachangia katika kupunguza
nguvu kazi yetu kwa kasi kubwa. Miongoni mwa tahadhari mnazostahiki kuchukua ni
kuwa waaminifu michezoni, kujiepusha na marafiki ambao si waadilifu, kuweka
mazingira safi na kufuata maelekezo ya wataalamu wetu wa afya katika
kukabiliana na maradhi hayo thakili.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Kwa mara nyengine tena napenda niipongeze
kwa dhati kabisa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya
Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kwa jitihada zao katika kuwaunganisha na
kuwaweka pamoja wanafunzi wote wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu
ya Juu hapa Zanzibar, pamoja na Bodi ya Wadhamini ya Shirikisho na kuandaa
mashindano haya yaliyofana sana. Katika
kuyafanikisha mashindano ya mwaka huu, nimesikia kuna waliochangia kwa njia
mbali mbali. Napenda niungane na
waandaaji wa mashindano haya kwa kuwashukuru na kuwapongeza sana kwa moyo wao
wa kizalendo. Naipongeza Benki ya
Afrika, Baraza la Manispaa Zanzibar, Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi,
Unguja, Mfuko wa Hifadhi ya Taifa (NSSF), Kituo cha Azam Media, ZSSF, Shirika
la Bandari na wahisani wote waliosaidia kuyafanikisha mashindano haya yenye
kauli mbiu inayohamasisha michezo, elimu bora pamoja na mazingira safi na
salama ambayo ndio njia kuu ya kupambana na maradhi ya kuambukiza kikiwemo
kipindupindu.
Ndugu
Wanamichezo na Ndugu Wananchi,
Kabla sijamalizia kutoa nasaha zangu,
napenda nisisitize kuwa michezo kama hii itumike katika kuwatafuta na kuwaandaa
wanamichezo bora watakaoweza kuendelezwa na hatimae kuwapata wachezaji mahiri
wa michezo mbali mbali watakaoiletea sifa nchi yetu katika medani za
kimataifa. Kwa hivyo, walimu wa michezo
na waamuzi, wahakikishe kuwa mashindano
haya yanaendeshwa kwa kuzingatia sheria za michezo za kimataifa. Vile vile, mashindano haya yawe ni maandalizi
kwa timu zetu zinazotuwakilisha kwenye mashindano mengine. Namaliza hotuba yangu kwa kukutakieni kila
la kheri na mafanikio katika kipindi hiki cha mashindano. Michezo ni furaha, michezo ni umoja, michezo
ni amani na michezo ni afya.
Yazingatieni mambo hayo katika mashindano yenu.
Baada
ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Mashindano ya Michezo ya Shirikisho la Vyuo
Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar ya mwaka 2016, yamefunguliwa rasmi.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment