Habari za Punde

UVCCM Zanzibar kuanzisha vikundi vya Ujasiri amali kuwawezesha viojana kujiajiri

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

UMOJA wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar umewaagiza Makatibu wa umoja huo katika Mkoa wa Kusini Unguja kusimamia mchakato wa kuanzisha vikundi vya Ujasiria Mali ili Vijana wapate fursa za kujiajiri.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo  Zanzibar, Abdulghafar Idrissa katika ziara Maalum iliyofanyika Mkoa wa Kusini Unguja ya kuwashukru wafuasi wa CCM na wananchi kwa ujumla waliokipa nafasi ya kurudi madarakani Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio Zanzibar.

Amesema njia pekee ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini ni lazima kuwepo na mipango  mbadala ya kubuni fursa za ajira kutoka katika mazingira yaliyowazunguka kwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili vijana waweze kujiajiri wenyewe.

Abdulghafar ameeleza kwamba makatibu wa umoja huo wanatakiwa kusimamia ipasavyo mchakato wa kuanzisha vikundi mbali mbali vya ujasiriamali vitakavyowaunganisha vijana wa UVCCM katika jukwaa moja ili waweze kupata fursa za mikopo kwa urahisi kutoka serikalini itakayosaidia vikundi hivyo.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo, amefafanua kwamba tatizo la ajira ni changamoto ya kidunia sio Zanzibar pekee kwani serikali ina uwezo wa kuajiri wananchi 27,000 wakati idadi ya watu wote inakadiliwa wastani wa wananchi milioni 1.5, hivyo nafasi za ajira ni chache hali inayotakiwa wananchi kutafuta fursa nyingine za kujiajiri wenyewe.


Akizungumzia lengo la ziara hiyo amesema UVCCM inawashukuru wananchi wote  hasa waliokiamini na kukipa ridhaa Chama cha Mapinduzi Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Marudio na kupata  kikapata ushindi wa zaidi ya asilimia 91.

Amesema ushindi huo umetokana na nia ya dhati ya wananchi walioichagua CCM kutokana na utekelezaji wake mzuri wa Ilani za Uchaguzi za chama hicho katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

 Amesema CCM bado ina mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha kila mwananchi anapata maisha bora yanayoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ziara hiyo inaendelea  katika Zanzibar nzima kwa upande wa Unguja na Pemba kwa lengo la kuwashukru na kukutana na wananchi wote na makundi ya vijana walioshiriki katika zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Marudio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.