Habari za Punde

Wananchi wa Mwera Kikokwani hatarini kuangamia na KipindupinduNa Mwandishi Wetu, Zanzibar.

BAADHI ya Wananchi wa Shehia ya Mwera Kikokani Wilaya ya Magharibi “A” Unguja wameiomba serikali kuwatembelea wahanga wa mafuriko wa maeneo hayo ili kufahamu changamoto zinazowakabili  kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu, kabla hawajapata maafa makubwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamedai kuwa toka wamepata mafuriko takriban wiki mbili zilizopita hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyeweza kufika katika eneo hilo kwa kuwafariji ama kutoa msaada wowote wa kibinadamu.

Akizungumza mmoja wa wakaazi wa eneo hilo, Kadika Khamis alisema kuwa yeye ni miongoni mwa wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo na kuhama nyumba yake  baada ya kujaa maji ambapo kwa sasa ameomba hifadhi kwa jamaa zake.

Khamis alisema chanzo cha Mafuriko hayo ni kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kujaza maji katika bonde la Mtofaani ambayo njia yake imezibwa na ujenzi wa barabara pamoja ujenzi holela na kusababisha maji hayo kuingia katika makaazi ya watu.

“Maeneo haya siyo sehemu ya mabonde na hayajawahi kujaa  maji wala kutokea mafuriko wakati wa msimu wa mvua, hivyo hii ni mara ya mwanzo lakini  imesababisha hasara kubwa kwani mpaka sasa tumehama makaazi yetu na hatujui matatizpo haya yataisha lini kwani mpasa sasda babo maji yapo katika majumba yetu kama mnavyoyaona.”, alisema Khamis.

Kwa upande wake, Rajab Simai alisikitishwa na kitendo cha viongozi wa serikali hasa viongozi wa jimbo kushindwa kuwatembelea wananchi hao ambao kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu.

Alisema kwamba kutokana na mafuriko hayo kwa sasa wananchi hawana huduma muhimu za kibinadamu zikiwemo malazi, chakula na maji safi kwani vyote vimeangamizwa na maafa hayo.

“ Tunawaomba serikali kuu waje wafanye japo ziara huku na kutuona maisha tunayoishi kwani watu wamehama katika nyumba zao wengine zimeanguka, na tunaishi maisha magumu tunahitaji msaada.”alisisitiza Simai.

Simai alieleza kwamba kutokana na maji yaliyotwaama katika maeneo hayo ambayo ni makaazi ya watu na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya maji safi kuna hatari ya wananchi kupata maradhi ya kipindupindu kwani maji wanayotumia kwa sasa siyo salama na hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumzia hali hiyo Balozi wa nyumba kumi, Sharifa Hassan Ali alikiri kuwepo kwa uharibifu wa makaazi ya wananchi uliosababishwa na mvua za mafuriko zilizonyesha siku kadhaa zilizopita.

Alisema kwamba baada ya kutokea hali hiyo alipeleka taarifa kwa Sheha wa Shehia ya Mwera ili aweze kukagua na kuhesabu nyumba zilizoathirika na kupeleka taarifa hiyo kwa ngazi za juu serikali lakini hawakupata mrejesho wowote mpaka sasa.

Sharifa alisema kwamba kutokana na hali iliyopo katika eneo hilo kuna baadhi ya wananchi wanatumia muda mwingi kuwachunga watoto wao wasiende kuchezea maji machafu yaliyotwaama katika eneo hilo ili wasipate maradhi ya kipindupindu.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia hiyo, Khamis Bilal Risasi alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kufafanua kwamba yeye baada ya kupata taarifa za maafa hayo alienda kukagua na kuwafariji wananchi waliopata maafa hayo.

Alipoulizwa suala la kutotoa ushirikiano kwa wahanga wa mafuriko hayo, alikanusha na kueleza kwamba yeye ni miongoni mwa viongozi wa serikali walioenda kukagua sehemu ya tukio hilo.

“ Hao wananchi wanaosema kwamba eti hakuna kiongozi yeyote aliyefika katika eneo hilo kuwafariji sio kweli mimi pamoja na mwakilishi wa jimbo letu tulienda kuwakagua na tukawataka waliokuwa hawana sehemu za kuishi tuwatengenezee kambi huko Beit-el-sie wakakataa”. Alieleza Sheha huyo licha ya kutoweka wazi kama taarifa hizo alizifikisha Idara ya Maafa Zanzibar au la.


Alisema kuwa robo tatu ya eneo la shehia ya Mwera limezungukwa na mito ya maji pia kuna baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya juu wamejenga katika miundombinu ya kusafirisha maji ya mvua hivyo mvua zikinyesha nyingi maji hayo yanakosa njia za kupita na kupelekea kuvamia makaazi ya wananchi wasiokuwa na hatia.

Aidha alipoulizwa suala la kuwepo kwa huduma za dawa za kutibu maji(water gurd) na vyandarua vya kuwagawia wananchi, alisema kuwa aliwahi kupewa vidonge 300 ambavyo havikukidhi mahitaji kwani aliwagawia baadhi ya  wananchi waliopo katika mazingira hatari ya kupata kipindupindi na mgao wa vyandarua alisema shehia hiyo haijapata.

Akizungumzia maradhi ya kipindupindu Sheha Risasi aliwasihi wananchi wa maeneo hayo kuweka mazingira yao katika hali ya usafi kwa kutumia vyoo vilivyokuwa katika sehemu salama pamoja na kuchemsha maji kabla ya kuyatumia ama kunywa ili kujikinga na maradhi ya miripuko hasa kipindupindu.

Zaidi ya Nyumba zinazokadiliwa kufikia 70 zimekubwa na mafuriko hayo na kati ya hizo nyumba 40  wakaazi wake wamehama kutokana na maji kuingia ndani ya nyumba hizo na kuharibu mali na miundombinu mbali mbali zilizokuwemo katika nyumba hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.