Habari za Punde

Fursa za Kiuchumi ni Changamoto kwa Watu Wenye Ulemavu -Mhe. POSSI

Naibu Waziri, Ofisi  ya  Waziri Mkuu, Mhe. Dr. Abdallah Possi ( Mb) akizungumza wakati wa majadiliano ya jumla kuhusu  utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu. Mhe. Possi anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa  wa Nchi  Wanachama  wa Mkataba  wa Watu  Wenye Ulemavu. Mkutano huu wa siku tatu umeanza siku ya  Jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.  Wajumbe wengine katika  picha ni kutoka kushoto Mhe. Stella Ikupa Alex ( Mb), Mhe. Riziki Said Lulida ( Mb) na Mhe Elly Marko Macha ( MB).
Ujumbe wa Tanzania wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa  Tisa wa Mkataba wa Watu  Wenye  Ulemavu,  ufunguzi wa mkutano  huu  ulifanyika katika  Ukumbi Mkuu wa Mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mkutano huu wa siku tatu ajenda yake ni "Utekelezaji wa  Agenda  ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”. Unahudhuriwa na  Washiriki kutoka nchi 164   ambazo zimeridhia  Mkataba huu, Asasi zisizo za kiserikali pia  zinahudhuria katika  mkutano  huu ambao ni  maalum kwa watu wenye ulemavu wa aina zote.


Na  Mwandishi Maalum, New York

Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za 

Watu Wenye Ulemavu(CRDP),umeanza jana (Jumanne)  hapa 

Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  New York, Marekani.

Mada au  ujumbe wa Mkutano huu wa siku tatu ni “ Utekelezaji 

wa  Agenda  ya Maendeleo Endelevu (Agenda2030) Kwa Watu 

Wote Wenye Ulemavu:  Pasipo Kumwacha Yeyote”

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania katika Mkutano 

huu, unaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. 

Dr.Abdallah Possi(Mb). Wajumbe wengine ni Mhe. Riziki Lulinda( MB), Mhe. Elly Macha (Mb) Mhe. Stella Ikupa (Mb), Bi Josephine Lyengi, Kaimu Kamishna kuhusu watu wenye ulemavu na Bi.Ngusekela Nyerere,Afisa Mambo ya Nje, Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Akizugumza wakati wa majadiliano ya jumla mara baada ya hafla 

ya ufunguzi , Naibu Waziri. Dr. Abdallah Possi amesema, 

changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu nchini 

Tanzania, ni fursa za kiuchumi.

“Licha ya mafanikio kadhaa yakiwamo ya utungaji wa sera,  sheria 

na mabadiliko mbali mbali kuhusu watu wenye ulemavu, bado 

kunachangamoto nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa 

lengo la kuwapunguzia matatizo watu wenye ulemavu yakiwamo 

matatizo ya kutokuwa na fursa sawa na kuondokana na 

umaskini”. Akaeleza Naibu  Waziri

Na Kuongeza kwamba, Tanzania kama ilivyo kwa nchi yingine 

inakabiliwa pia na vipaumbele vinavyokinzana na ambavyo ni 

muhimu lakini vikiwa athiri zaidi watu wenye ulemavu.

Akavitaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na 

upatikanaji wa maji safi na salama, chakula, huduma za afya, 

elimu na ukosefu wa ajiria.

Vile vile Naibu Waziri ameeleza kuwa mtazamo husika kuhusu 

watu wenye ulemavu ni changamoto nyingine ambayo inatatiza 

ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika fursa mbali mbali za 

maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambazo wangeweza kunufaika 

nazo bila ya kujali hali zao.

Akizungumzia kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini 

Tanzania, Mhe. Dr.Possi, ameeleza washiriki wa mkutano huu 

kutoka nchi 164 ambazo zimeridhia mkataba wa watu wenye 

ulemavu kwamba,  watu wenye ulemavu nchini  Tanzania 

wanakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na vifaa saidizi 

ambavyo vingewasaidia na kuwawezesha katika shughuli zao za 

kila siku.

Vile vile akabainisha kuwa mwaka  2015, Tanzania ilikuwa moja 

ya wadhamini wakuu wa Azimio kuhusu watu wenye ualibino, 

azimio ambalo pamoja na mambo mengine limelenga katika 

kutafutia ufumbuzi baadhi ya changamoto zinazowakabili watu 

wenye ualibino katika maeneo mbali mbali yakiwamo ya elimu, 

afya na ajira.

“Bila ya kuwa na vifaa saidizi watu wenye ulemavu wa aina 

yoyote ile wanashindwa kupata fursa ambazo kwa kuwawezesha kuishi pasi utegemezi na hivyo kuchangia katika yao binafsi na maendeleo ya nchi yao” akasisitiza Naibu Waziri. Na akatumia fursa hiyo ya kuhimiza upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujitegemea.

Awali akifungua mkutano wa tisa wa Mkataba wa Watu Wenye 

Ulemavu,  Rais wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  

Bw.Mogens Lykketoft, amesema nchi ambazo zimeridhia mkataba huo zinaowajibu wa kuchukua hatua zote muhimu zikiwamo za maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

“Kila nchi mwanachama wa mkataba huu na asiye wamanachama 

anakazi ya kufanya, lakini katika dunia ya leo mafanikio hayamo 

katika mikono ya serikali peke yake” akasisitiza Rais wa Baraza 

Kuu la Umoja wa Mataifa.

Na kwa sababu hiyo ametoa wito kwa serikali zote pamoja na 

wadau mbali mbali kufanyakazi kwa pamoja kwa lengo la 

kuwawezesha watu wenye ulemavu zaidi ya bilioni moja.

Pamoja na hotuba kutoka kwa nchi wanachama, mkutano huu 

ambao ni wa siku tatu utakuwa na mijadala ya mapendekezo yenye 

mada tofauti. Mkutano huo pia  unashirikisha Asasi zisizo za 

kiserikali zinazojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.