Habari za Punde

Lipeni fidia kwanza kisha ujenzi wa barabara uanze: Jumbe

Na Haji Nassor, Pemba
KATIBU Mkuu wizara ya Ujezi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe amesema, kila mwananchi anaepaswa kufidiwa kwenye ujenzi wa barabara ya Ole –Kengeja apewa haki yake, ili ujenzi ukianza kusiwe na manun’guniko ya fidia.

Alisema hataki kuona ujenzi umeanza na kuna baadhi ya wananchi wakiilalamikia wizara, kwa kutolipwa fidia kwa kuathiriwa na ujenzi huo, ambao utakuwa wa kiwango cha lami.

Katibu Mkuu huyo alieleza hayo, alipokuwa akizugumza na Meneja wa mradi na Mhandisi wa ujenzi, kwenye barabara hiyo, eneo la Ole Kiyanga wilaya ya Chakechake, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku mbili, alioambatana na waziri wa ziara hiyo.

Jumbe alisema, hataki kuona wala kusikia wakati fedha zikiwa tayari kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, na kisha kukajitokeza mwananchi ambae hajafidiwa nyumba yake.

Alisema kuwa, anakumbuka sana ujenzi wa barabara ya Amani- Mtoni Unguja, ambao uliwahi kusita kutokana na sababu ya mwananchi mmoja, kudai haki yake ya fidia, hivyo anahofia na kwenye barabara hiyo, kusijejitokeza kama hilo.


“Mimi niwaombe Meneja na Mhandisi mjipange vyema na muhakikishe kila kitu kimekaa sawa, ili mkianza ujenzi hakuna kusita sita na hasa kwa sababu ya kutolipwa fidia waathirika wa ujenzi’’,alifafanua.

Meneja wa Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo Amina Mohamed Habibu alisema, zipo nyumba 65 ambazo zinapaswa kulipwa fidia, na tayari 13 katia ya hizo, wahusika wameshakamilishiwa hazki zao za fidia na 52 zilizobakiwa wanaandaa.

“Ni kweli wananchi 13 wameshapata haki yao, na waliobakiwa wasiwe na wasiwasi watapewa, maana fedha zipo ila taratibu ndio hazijakaa sawa sana’’,alifafanua.

Mapema waziri wa wizara hiyo inayoshughulikia ujenzi, Balozi: Ali Abeid Karume, alisisitiza mara tu taratibu zitakapokamilika, ujenzi huo uende kwa haraka, ili kuepuka vifaa kupanda bei.

Alieleza kuwa, vifaa vinaweza kupanda bei mara maoja na kusababisha gharama iliopangwa kupanguka, hivyo ni vyema uharaka wa kujenga uwepo.

“Mimi nashukuru kwa hatua mliofikia, na hasa nimeridhika kusikia fedha zipo, sasa lazima mkaze mkono mkijenga, maana vifaa kupanda bei ni mara moja’’,alifafanua Waziri.

Mapema Mhandisi ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa Opec, Amini Khalid, alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 35 ilianza kutajwa ujenzi wake tokea mwaka 2007.

Alisema inasimamiwa na mzalendo na wanatarajia baada ya kukamilika utiaji lami, itakuwa na upana wa mita7.5, na kuwaomba wananchi washirikiane ili wakamilishe kazi hiyo kwa wakati.

Wakati huo huo waziri huyo na ujumbe wake ulishuhudia uchakavu na uchafu uliopo kwenye nyumba za maendeleo ya Mtemani Wete, ambapo wizara inafikiria kuzifanyia matengenezo.

Kwa upande wake Mdhamini wa shirika la nyumba Pemba, Suleiman Hamad Omar, amemueleza waziri huyo kuwa, kumekuwa na hujuma za makusudi zinazofanywa na baadhi ya wanachi, wanaoishi kwenye nyumba hizo.

“Kuna taka taka zimetiwa kwenye eneo lenye miundombinu ya umeme na maji, yalioko chini ya nyumba hiyo, hali ambayo pia inasababisha kukaribisha maradhi ya miripuko’’,alifafanua.


Ujumbe huo wa wizara ya Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji ukiongozwa na waziri wake na katibu mkuu ulitembelea pia barabara ya Mtambwe, Finya, Pandani, Mgagadu –Kiwani, Ole- Kengeja, bandari za Mkoani na Wete.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.