Habari za Punde

Rais Mstaafu JK na Makamu wa Rais Balozi Seid Ali Washiriki Matembezi ya Kuchangia Mpango wa Fadhili Mtoto Asome.

Rais Mstaafuwa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakiyaongoza matembezi ya Tamasha la kuchangia Mpango wa Fadhili Mtoto Asome lililoandaliwa na Taasisi ya Binti Foundation Kinondoni Jijiji Dar es salaam.
Watoto wa skuli Nne za Wilaya ya Kinondoni wanaoishi katika mazingira magumu wakishiriki matembezi ya kuchangia Mpango unaowahudumia wa upatikanaji wa vifaa vyao vya skuli.
Rais Mstaafu wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi zawadi mwanafunzi Rehema Abdulla  wa darasa la Pili miongoni mwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambae amefanya vizuri kwenye mitihani yake.
Baadhi ya Wanafuzi wa skuli ya Hananifu, Mwananyamala Kisiwani, Kiwalani,Kumbu kumbu na Msasani wakifuatilia hotuba za Viongozi baada ya kumaliza matembezi yao.
Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Leaders Club Upanga Jijini Dar es salaam mara baada ya kumaliza kwa matembezi ya Tamasha la kuchangia mpango wa Fadhili Mtoto asome yaliyoandaliwa na Taasisi ya Binti Foundation.(Picha na – OMPR).
Na Othman Khamis 0MPR. 
Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungno wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete  alisema watoto wanaoendelea kusihi katika mazingira magumu nchini wanashindwa kuitumia vyema haki yao ya kupata elimu kutokana na sababu za unyonge unaowakabili.Alisema mazingira hayo ni miongoni mwa changamoto nyingi zinazowakumba baadhi ya watoto hao kukosa kufanya vyema katika masomo yao na hatimae wanalazimika kujiingiza katika vitendo viovu vinavyoishia kupata msongo wa maisha yao ya baadaye.

Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alieleza hayo wakati akizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi  wanaoishi katika mazingira magumu na mayatima wa skuli Nne za Wilaya ya Kinondoni Mjini Dar es salaam zilizo chini ya mpango maalum wa miaka minne wa kusaidiwa huduma za shule unaosimamiwa na Taasisi ya Binti Mtoto asome yaliyoanzia Mtaa wa Biafra kupitia Bara bara ya Ali Hassan Mwinyi na kuishia katika Viwanja vya Leaders Club Upanga Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam.


Alisema Vijana wengi Mayatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na umasikini wa kipato uliowakumba wazazi wao wanapata unafuu wa maisha pale Jamii inapoelewa wajibu wao wa kukisaidia kizazi hicho jambo ambalo huwapunguzia ukali wa maisha.

Rais Mstaafu huyo wa Tanzania ameipongeza Taasisi ya Binti Foundation chini ya Mkurugenzi wake Bibi Johar  Sadiq kwa uamuzi wake wa kuanzisha mpango wa kusaidia Watoto Yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu ambao tayari umeshaleta mafanikio na faraja kubwa kwa kundi la watoto hao.

Dr. Kikwete aliwaomba Viongozi, Taasisi za Misaada pamoja na Wazazi na Walezi kuunga mkono mpango wa Taasisi ya Binti Foundation katika kuhakikisha changamoto zinazowasumbuwa Watoto mayatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu zinakwisha au kupunguwa kwa kiwango kikubwa.

Rais Mstaafu wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amejitolea kuchangia kuwasomesha Watoto Kumi wanaopata huduma kwenye mpango huo wa miaka Minne wa Taasisi ya Binti Foundation.

Akitoa salamu za Wananchi wa Zanzibar katika  matembezi hayo yaTamsha la Hifadhi Mtoto asome Makamu wa ili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mtoto ana haki ya kutimiziwa haki yake ya kupaya elimu licha ya kwamba ina gharama katika kumsomesha.

Balozi Seif alisema kitendo cha kumuandalia mazingira mazuri ya elimu mtoto akiwa bado mdogo ndio njia sahihi ya kujengea uwezo wa kuwa kiongozi, mtaalamu au mtumishi bora katika maisha yake ya utu uzima.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefikia hatua ya kugharamia elimu ili watoto wawe na fursa pana  ya kusoma bila ya malipo kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo kwa ustawi wa Jamii na Taifa kwa ujumla.

Katika kuunga mkono mpango huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameahidi kuchangia shilingi Milioni 5,000,000/- zitakazosaidia kugharamia watoto 15 kwenye mpango wa Taasisi ya Binti Foundation ya kusaidia watoto wenye mazingira magumu.

Mapema Mkurugenzi wa Taasisi ya Binti Foundation Bibi Johari Sadiq alisema Taasisi yake imefikia hatua ya kuandaa mpango huo wa miaka minne wa kuwahudumia watoto wenye mazingira magumu na yatima kutokana na changamoto aliyoambana nayo yeye wakati akiwa mdogo baada ya kufiwa na wazazi wake.

Bibi Johar alisema mpango huo wa Fadhili Mtoto asome unahudumia  sare, viatu pamoja na vifaa vya masomo kwa watoto wapatao 500 walio kwenye Skuli Nne za Wilaya ya Kinondoni  ambapo kila mtoto Mmoja hupatia Vifaa vyenye gharama ya shilingi laki 300,000/- kwa kila mwaka.

Mkurugenzi huyo wa Binti Foundation alifafanua kwamba mpango huo ulioanza  mwaka 2014 kwa skuli za Mwananyamala Kisiwani, Kumbukumbu, Kiwalani na Hananifu zilizomo ndani ya Wilaya ya Kinondoni uko katika
majaribio wa miaka minne.

Alisema mafanikio ya mpango huo ndio mwanzo wa sfari ndefu ya Taasisi hiyo kuelekea kutoa huduma za Hifadhi Mtoto Asome katika Wilaya na Mikoa mengine Nchini Tanzania.

Mkurugenzi huyo wa Binti Foundation aliendelea kuwakumbusha Viongozi, Wazazi, Walezi na washirika wa Maendeleo hasa katika sekta ya elimu kuunga mkono taasisi hiyo katika azma ya kumkomboa kielimu Mtoto wa Tanzania.
Akisoma Risala ya Wanafunzi hao wa Skuli Nnne za Wilay ya Kinondoni Mmoja wa Wanafunzi hao Naomi Edison alisema licha ya elimu kutangazwa bure na Serikali Kuu lakini bado watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu wanaendelea kukabiliwa na matatizo mbali mbali muhimu.

Naomi alisema watoto wengi waliofiwa na wazazi na wale ambao wazazi wao wanakabiliwa na maisha duni wamekuwa wakiata taabu kwenye masomo yao kwa kukosa vifaa vya skuli kama sare na baadhi ya madaftari kitendo ambacho huwapa simanzi wakati wanapoendelea masomo yao ndani
ya kundi la watoto wenye kipatro kizuri.

Alisema matukio ya kubakwa,utumiaji wa dawa za kulevya, wivi na mambo mengi ya ajabu hufanywa na watoto wengi wenye mazingira magumu na waliofiwa na wazazi wao kwa kukosa muelekeo sahihi wa kuendelea na masomo yao baada ya kupoteza matumaini ya maisha yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.