Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi Sekta ya Umma (ZAPSWU)


Balozi Seif  akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Zapswu uliojumuisha wajumbe wa Baraza Kuu pamoja na Kamati Tendaji ya Chama hicho.
Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Nd.Ameir  Mwadini Nahoda.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akibadilishana mawazo na Uongozi Mpya wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma {ZAPSWU} uliofika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
(Picha na OMPR)

Na. Othman Khamis OMPR.
Ushirikiano wa karibu  wa mara kwa mara baina ya Vyama vya Wafanyakazi na Viongozi wa Taasisi za Umma  katika kutatua changamoto zinazowakabili Wafanyakazi  hasa maslahi yao ndio njia pekee inayosaidia kuwafanya watekeleze kazi zao kwa juhudi, maarifa na nidhamu.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akibadilishana mawazo na Uongozi Mpya wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma { ZAPSWU } uliofika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi alisema ipo migogoro kadhaa inayowasumbuwa Wafanyakazi katika sekta tofauti Nchini na kuitanzua kwake ni kutafuta suluhu inayotoa fursa kwa kuwakutanisha wadau wote ili kupata njia ya kukabiliana na migogoro hiyo kwa njia ya mazungumzo ya amani.

Akifafanua mgogoro wa muda mrefu  uliowakumba wafanyakazi wa shamba la Mipira Kichwele dhidi ya mwekezji wa shamba hilo { Agro Tec } waliotaka kujua Viongozi hao wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Balozi Seif alisema Wizara ya Fedha na Uchumi ndio iliyopewa jukumu na Serikali Kuu kuangalia hatma ya suala hilo.

Balozi Seif alisema Wizara ya Fedha kwa sasa inaendelea kutafakari namna ya kuukwamua mradi huo kwa kutafuta mbinu nyengine za uwekezaji  baada ya kampuni iliyokodishwa kuendesha mradi huo  kushindwa kuliendeleza na kuwaacha wafanyakazi wake njia panda.

Mapema Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi  wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar { ZAPSWU } Bibi Mwatum Othman alisema Chama hicho kipya ni mjumuisho wa vyama vya Wafanyakazi vitatu vya Raaw, Zadgu na Zipau.

Bibi Mwatumi alisema Viongozi na wanachama wa vyama hivyo wamefikia muwafaka wa kuwa na nguvu za pamoja za kuunganisha vyama hivyo ili kupunguza utitiri wa vyama uliokosa uwakilishi madhubuti.

Katibu Mkuu huyo wa Zapswu aliiomba Serikali kuu kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuangalia kwa kina Sheria ya utumishi wa Umma inayoelekeza Muajiri kumpatia Mkataba Mfanyakazi wakati anapoajiriwa kazi.

Bibi Mwatum alisema utaratibu unaotumika hivi sasa ni kwa muajiriwa kupewa Barua ya Ardhi-lhali kuthibitisha ajira yake inayotoa fursa pana kwa Muajiri kuchukuwa hatua  dhidi ya mfanyakazi wake wakati inapotokea hitilafu.  

Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi huo wa Zapswu uliojumuisha Viongozi wa Baraza Kuu na Kamati Tendaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Nd.Ameir  Mwadini Nahoda aliomba Uongozi wake kuendelea kupatiwa fursa kama hizo kwa lengo la kupunguza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wanaowasimamia.

Nd. Ameir alisema Mkutano huo umewapa faraja kubwa kiasi kwamba utafungua pazia jipya litakalotoa mwanga wa kufikia malengo na kupata ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuitumikia jamii.

Kampuni ya Agro Tec  iliyopewa shamba la Mipira Kichwele hadi inaingia kwenye mgogoro wa ugemaji wa utomvu kwa ajili ya mipira ilikuwa ikikabiliwa na madeni ya zaidi ya shilingi Milioni 284,839,982/- ikiwa ni pamoja na Mishahara ya wafanyakazi  wa mashamba ya Mipira Unguja na Pemba, fedha za Likizo pamoja na deni la  ZSSF kwa wafanyakazi wake katika kipindi kati ya miezi Mitatu hadi Minane.

Utafiti wa Kitaalamu unaonyesha kwamba umri wa ugemaji wa Utomvu kwenye Mipira iliyooteshwa tokea mwaka 1977 umekwisha na kupindukia uzalishaji kiuchumi.
Bei ya bidhaa hiyo ya mipira katika soko la kimataifa pia imeshuka chini kiasi kwamba haiwezi kuongezeka tena sambamba na kukumbwa na ukosefu wa ushindani kwenye soko hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.