Habari za Punde

Zantel yatoa msaada wa vitabu vya Uhandisi kwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume.

 Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Bwana Haji Abdulhamid akimuonyesha baadhi ya vitabu vilivyopo katika maktaba ya taasisi, Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Bwana Benoit Janin. Anayetazama kulia ni Mkuu wa Zantel upande wa Zanzibar, Mohamed Mussa.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Bwana Benoit Janin (kulia) akikabidhi hundi ya mfano Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Bwana Haji Abdulhamid. Anayetazama katikakati ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, bwana Idrissa Muslih Hijja.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Bwana Haji Abdulhamid (katikati) akionyesha ramani mpya ya taasisi ya Karume. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, bwana Idrissa Muslih Hijja na kutokea kushoto ni Mkuu wa Zantel upande wa Zanzibar, Mohamed Mussa akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Bwana Benoit Janin (kulia).



• Yazindua ofa mpya ya gharama nafuu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu

Zanzibar, Juni 3, 2016: Kampuni ya simu inayoongoza visiwani Zanzibar, Zantel leo imetoa msaada wa vitabu vya uhandisi kwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kama sehemu ya jitihada zinazofanywa na kampuni hiyo kumaliza tatizo la uhaba wa vitabu katika taasisi ya Karume na kusaidia utoaji wa elimu bora.

Taasisi ya Karume ilianzishwa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uhandisi kwa fani mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ufundi wa magari, umeme, kompyuta, mawasiliano na teknolojia ya uchukuzi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Zantel, Bwana Benoit Janin alisema msaada huo umelenga kusaidia taasisi ya Karume kuendelea kukuza taaluma yake ya mafunzo kwa kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu vya kujifunzia.


'Vitabu ni muhimu kwa ajili ya kuongeza maarifa na hivyo basi msaada huu utasaidia Taasisi hii kuendelea kutoa elimu bora na kuwahakikishia wanajumuiya wa chuo hiki upatikanaji wa dhana za kujifunzia kwenye mafunzo yao' alisema Bw.Janin.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume, Bwana Haji Abdulhamid aliishukuru kampuni ya Zantel kwa msaada wake akisema umekuja wakati muafaka kwani taasisi yake imekuwa inakabiliana na changamoto za uhaba wa vitabu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi zaidi ya 1,500 ilionao sasa.

'Swala la uhaba wa vitabu katika chuo chetu limechangia kupungua kwa ufaulu na uelewa katika masomo ya sayansi ’ alisema Bwana Haji Abdulhamid.

Pamoja na kukabidhi msaada huo, kampuni ya Zantel pia imeanzisha mpango maalumu wa kushirikisha wafanyakazi wake kwa kutoa semina kwa wanafunzi ili kubadilishana mawazo na kuwaongezea ujuzi na uzoefu wanafunzi walio vyuoni.
Pamoja na makabidhiano ya msaada kampuni ya Zantel pia imezindua huduma mpya kwa ajili ya wanafunzi wa vyuoni ili kuweza kukidhi mahitaji yao ikiwemo kupata gharama nafuu za kupiga simu, kutuma ujumbe pamoja na mtandao na hivyo kuboresha na kuimarisha  mazingira ya kujifunzia.
 'Ofa hii ni kwa ajili ya wanafuzi wa vyuoni imezingatia uwezo wao kiuchumi kwa kuzingatia kipato chao pamoja na mahitaji na matumizi, lakini lengo haswa ni kuwapunguzia gharama ili kuwapa thamani ya fedha zao' alisema Bw.Janin.
ili kufurahia huduma hiyo mwanafunzi atatakiwa awe na laini ya Zantel na kujisajili kwa kutumia kitambulisho chake cha chuo kisha apige *149*1 # kujiunga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.