Habari za Punde

Dk Shein:Nitashirikiana na Dk Magufuli Kuhakikisha Tanzania Inabaki Kuwa Nchi ya Amani na Utulivu

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                            25 Julai, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia watanzania kuwa ataendelea kushirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki tulivu na salama kwa kuwa hakuna mbadala wa amani.

 “katika jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama nitaendelea kusaidiana na kufanyakazi na Mheshimiwa Magufuli kwa kadri ya uwezo nitakaojaaliwa na Mwenyezi Mungu na kama nilivyofanya na viongozi waliomtagulia” Dk Shein alieleza wakati akitoa salamau zake fupi kwa wananchi wa Dodoma kwenye maadhimisho ya siku ya Mashujaa.

Dk. Shein alifafanua kuwa utulivu na amani iliyopo ikitetereka haitakuwa rahisi kujenga upya hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushirikiana na serikali na viongozi kuhakikisha kuwa amani inaendelea kuwepo huko akihimiza upendo na mshikamano miongoni mwa watanzania.

Alisisitiza kuwa “watanzania wote ni wamoja na lengo letu ni moja la kujenga nchi yetu” na kutoa wito kwa watanzania kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli ambaye alisema amedhihirisha kuwa ni mtu wa vitendo kwa kuanza kuitekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

“Tulimsikia wakati wa kampeni, tumeanza kuviona vitendo vyake, sisi tumuunge mkono tuijenge Tanzania” alieleza Dk. Shein na kuwataka watanzania kuzingatia ujumbe alioutoa Mheshimiwa Magufuli katika salamu zake kwao kuadhimisha siku hiyo muhimu ya historia ya mapambano ya watanzania dhidi ya ukoloni pamoja na mchango wa watanzania katika ukombozi wa Afrika.

“Tuyazingatie maneno ya busara na hekima yaliyoelezwa na Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli na Rais Mstaafu Mzee Mwinyi ili tuendelee kuijenga nchi yetu”alieleza Dk. Shein.

Katika salamu zake kwa wananchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliwataka watazania kuwaenzi mashujaa wa walipoteza maisha yao katika kuipigania nchi yetu kwa kuendeleza amani na utulivu, kuzidisha upendo miongoni mwao bila kujali dini,kabila au vyama vya siasa.

“waliopigana na kupoteza maisha yao walifanya hivyo bila ya kujali dini zao, makabila yao wala vyama vyao bali walithamini na kujali utanzania wao hivyo nasi tuwaenzi kwa kuendelea kuiweka Tanzania katika amani na utulivu” Dk. Magufuli alieleza.

Ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki maadhimisho hayo tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli alisema maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuwa tunaonesha upendo na kuthamini watazania wenzetu walipoteza maisha kuikomboa nchi yetu na wengine waliopoteza maisha kulitumikia jeshi letu nje ya nchi.

“wako walipoteza maisha kwa kuikomboa nchi yetu, waliopoteza maisha katika Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, wako waliopoteza maisha yao wakati wakimtoa nduli Iddi Amin alievamia nchi yetu na wako walipoteza maisha katika ukombozi nchi marafiki wote hao ni mashujaa wetu tunawakumbuka” Dk. Magufuli alieleza.

Wakati huo huo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi alitoa wito kwa wananchi kumuunga mkono Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika hatua zake za kushughulikia kero za wananchi na kumpongeza rais huyo kwa kazi nzuri anayoifanya kuwatumikia wananchi.

Rais huyo mstaafu alieleza kuwa Dk. Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake ameonesha kwa vitendo uwezo mkubwa wa uongozi na kuwataka wananchi kwenda nae sambamba kwa kufanyakazi kwa bidii kufikia malengo.

Akizungumza pia katika hafla hiyo Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Dk. John Samwel Malecela alimpongeza Rais Magufuli kwa kuonesha dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi na kuelta maendeleo nchini.

“sisi tunakupongeza sana na tunakuhakikishia kuwa tuko bega kwa bega nawe na tumefurahishwa na kauli yako ya kutekeleza uamuzi serikali yetu tangu enzi za Mwalimu wa kuleta makao makuu ya sweriklai hapa Dodoma” Dk. Malecela alieleza huku akionesha kuipokea klwa furaha kauli hiyo ya Mheshimiwa Magufuli ya serikali kuhamia Dodoma.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.