Na Mwandishi wetu
BENKI ya Watu wa
Zanzibar (PBZ) imesema mtaji wake umeimarika kutoka shilingi milioni 16 wakati
ikianzishwa Juni 30, 1966 hadi shilingi bilioni 40 Juni 30, 2016 huku
faida katika kipindi cha Januari hadi
Juni mwaka huu ikifikia shilingi bilioni 8.
Mkurugenzi Mtendaji
wa benki hiyo, Juma Ameir, alisema hayo katika hafla ya miaka 50 tokea
kuanzishwa benki hiyo iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Aidha alisema
katika kipindi cha Januari-Judi mwaka huu, benki imelipa kodi serikalini
inayofikia shilingi bilioni 2.6.
Alisema katika
kipindi cha miaka 50 benki imeimarisha zaidi huduma zake baada ya kuwa benki
kamili ya biashara ikiwemo kuongeza vituo vya kutolea huduma na mashine za ATM,
ambapo hivi karibuni itaweka kituo cha huduma katika kijiji cha Kiwengwa mkoa
wa kaskazini Unguja.
Pia benki itaongeza
mashine za ATM katika maeneo ya Kibweni, Kivunge, Mperani na Baraza la
Wawakilishi pamoja na kuanzisha mawakala
wa benki (agency banking) na mfumo wa kukusanya mapato ya serikali.
Hata hivyo, licha
ya mafanikio hayo, alisema benki bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo
baadhi ya huduma kuendelea kutolewa kwa mfumo wa kizamani (manual).
Aidha alisema pia
benki inakabiliwa na changamoto za kimahakama, ambapo baadhi ya wateja
wanaodaiwa na benki wanaposhindwa kulipa deni benki huamua
kuchukua mali zao kwa ajili ya kufidia.
Hata hivyo, alisema
wateja hao huamua kukimbilia mahakamnani hali inayosababisha kesi kukaa muda
mrefu huku benki ikishindwa kurejesha deni lake.
Aliiomba serikali
kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, akisema kama serikali haitakubali
kuwapunguzia mzigo wa kodi hawataendelea na watakuwa hawakubaliki kukopeshwa
katika taasisi za fedha.
“Mfumo wa sasa wa
kodi haubagui mfanyabiashara mdogo, wa kati wala mkubwa, wote walipa kiwango
sawa, sasa hii haiwezi kuwasaidia wafanyabiashara wadogo, lazima serikali
iwaangalie hawa vyenginevyo hawawezi kukua na ni vigumu kukopesheka.
Mapema Naibu Katibu
Mkuu wizara fedha na mipango, Ali Khamis Juma, aliwataka wafanyakazi wa benki hiyo
kuendelea kuchapa kazi ili benki ipate mafanikio zaidi.
Wakati huo huo,
benki hiyo benki hiyo imetoa msaada wa vyakula, magodoro na mashuka kwa taasisi
mbali mbali za serikali na binafsi.
Taasisi zilizofaidika
ni Chuo cha Mafunzo ambacho kilipatiwa magodoro 100, hospitali ya wagonjwa wa
afya ya akili ambayo ilipatiwa mashuka 200 na tende.
Kijiji cha kulelea
watoto (SOS) kilipatiwa tani moja ya unga wa ngano, sukari nusu tani, mchele
nusu tani na mafuta ya kupikia lita 250.
Mayatima
wanaolelewa katika nyumba ya mayatima Mazizini walipatiwa kilo 200 za unga wa
ngano, sukari kilo 10, mchele kilo 100 na mafuta lita 50.
Taasisi nyengine
zilizofaidika ni pamoja na Isla Centre iliyopo Mpendae ambayo inajishughulisha
na kutunza watoto, Omar Bin Khatab iliyopo Fumba, kituo cha mayatima cha
Magogoni Chake Chake.
No comments:
Post a Comment