Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Balozi wa Cuba Nchini Tanzania na Uogozi wa Wazira ya Habari Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez Tormo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Viongozi hao walipata fursa pana katika kubadilishana mawazo juu ya umuhimu wa kuimarisha sekta ya afya Visiwani Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akizungumza na Watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari, Mh. Rashid Ali Juma, Naibu Waziri wa Wizara Mh. Choum Kombo Juma, Katibu Mkuu Omar Hassan Omar, Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Nd. Rafii Haji, Mkurugenzi  Masoko Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dr. Miraji Ukuti Ussi na Mkuu wa Chuo cha Habari  Zanzibar Nd. Chande Omar Omar.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR.
Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez Tormo amesema Madaktari sita Mabingwa wa Nchi hiyo wanatarajiwa kuwasili Zanzibar mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kutoa huduma za Afya pamoja na mafunzo kwa Madaktari wanafunzi Wazalendo wanaopata elimu kupitia mpango wa mafunzo unaoratibiwa na Nchi hiyo.

Alisema Madaktari hao Mabingwa wataungana na wenzao Sita wanaoendelea kutoa huduma za afya hapa Zanzibar na kufanya idadi ya Madaktari hao Mabingwa wa Jamuhuri ya Cuba kufikia 12.

Balozi Jorge Luis Lopez Tormo alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakibadilishana mawazo na kugusia zaidi umuhimu wa kuimarishwa kwa Sekta ya Afya kwa lengo likiwa kustawisha  ustawi wa Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.

Alisema Madaktari hao hivi sasa wako katika matayarisho ya mwisho kukamilisha mitakaba yao kwa ajili ya kuanza kazi hiyo ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Alifafanua kwamba hivi sasa Madaktari  Wanafunzi 12 Wazalendo wa Zanzibar  wanaopata mafunzo ya muda mrefu katika fani ya Udaktari chini ya usimamizi wa Taaluma hiyo kutoka kwa  Madaktari Mabingwa wa Cuba wako katika hatua za mwisho kukamilisha mafunzo yao Kisiwani Pemba.

Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania amefurahia Ukimwa wa amani uliopo Visiwani Zanzibar  ambao mbali ya kutoa fursa kwa Wananchi kuendelea na harakati zao za kujitafutia maendeleo lakini pia utatoa nafasi pana kwa Madaktari hao wa Nchi yake kutekeleza vyema majukumu yao kwa matumaini wawapo Zanzibar.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba wazo la Serikali ya Jamuhuri ya Cuba la kuijengea Uwezo Zanzibar kuwa na Madaktari wake mabingwa limeanza kuleta matumaini.

Balozi Seif alisema wazo hilo limekwenda sambamba na mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya wa kuimarisha sekta ya afya itakayopatikana umbali usiozidi Kikomita Tano ili  kuwaondoshea usumbufu Wananchi  wake katika kupata huduma hizo.

Katika mpango wa kuimarisha huduma hiyo muhimu Balozi Seif  alimueleza Balozi wa Cuba Nchini Tanzania kwamba alikutana na Waziri wa Afya wa Cuba wakati wa safari yake ya kawaida ya Uchunguzi wa Afya ya kila mwaka nchini humo hivi karibuni na kuiomba Cuba kuendelea kuisaidia Zanzibar kwa kuipatia Madaktari Mabingwa 16.

Alisema msaada huo unaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa nia ya Wizara ya Afya Zanzibar ya utanuzi wa chuo chake cha Afya kitaaluma utakaoondoa upunguza wa watendaji na wataalamu wa sekta hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania kwamba Zanzibar  kwa kipindi hichi imetulia na kuendelea kuwa ya amani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.