Habari za Punde

Zatakiwa Taasisi za Kiraia Kusaidia Madrasa Zanzibar Kukuza Elimu ya Dini.

Na Rahma/ Khamis Maelezo –Zanzibar.
Walimu wa Madrasa za Qur-an wamezitaka Taasisi za kiraia zenye uwezo  kusaidia Madrasa za kiislamu kwa lengo la kukuza na kuiendeleza Dini ya kiislamu nchini.

Wito huo umetolewa na Msaidizi Mwalimu Mkuu Muhdin Rajab Ramadhan wa Almadrasat Twarikat Ir-shaad Almuslimiin huko Ofisini kwake Tunguu kwa Shemego wakati alipokuwa akieleza changamoto zinazowakabili katika Madrasa hiyo.

Amesema baadhi ya watu wenye uwezo husaidia elimu ya dunia na kusahau kabisa Taasisi za kiislamu ambazo zinasaidia  kuwakuza watoto katika malezi bora ya Duniani na Akhera.

Aidha amefahamisha kuwa madrasa za kiislamu ndizo za kupewa kipaumbele  kutokana na kuwajengea uwezo na msingi mzuri  watoto kuwa na madili mema hasa katika kipindi hiki ambapo watoto wengi huporomoka kimaadili.

Mwalim Rajab amesema kuwa licha ya kuwafundisha malezi, wanakabiliwa na upungufu  wa madarasa ya kufundishia, ukosefu wa  Ofisi, vyoo na vifaa  muhimu ikiwemo Computer  pamoja na ushirikiano mdogo kwa baadhi ya wazazi na walezi hasa katika suala la michango ya wanafunzi.

“Wazazi unapowaita  kwa ajili ya  michango  hawahudhurii ipasavyo jambo linalorejesha nyuma kwani husababisha  waalimu wanaotoka masafa ya mbali kushindwa kufika  na kupelekea kutoa fedha mifukoni mwetu ili tuwasaidie  kufika madrasa,” alisema mwalimu Rajab.

Hata hivyo amefahamisha kuwa Madrasa yao ina vyumba sita, viwili  vya maandalizi  na vinne  msingi na wanafundisha masomo ya dini na masomo ya skuli asubuhi na jioni kutokana na wingi wa wanafunzi na kupelekea usumbufu.

Ameeleza kuwa pamoja na changamoto hizo wameweza kuiendeleza madrasa hiyo hadi kufikia kuanzisha Skuli  na kusaidia  kuzuwia  watoto kuzurura ovyo mitaani.,

Nae Mwalimu Mkuu wa Madrasa hiyo Juma Mussa Juma amewaasa wazazi na walezi kutojishirikisha na  masuala ya siasa na badala yake kujenga ushirikiano kati yao ili kuendeleza madrasa yao.

“Kuna baadhi ya wazazi na walezi wanajishirikisha na itikadi za siasa na masuala yasio ya msingi na kupelekea kukosa baadhi ya misaada kupitia viongozi wa jimbo,  hili linatukera sana kwani sisi hatupendi kuchanganya dini na siasa katika suala la maendeleo,” mwalimu mkuu amesisitiza.

Pamoja na hayo, Mwalimu mkuu huyo ameiomba Serikali msaada wa kuwajengea uzio katika eneo la madrasa kwani ipo karibu na barabara jambo ambalo litapelekea kuhatarisha usalama wa wanafunzi wao.

Baadhi ya wazazi na walezi wamewaomba walimu wa madrasa hiyo kuwa wastahamilivu kwani wanafahamu  umuhimu wa michango kwa maendeleo ya watoto wao lakini  baadi ya wakati wanachelewa kutokana na hali  ngumu ya maisha inayowakabili.

Almadrasat Twarikat Ir-Shaad Almuslimiin imeanzishwa mwaka 1996 na wanafunzi 40 na hivi sasa wamefikia wanafunzi 330  na walimu 14 na inafundisha masomo ya sira, fiqhi, Computer,  mazingira, kiarabu, hadithi za Mitume na masomo kwa vitendo.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.