Habari za Punde

DK. Shein Awataka Viongozi wa Wizara ya Elimu Kuwa Karibu na Taasisi za Elimu Zilizo Chini Yao.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                      06 Septemba, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali umetakiwa kuhakikisha kuwa unatumia muda wake mwingi katika maeneo ya taasisi za elimu badala ya kukaa maofisini.

Wito huo umetolewa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akifunga kikao cha kujadili Mpango wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2015-2020) kwa sekta ya elimu.  

“Skuli ni wanafunzi nendeni maskulini mkazungumze nao, mkazungumze na walimu mjue mazingira yao ya kazi na changamoto zinazowakabili” Dk. Shein aliueleza uongozi wa Wizara hiyo.

Alisisitiza kuwa usimamizi wa elimu maskulini usiachwe tu kwa wakaguzi wa elimu badala yake viongozi nao kuanzia waziri hadi wakuu wa Idara wafanye ukaguzi wa mara kwa mara na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo kasoro nyingi zitaweza kuepukwa.

“Tunazungumzia watoto kutofanya vizuri. Sababu zipo lakini tunashindwa kuzifahamu kwa kuwa tuko mbali na skuli zetu” Dk. Shein alisema na kusisitiza kuwa viongozi wa wizara wanapaswa “kuwa karibu na skuli na taasisi za elimu zilizo chini yao” kwa kuwa itakuwa rahisi kuzielewa na kuzifanyia kazi kasoro zinazojitokeza.

Kuhusu utekeleza wa Ilani, Dk. Shein aliutaka uongozi huo kufanyakazi kwa bidii na umakini mkubwa ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Ilani pamoja na ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni ili ifikapo mwaka 2020 tathmini ya utekelezaji iweze kufanyika kwa uhakika.

“”Tunahitaji umakini katika kupanga na kutekeleza malengo hivyo ni lazima malengo yetu tuyaweke katika hali ambayo mwishoni tutaweza kuyapima na kutoka jawabu sahihi juu ya utekelezaji wake” Dk. Shein alisisitiza.  

Katika hatua nyingine Dk. Shein ameutaka uongozi wa wizara ya Elimu kukiimarisha kitengo kinachoshughulikia masuala ya elimu ya juu ambapo kwa maoni yake kitengo hicho kwa sasa utendaji wake hauendani na hali halisi ya mahitaji ya sasa ya elimu ya juu. Kwa hivyo alisisitiza uwepo wa mikakati mizuri na makini ya kulifanisha sual hilo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Riziki Pembe Juma alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa wizara yake itasimamia kwa makini utekelezaji wa Ilani hiyo kwa kuhakikisha kuwa unakwenda sambamba na mpango mkuu wa Elimu.

Aidha, alikieleza kikao hicho kuwa Wizara hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufinyu wa jengo la ofisi ambapo baadhi ya idara na vitengo vimelazimika kuhamia katika majengo la kukodi yanayoigharimu wizara hiyo fedha nyingi.

Akizungumza katika kikao hicho Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi na Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza umuhimu wa kuwepo kwa uwiano mzuri wa majukumu baina ya Wizara na ofisi zake ziliko kisiwani Pemba kwa vile ni wote ni wizara moja.
“Lazima kuwe na uwiano wa majukumu kati ya wizara na Ofisi ya Afisa Mdhamini Pemba ambaye yeye ni mratibu tu wa shughuli za Idara za wizara hiyo kisiwani Pemba” Dk. Abdulhamid alifafanua.

Kikao hicho ni mfufulizo wa vikao vya kujadili Mpango wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM ya Mwaka 20215-2020 ambapo jana alikutana pia kwa nyakati tofauti na uongozi wa Wizara za Afya, wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira; na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                                

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.