Habari za Punde

Jumuiya ya Kanga Matenity Trust Yaandaa Mafunzo kwa Madaktari wa Ganzi na Usingizi wa Zanzibar.

Mkufunzi wa mafunzo ya siku tatu ya Madaktari wa ganzi na usingizi wa Zanzibar Dkt. Lee Ngungi kutoka Kenya akielezea umuhimu wa taaluma ya ganzi na usingizi katika sherehe ya ufungaji wa mafunzo hayo iliyofanyika Hoteli ya Mazson Shangani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kanga Martenity Trust Dkt Mohd Hafidh (aliyesimama) akifunga mafunzo ya siku tatu  yaliyowashirikisha madaktari wa ganzi na usingizi wa Hospitali kuu ya Mnazimmoja yaliyofanyika katika Hoteli ya Manson Shangani mjini Zanzibar
Mshiriki wa mafunzo ya Ganzi na Usingizi Dkt. Mohd Rashid akikabidhiwa cheti na Mwenyekiti wa Kanga Trust  Mohd Hafidh.
Washiriki wa mafunzo ya Ganzi na Usingizi wakiwa katika picha ya pamoja (Picha na Makame Mshenga   Habari Maelezo Zanzibar),

Na. Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar 
                         
Mtaalamu wa Sayansi ya ganzi na usingiza  Dkt. Lee Ngungi kutoka Kenya amesema teknolojia ya taaluma  hiyo inabadilika kwa haraka hivyo kuna haja kwa madaktari wanaoshughulika na fani hiyo kuandaliwa mafunzo ya mara kwa mara ili kwenda sambamba na mabadiliko hayo duniani.

Dkt. Ngungi ambae alikuwa mkufunzi wa mafunzo ya siku tatu ya madaktari wa ganzi na usingizi wa Zanzibar yaliyofadhiliwa na Jumuia ya Kanga Maternity Trust  katika Hoteli ya Mazsons Shangani, amesema elimu kwa ajili ya madaktari wa kada hiyo inahitaji kupewa kipaumbele ili kuwajengea uwezo wa kuhudumia jamii kwa ufanisi zaidi.

Amesema lengo la teknolojia ya ganzi na usingizi kwa sasa hasa kwa upande wa mama wajawazito inapobidi  kufanyiwa upasuaji ni kuwawezesha  kujifungua bila matatizo na baada ya kupata fahamu wasiweze kupata maumivu makali.    

Dkt. Ngungi amezishauri jamii za nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki  kuunga mkono na kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali na Taasisi nyengine za Kimataifa na Kitaifa  za kuwapatia elimu madaktari wa ganzi na usingizi katika nchi zao.

Mratibu wa mafunzo hayo ambae ni Mkuu wa Kitengo cha ganzi na usingizi katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja Dkt. Khamis Wazir amesema mafunzo hayo ya kwanza, ndani ya kazi, kwa wafanyakazi wa kada hiyo Zanzibar yataongeza ufanisi katika kuhudumia mama wajawazito.

Ameishukuru Kanga Maternity Trust kwa kushirikiana na Hospitali kuu ya Mnazimmoja kufadhili mafunzo hayo na kusema kuwa wataalamu wa fani ya ganzi na usingizi wanahitaji vifaa na elimu zaidi  ili kupunguza vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Ameongeza kuwa wataalamu wa kada hiyo kwa kipindi kirefu walikuwa hawatambuliki  umuhimu wao lakini ametanabahisha kuwa wao ni muhimili mkubwa wa Hospitli hasa zinazoendesha upasuaji.            

Akifunga mafunzo hayo yaliyowashirikisha madaktari 25 wa ganzi na usingizi kutoka Hospitali za Unguja na Pemba, Mwenyekti wa Kanga Maternity Trust Dkt. Mohd Hafidh amesema akinamama wanapo beba ujauzito  wanakuwa na wakati mgumu na siku ya kujifungua shida inaongezeka hivyo wananchi wenye uwezo wa kusaidia nyenzo kuokoa maisha ya mama na mtoto kupitia Jumuia hiyo wanakaribishwa.         

Amesema mafunzo yaliyotolewa kwa  wataalamu wa ganzi na usingizi  kutoka Hospitali mbali mbali za Zanzibar ni kuthamini kazi nzuri wanayofanya na lengo ni kuwapatia  taaluma zaidi .

Ameahidi kuwa Kanga Meternity Trust itaendelea kusaidi ufanisi kwa wataalamu wa fani ya usingizi na ganzi ili kusaidia wagonjwa hasa akinama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.