Habari za Punde

Yanga Ipo Pemba ikijifua kwa ajili ya mchezo wao na watani wa jadi Simba


WACHEZAJI wa Timu ya Yanga ya Tanzania Bara, wakifanya mazoezi katika uwanja wa michezo Gombani, kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Timu ya Simba mchezo huo utakaopigwa Oktoba mosi katika uwanja wa Taifa wa Tanzania.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA.)

KOCHA Mkuu wa Timu ya Yanga Hans Van Pluijm, akiwa katika harakati zake za upangaji wa Koni za kufanyia mazoezi katika uwanja wa michezo gombani, katika kambi yao ya wiki moja kisiwani Pemba.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA.)

Na Abdi Suleiman, PEMBA.

BAADA ya Kuwasili Kisiwani Pemba jana mchana, hatimae mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania bara timu ya Yanga, imeanza rasmi mazoezi yake leo katika kiwanja cha michezo Gombani Kisiwani Pemba.

Timu hiyo baada ya kufika kisiwani hapa, iliweza kwenda moja kwa moja katika hoteli ya Pemba Misali sunset Beachi iliyoko nje kidogo ya mji wa Chake Chake Wesha, ambako hoteli hiyo imezungukwa na bahari.

Kikosi cha mabingwa hao wa Tanzania bara, wakiongozwa na kocha wao mkuu Hans Van Pluijin na Kocha msaidizi wa timu hiyo Juma Mwambusi na viongozi mbali mbali wa timu.

Timu hiyo jana jioni iliweza kufanya mazoezi katika ufukwe wa bahari iliko hoteli hiyo, kutokana na mazingira yake kuwa tulivu na ya kuvutia.

Yanga iliweza kufika katika uwanja wa Gombani saa mbili kamili za asubuhi, kwa ajili ya mazoezi hayo yaliyotumia muda wa masaa mawili hadi saa nne kamili kumaliza.

Timu hiyo ambayo ipo kisiwani Pemba kwa ajili ya kujiandaa dhidi ya mahasimu wao wa karibu timu ya Simba katika mchezo wao wa Oktoba mosi mwaka huu.

Yanga imekuwa na mafanikio mazuri kila inapowasili kisiwani Pemba, kwa ajili ya kambi yao kutokana na utulivu wa hali ya hewa na utulivu wa mazingira ya Pemba.

Hata hivyo timu hiyo haikutaka waandishi wa habari kupiga picha katika mazoezi yao, pamoja na kutokuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari kutokana na mazoezi yao kufanya siri zaidi.

Mmoja wa viongozi wao kwa masharti ya kutokutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema viongozi wakuu wamekataza waandishi wa habari kuchukuwa Picha, kwani wataweza kuharibu mipango ya mwalimu.

Alisema timu hiyo itakuwepo kisiwani Pemba kwa muda wa wiki moja, huku wakitarajiwa kufanya mazoezi siku mbili kwa siku asubuhi na jioni, ili kuwaweka wachezaji kuwa katika mazingira mazuri dhidi ya michezo yao ya mbele inayowakabili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.