Tulipofika
Mina nikaendelea na siku yangu ya tatu ya mafunzo, siku hii huitwa siku ya
kuchinja – Yawmun Nahr. Ndio siku yenye mafundisho mengi kuliko siku nyengine
za Hijja. Tuendelee
Nikaianza
safari yangu kuelekea Jamaraat (kupiga mawe) nikitokea Mina kwa miguu ni mwendo
wa nusu saa tu, lakini kutokana na msongamano wa watu jinsi walivyokuwa wengi
ilinichukua saa 1.30 kufika Jamaraat.
Siku
kila aliyekuja kuhiji hutakiwa kupiga mawe Jamaratul ‘Aqabah au kubra. Mnara
mkubwa katika minara mitatu iliyopo eneo la Jamaraat.
Nilifika
salama usalimini eneo la kupiga mawe (hii ni sehemu ya hatari katika sehemu
zote za hijja kwa kuwepo msongamano mkubwa kila mwaka ambao mara nyingi hupelekea
vifo vya mahujjaaj). Nikakoma kusema Talbiyah kwani kisheria nikifika sehemu ya
Jamaratul ‘Aqabah ndiyo sehemu ya mwisho ya kusema Talbiyah ambayo niliikuwa
nikiisoma tokea nilipovaa Ihraam siku ya tarehe 8 dhulhijjah.
Nikatafuta
sehemu muwafaka ya kurusha mawe kutokana na wingi wa watu na nilipoipata
nikaanza kurusha kijiwe cha kwanza huku nikisema: Bismillaah Allaahu Akbar. Nikafuatanisha
na chengine kwa kusema Allaahu Akbar pekee bila ya
bismillaah hadi nikamaliza vijiwe saba. Jamaratul kubra ukimaliza kupiga mawe
hutakiwi kusimama baada yake na kuomba du’aa kama ilivyo kwa minara mengine na
pia ni Jamarah pekee ambalo limeruhusiwa kupigwa kabla ya Zawaal siku ya iyd (kuchinja).
Nilipomaliza
nikaendelea na safari yangu kwa miguu kutoka Jamaraat hadi ‘Aziziyah kitongoji
kimojawapo kaskazini mwa Makkah tulipofikia. Kutokana na msongamano safari hii
pia ilinichukua takriban saa nzima.
Alhamdulillah
nikatumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yangu (kutoka kwa kiongozi wa kundi letu)
kwamba kichinjwa changu tayari kimeshachinjwa kwani hii pia ni mojawapo ya
Ibada inayotakiwa kufanyika katika siku hii au ziku za Tashriyq (yaani tarehe
11,12 na 13 Dhulhijjah). Nikaulizia nini maana ya Tashriyq? Nikajuulishwa na
wenye weledi na Hijja ni ile nyama inayochinjwa siku ya Eid huanikwa juani hadi
kukauka na kuhifadhiwa ndiyo maana yake. (kumbuka miaka hiyo hawakuwa na
majokofu ya kuhifadhi nyama kama tulivyo siku hizi)
Baada
ya kupumzika kidogo, nilikoga na kuvua Ihraam zangu kwani hapa tayari nimekuwa
nimetahallal (kutoka ihram) kidogo kwani nimeruhusiwa kufanya mambo yote
isipokuwa kustarehe na mke nikatakiwa kuendelea na mafunzo yangu kwa siku kwa
kuelekea Al Ka’abah kwa ajili ye kutekeleza nguzo mbili kuu za Hijja, kufanya
tawaaf kufanya Sa’iy.
Safari
yangu kutoka Aziziyah hadi Al Ka’abah ilinichukua saa 1.15 naam kwa miguu.
Nilipofika Al Ka’abah ambapo umati uliokuwepo hapo siku hii ukiteleza nguzo za
Hijja na umati mwengine ambao niliuacha Mina nikajisemea moyoni Alhamdulillaah,
haya ndio matunda ya kazi aliyoifanya Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi
Wasallam. Ninayoshuhudia kwa macho yangu ni ushuhuda kwamba Mtume Muhammad
Swalla ‘Allaahu ‘alayhi Wasallam amefikisha ujumbe na kutimiza amana aliyopewa
na Allaah ‘Azz wa Jall. Nina imani Allaah ‘Azza wa Jall anashuhudia kwamba
Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amefikisha ujumbe kama alivyoagizwa.
Nikaingia
msikitini kwa kuomba du’aa ya kuingia msikitini na kuelekea sehemu ya kuanzia
Tawaaf.
Tawaaf
ni ibada unayotakiwa uizunguke Al Ka’abah mara saba ukianzia sehemu lilipo jiwe
jeusi (Hajarul aswad). Unatakiwa kuzunguka ilhali Al Ka’abah ipo upande wako
kushoto ( anti clockwise). Ni mojawapo katika nguzo za Hijja na lazima ifanyike
veynginevyo Hijja haitosihi.
Tawaaf
ya nguzo huitwa Tawaaful Ifaadhah au Tawaafu Ziyaarah. Lazima uwe katika hali
ya tohara kabla ya kufanya tawaaf (uwe na udhu).
Sehemu
ya kuanzia imewekewa ishara ya taa rangi ya kijani pamoja na maelezo kwa
kiarabu kwamba hapa ndipo sehemu ya kuanzia na kumalizia Tawaaf. Nikaelekea
kona lilipo Hajarul Aswad (jiwe jeusi) na kuliashiria na kusema Allaahu ‘Akbar
na kuanza Tawaaf huku Al Kaabah ikiwa kushoto kwangu.
Siku
hii na umri huu na umati uliokuwepo sikuwa na ubavu wa kulifikia Hajarul aswad
na kulibusu kama alivyofanya Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi wasallam
nikabaki kuliashiria tu ambayo pia inakubalika kisheria. Kila nikifika Ruknil
Yamani (kona ya Yemen kona ya tatu kabla ya kona ya hajarul aswad) nilitakiwa
kuomba dua’a aliyotufundisha Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi Wasallam na
kusema: ` Rabbanaa aatinaa fiddunyaa hasanatan wafil akhirati hasanatan waqinaa
‘adhaaba Nnaar. (Mola wetu tupe katika dunia yaliyo mazuri na katika akhera
yaliyo mazuri na utuepushe na adhabu ya moto)
Umati
uliokuwepo ukifanya Tawaaf ukanikumbusha kwamba kwenye Baytul Ma’amuur,
mbinguni kuna umati kama huu wa Malaika nao ukifanya Tawaaf. Tofauti na umati
uliokuwepo baytul haraam na baytul ma’amuur ni kwamba umati wa baytul maa’muur
hufanya tawaaf mara moja katika uhai wao na hawarudi tena! Allaahu Akbar
Nikiendelea
kufanya Tawaaf kwa kuizunguka Al Ka’abah mara saba na kila nikifika eneo la
Hajarul aswad niliashiria na kusema Allaahu Akbar. Ilikuwa ni wakati wa
adhuhuri jua likiwa kali na tayari nimeshapata kufanya mwendo tokea Mina hadi
Jamaraat, Jamaraat hadi Aziziyah, Aziziyah hadi Al Ka’abah na sasa nikiendelea
na mwendo wenye kheri na Baraka wa Tawaaf, sikuhisi machofu ya aina yoyote.
Nilipofanya
Tawaaf na nikabahtika kuifanya kwenye Mataaf (sehemu ya chini ya kutufu karibu
na ‘Al Ka’abah) nilikuwa nnajiuliza inawezekana katika mojawapo ya sehemu
nimepita ni sehemu alipopita Mtume Swalla ‘Allaahu ‘alayhi wasallam alipofanya
Hijja yake kwa hivyo nimeweza kupata angalau Sunnah. Ila nitajuaje kama
nimeipatia?
Naam
kwenye Mataaf kuna msongamano, kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume lakini
yote haya hayakunijia katika mawazo yangu. Kilichokuwepo katika mawazo yangu ni
kupata fursa nadra ya kuwa karibu sana na Al ka’abah – nyumba ya kwanza
iliyoasisiwa kwa ajili ya Ibada. Allaahu Akbar! Kama ni unyenyekevu basi ukiwa
karibu na Al Ka’abah utaupata wa hali ya juu. Kama ni udhalili basi ukiwa
karibu na Al Ka’abah utaupata wa hali ya juu. Ni hisia ambazo haziwezi
kuelezeka mpaka uwepo mwenyewe karibu na nyumba ya Allaah ‘Azza wa Jall ndipo
utakapozifahamu hisia hizi. Kama bado hujafanya ibada ya Hijja ndugu yangu
katika Imani, jihimu na fanya haraka.
Nilipomaliza
kufanya Tawaaf ambayo ilinichukua takriban saa 1.15 nikatafuta sehemu nyuma ya
Maqaamu Ibrahim kwa ajili kusali Sunnah rakaa mbili, sikuipata kutokana na
zahma na msongamano. Nikatafuta sehemu tu na nikaswali rakaa mbili , rakaa ya
kwanza nilisoma Alhamdu na Qul Yaa ayyuhal Kaafirun na rakaa ya pili nilisoma
alhamdu na Qul huwa Llaahu ahad. Ndivyo alivyotufundisha Mtume wetu Swala
Allaahu ‘alayhi wasallam.
Baada
ya hapo nikaelekea sehemu yalipo maji ya zamzam, nikanywa kadri ya kiu yangu
huku kila nikinywa huomba du’aa. Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam
alituagiza tunapokunywa maji ya zamzam ni dawa ya maradhi na pia kujipangusa
katika sehemu za mwili.
Nilipomaliza
nilitakiwa kurudi tena na kulibusu Hajarul aswad lakini haikuwezekana kutokana
na msongamano nikabakia kuliashiria tu.
Itaendelea...
No comments:
Post a Comment