Bado
niko katika siku yangu ya tatu ya mafunzo na nilipomaliza funzo la Tawaaf nikaanza
funzo la Sa’iy.
Sa’iy ni kwenda matiti kati ya Jabal Swafaa na
Jabal Marwah. Milima hii imo ndani ya Msikiti ambako kumetengenezwa eneo maalum
la kjufanya ibada hii. Fundisho hili ni muhimu kwa ni mojawapo katika mambo
ambayo lazima niyafanye ili Hijja yangu ikamilike ni mojawapo ya nguzo za
Hijja.
Fundisho
hili lina mazingatio makubwa kwani linatukumbusha kisa cha mke wa Nabii
Ibrahiym ‘alayhis salaam alipomwacha mkewe bi Hajrah na mtoto mchanga Nabii
Ismaail ‘alayhis salaam kwenye jangwa lisilokuwa na chochote wakati huo. Na Bi
Hajrah alimuuliza Nabii Ibrahiym ‘alayhis salaam: “kwanini unatuacha hapa?” Nabii
Ibrahiym ‘alayhis salaam hakumjibu kitu mpaka alipomuuliza: “hivi ndivyo
alivyokuamrisha Mola wako?” Akajibu: “naam” basi Bi Hajra akasema: “Mola wetu
hatotuacha mkono”.
Ni
kisa kirefu ila fundisho muhimu ni pale Bi Hajrah alipoishiwa na maji na akawa
anatafuta kila upande akihaha huku na kule akienda katika ya Jabal Swafaa na
Marwah. Na kila akipita sehemu alipomwacha Ismaaiyl na kumsikia akilia
alizidisha mwendo kutafuta maji.
Naam
tunafanya Sa’iy kwa kumkumbuka mke wa Nabii Ibrahiym ‘alayhis salaam alipokuwa
akihangaika kutafuta, maji kwa ajili ya mwanawe.
Nikafika
Jabal Swafaa ambapo hutakiwa kuanzia na kumalizia Marwah. Nilipoweka mguu wangu
kwenye mlima Swafaa nikasoma aya Inna Swafaa walmarwata min sha’aairi Llaah,
faman hajjal bayta awi’itamara falaa junaah ‘alayhi an yatawwafa bihimaa, wamna
tattawa’a khayran, Fainna Llaah Shaakirun ‘aliym. (Suuratul Baqarah 158)
Nilipomaliza
nikasema kama alivyosema Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam – abdau bimaa
bada-a Llaahu bihi ( Ninaanza kwa kile ambacho Allaah alianzia)
Kisha
nikapanda Jabal Swafaa (ukitaka kulipata Jabal Swafaa itakubidi ufanye Sa’iy
chini na si kwenye ghorofa ya kwanza au ya pili) mpaka kufikia sehemu ambayo
ninaweza kuliona Al Ka’abah, nikaelekea qiblah na kisha nikaomba dua’a
aliyotufundisha Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam
Kisha
nikaanza kutembea kutoka Jabal Swafaa nikielekea Marwah ili kukamilisha
mzunguko mmoja.
Nilipofika
kwenye alama za taa za kijani (karibu na Jabal Swafaah) nikaongeza mwendo na
kwenda mwendo wa haraka (ni Sunnah kwa wanaume tu jambao ambalo pia hushangaza
kwani alietuletea utaratibu huu ni mwanamke , mke wa nabi Ibarhiym ‘alayhis
salaam) na zilipomalizika alama nikaendelea na mwendo wa kawaida hadi
nilipopanda Jabal Marwah nikasoma kama nilivyosoma nilipanza Jabal Swafaa na
kuendelea na sa’iy.
Nilikithirisha
kuomba du’aa na kumkumbuka Allaah ‘Azza wa Jall muda wote wa Sa’iy mpaka
nnamaliza.
Kila
nikijaribu kupata mazingatio katika Sa’iy naona tuna mengi ya kujifunza kwani
chimbuko la maji ya zamzam ni kutokana na Sa’iy aliyoifanya Bi Hajrah. Tukio
hili ambalo mamilioni ya waislamu duniani hulifanya kila mwaka ni limeanzia na
Bi Hajrah wakati alipokuwa akihangaika kwa ajili ya mwanaye mchanga. Kwanini
Nabii Ibrahiym ‘alayhis Salaam amuwache mkewe kwenye jangwa ambalo halina kitu
wala watu wala maji? Majibu ya masuala haya ndiyo hii nyumba ya mwanzo
iliyoasisiwa kwa Ibada. Allaahu Akbar.
Alhamdulillaah
nimemaliza fundisho muhimu la Hijja ambalo limehitaji kutumia mwendo wa miguu
kama ilivyokuwa Tawaaful Ifaadhah, kama ilivyokuwa safari yangu kutoka Mina
hadi Jamaraat, Jamaraat hadi Aziziyah, Aziziyah hadi Haram.
Naam
mwili sasa niliusikia kama umechoka na kipande cha kurudi Aziziyah nilipofikia
kilikuwa si kidogo kutembea kwa miguu na bado nitatakiwa kutembea tena usiku
kurudi Mina.
Niliamua
kuchukua Taxi na kurudi Aziziyah ambapo nilipofika kabla ya kupumzika
nilitekeleza fundisho jengine la Hijja la kunyoa nywele zote. Naam mara nyingi huwa sinyoi kipara, hupunguza
tu nywele zangu lakini ili Hijja yangu iwe na ubora niliamua kunyoa kwani Mtume
Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam aliwaombea du’aa mara tatu walionyoa na mara
moja waliopunguza.
Baada
ya kumaliza kunyoa sasa nimetahallal kikamilifu yaani yale mambo yote
niliyokatazwa wakati nipo katika Ihraam sasa nimeruhusiwa mpaka kustarehe na
mke .
Natumai
uliebahatika kusoma waraka huu utaweza kufaidika japo kidogo hasa kwa
kuzingatia ibra – mazingatio yanayopatikana katika Ibada ya Hijja na Umrah na
Allaah atuwafikishe katika kila lililokuwa na kheri kwetu.
Aamiyn
No comments:
Post a Comment