Habari za Punde

Dk Shein: Ongezeni kasi ya kuwaelimisha wananchi juu ya sheria ya ardhi na matumizi yake

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                 18 Oktoba, 2016


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kuongeza kasi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria ya ardhi kuanzia umiliki hadi matumizi yake ili wananchi wawe na uelewa mzuri zaidi kuhusu suala hilo.

Amesema ardhi kwa Zanzibar ni suala lenye umuhimu wa kipekee na wakati wote Serikali kupitia wizara husika haina budi kujikita katika kuwaeleza wananchi mipango na hatua mbali mbali ambazo inakusudia kufanya ili waende sambamba na mpango hiyo ya serikali.

Dk. Shein alitoa wito huo wakati wa kikao cha kujadili Utekelezaji wa Mpango kazi ya Wizara Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016-2017 (Julai-Septemba 2016) kilichofanyika jana Ikulu Zanzibar.

Katika mnasaba huo Dk. Shein ameiagiza wizara hiyo kufanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ambayo hayatumiki na kuyapima kwa lengo la kuyahifadhi ili kuepeka matumizi yasiyostahiki.

“Ni lazima ardhi yote itambuliwe na kupimwa kwani hakuna ardhi isiyokuwa na matumizi. Inawezeka kufaa kwa kilimo au makazi” Dk. Shein aliwaambia viongozi na watendaji wa wizara hiyo huku akisisitiza kuwa suala la ardhi kuwa ni nyeti na linahitaji mipango madhubuti.

Aliutahadharisha uongozi wa wizara kuwa hatua za haraka hazina budi kuchukuliwa kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi kwa kuwa wananchi kamwe hawataisubiri badala yake wataendelea kutumia ardhi kwa mujibu wa mahitaji yao ambayo yanaweza kuwa kinyume na mahitaji, malengo na mipango ya serikali.      

Kuhusu migogoro ya ardhi ambayo inasababisha kuwepo na kesi nyingi katika mahkama ya ardhi, Dk. Shein ametoa wito kwa wizara hiyo kuharakisha mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria Namba 7 ya mwaka 1994 na marekebisho yake ya Sheria Namba 1 ya mwaka 2008 ya Mahkama ya Ardhi ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha kesi nyingi za ardhi kuchukua muda mrefu kuhitimishwa. 

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Dk. Shein alihimiza kuendelezwa kwa jitihada za kuwaelimisha wananchi kuhusu uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi na namna zinavyoathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi kama vile maji.

Dk. Shein aliipongeza wizara hiyo kwa kufanyakazi kama timu na kuwataka viongozi na watendaji kuzidi kushikamana ili waweze kutimiza malengo ya wizara na kukidhi matarahji ya wananchi.

“Nimetiwa moyo sana na matokeo ya utekelezaji wa Mpangokazi wenu kwa robo ya kwanza na natarajia matokeo mazuri zaidi katika awamu zijazo kwa kuwa majadiliano yetu hapa yatawasaidia kufikia hatua nzuri zaidi ya utekelezaji” Dk. Shein aliwaambia viongozi na watendaji wa wizara hiyo wakati akifunga kikao hicho.

Akitoa utangulizi wa utekelezaji wa mpangokazi wa wizara yake, waziri wa wizara hiyo Salama Aboud Talib alisema kuwa wizara yake inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za maji, nishati na mazingira bora ya kuishi pamoja na kuimarisha matumizi mazuri ya ardhi.

Alifafanua kuwa jitihada hizo zinazingatia sera na malengo ya mipango mikuu ya Taifa na maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020, MKUZA II, sera za kisekta na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 -2020.

Katika kikao hicho, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisisitiza kwa wizara zote kuzingatia msingi wa mfumo huo ambao ni kupata matokeo halisi ya programu iliyopangwa na hilo litawezekana kwa “kupanga shughuli makhsusi katika programu hizo kabla ya kupata fedha na isiwe kinyume chake”.

Alieleza kuwa programu zote lazima zizingatie majukumu ya msingi ya kila idara na kupanga shughuli makhsusi za kufikia malengo ya idara ya mwaka mzima ambapo ifikapo mwisho wa mwaka wizara na idara zitaweza kujitathmini kwa ufanisi zaidi.

Dk. Abdulhamid alisifu Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa kuzingatia kwa kiwango kikubwa maelekezo ya mfumo huo kama yaliyotolewa na Ofisi yake lakini akaeleza matumaini yake kuwa katika vikao vijavyo wizara hiyo itafanya vizuri zaidi.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais masuala ya Ardhi na Mazingira Burhan Saadat alihimiza jitihada zaidi zifanywe katika kukomesha vitendo vya uchafuzi wa mazingira ambavyo matokeo yake ni athari kubwa kwa uhai wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema Wizara hiyo inafanya kazi nzuri na imekuwa ikiimarika mwaka hadi mwaka lakini inapaswa kuchukua hatua za ziada kuelimisha wananchi kuhusu shughuli zake ikiwemo mafanikio na changamoto inazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mshauri huyo alisifu utaratibu wa kupitia na kutathmini utekelezaji wa majukumu ya wizara na idara za serikali kila baada ya robo mwaka maarufu Bangokitita kwa kuwa umezisaidia sana wizara na idara hizo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwezesha kupata matokeo mazuri.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.