Habari za Punde

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI; MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA MAHAFALI YA PILI YA CHUO CHA MADAKTARI CHA ZANZIBAR NA YA 23 YA CHUO CHA TAALUMA ZA SAYANSI ZA AFYA-MBWENI ZANZIBAR, TAREHE 27 OKTOBA, 2016


Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Afya, 
Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib,
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Wabunge na  Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Dkt. Abdullah Ismail Kanduru, M/kiti wa Baraza la Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya,

Profesa Idris A. Rai, Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,

Wajumbe wa Baraza wa kilichokuwa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya,
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa nchi mbali mbali mliopo hapa,

Viongozi mbali mbali Mliohudhuria,
Wakufunzi, Wafanyakazi wa Chuo na wazee mliohudhuria,
Wageni Waalikwa, 
Mabibi na Mabwana,
ASSALAAM ALAYKUM

Kila sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanaadamu na akamfundisha mambo mengi asiyoyajuwa kwa kalamu. Ni wajibu wetu kumshukuru Yeye kwa kutupa hidaya ya uzima na akatuwezesha kukutana hapa leo hii, tukiwa  na afya njema na furaha.
Natoa shukurani zangu za dhati kwa uongonzi wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali   kwa maandalizi mazuri  ya hafla hii  na kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi. Kadhalika, shukurani maalum kwenu nyinyi wazazi na         2/     wageni waalikwa kukubali mwaliko wa kuja kujumuika nasi katika mahafali haya ambayo kama tunavyoona yamefana sana.
Mahafali ya leo ni ya aina yake; yatakumbukwa kwa kipindi kirefu kijacho kutokana na mambo mengi makubwa ya kihistoria tunayoyashuhudia leo. Kwanza tunashuhudia wahitimu wa vyuo viwili wakifanya mahafali haya kwa pamoja. Haya ni Mahafali ya Pili kwa Chuo cha Madaktari cha Zanzibar, na ya 23 kwa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya.  Haya ni  mahafali ya mwisho kwa vyuo vyote viwili. Mswada wa  kuviunganisha vyuo hivyo na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar tayari umeshapitishwa tarehe 28 Septemba, 2016 na tayari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametia saini na kwa hivyo, tayari ushakuwa sheria.  Nakupongezeni waandaaji na wahitumu kwa maamuzi na kwa kukubaliana kuyachanganya mahafali haya.  Hongereni sana.
Kwa hivyo, kwa wale wahitimu  12 wa  Chuo cha Madaktari cha Zanzibar ambao ndio wa mwisho kati ya Wanafunzi 50 waliopata mafunzo katika chuo hiki, mnapaswa kuyasherehekea  mahafali haya  kama ni sherehe za mafanikio makubwa  tuliyoyapata tangu  mwaka 2007 tulipokianzisha chuo hicho, hadi hivi leo tunapowakabidhi vyeti na kuwa tayari kukifunga rasmi.  Itakumbukwa kuwa mara ya mwisho tulikutana hapa tarehe 28 Septemba, 2014, miaka miwili iliyopita, kwa ajili ya mahafali ya kwanza ya wahitimu 38  kati ya wanafunzi 50  waliosajiliwa na kupata mafunzo katika Chuo cha Madaktari cha Zanzibar.
Vile vile, kwa wahitimu wa Chuo Cha Taaluma za Sayansi za Afya, nanyi mnapaswa kuyasherehekea mahafali haya ikiwa ni kumbukumbu ya mafanikio makubwa tuliyoyapata tangu mwaka 1938 ilipoanza rasmi historia  ya chuo hiki  hadi hii leo tunapofanya mahafali yake ya mwisho. Kwa upande mwengine,  sote tuliopo hapa tunayasherehekea mahafali haya ikiwa ni sherehe za kujiunga na SUZA rasmi. 
Ni muhimu tukafahamu kwamba,  mpango huu wa kuviunganisha  vyuo vyetu vya elimu ya juu na  SUZA ni mpango wa muda mrefu  ambao utekelezaji wake nimekuwa nikiutolea maagizo na maelekezo,  hatua kwa hatua tangu nilipotoa agizo  hilo mara ya kwanza, takriban miaka minne iliyopita.
Dhamira yangu ya kuviunganisha vyuo hivi imelenga katika kuweka utaratibu wa kisheria utakaoiwezesha Zanzibar kuwa na Chuo Kikuu kimoja cha Serikali  kitakachokuwa imara na chenye ubora na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za nchi. Kadhalika, nataka kuona kwamba wanafunzi wa Zanzibar wanapata mafunzo yaliyobora na kukabidhiwa                    3/..                  stashahada na vyeti vyenye kuheshimiwa na kutambulikana katika ngazi za Kimataifa. Nina imani ya dhati kuwa maamuzi haya yanakupeni  fursa, nyinyi wahitimu, iliyo pana na bora   zaidi  katika nyanja za taaluma na soko la ajira popote pale mtakapokwenda.  
Muundo huo mpya wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar utahusisha Taasisi ya Uongozi wa Fedha ambayo imefutwa na itatambulika kuwa ni Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Taasisi ya Maendeleo ya Utalii nayo imefutwa na  itatambulika kuwa ni Taasisi ya Maendeleo ya Utalii ya Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar pamoja na Chuo Cha Taaluma za Sayansi za Afya ambacho kimefutwa na kitatambulika kuwa ni Skuli ya Tiba na Sayansi za Afya ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.
Kwa hivyo, wahitimu ambao tunawatunuku Shahada zao leo na  wanafunzi nyote mtakaoendelea  na masomo yenu hapa mkiwa ni wanafunzi wa SUZA mna sababu ya kusherehekea kwa shangwe na vifijo  mahafali haya  ya kihistoria. Hongereni sana.
Imani yangu ni kuwa Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Profesa Idris  Rai ataendelea  kuiongoza SUZA  vizuri, akijuwa kwamba majukumu yameongezeka. Atafanya hivyo kwa kushirikiana na wakuu wa skuli na idara mbali mbali bila ya kuathiri malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuviunganisha vyuo hivi pamoja na kuzingatia maslahi ya wafanyakazi, ili  tuweze kupata mafanikio tunayoyatarajia. Tutaifanya kazi hiyo kwa mashirikiano ya hali ya juu na kila mmoja wetu atoe mchango wake ipasavyo. Kwa hivyo, nakuhimizeni kuwa msisite kuja kushauriana nami kwa jambo lolote lile lenye manufaa, kwa kadri mtakavyohisi inafaa.  Nakukaribisheni wakati wowote - karibuni.
Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi,
Kwa namna ya pekee, nachukua fursa hii kukupongezeni kwa dhati wahitimu nyote  kwa kuweza kumaliza masomo yenu kwa ufanisi mkubwa. Nimearifiwa kwamba leo nakukabidhini Shahada ya Udaktari vijana wetu  12 mliomaliza masomo yenu  ya udaktari kutoka  Chuo cha Madaktari cha Zanzibar na  vijana wetu wapatao 514 kutoka Chuo Cha Taaluma za Sayansi za Afya wa kada mbalimbali mkiwemo Wasaidizi Madaktari (Clinical Officers), Wauguzi, Maafisa wa Afya, Mafundi sanifu wa maabara na kadhalika.
Sote tunaelewa kwamba kusoma si kazi rahisi. Maisha ya kijanafunzi yana changamoto nyingi. Yanahitaji uvumilivu, bidii na akili yenye upeo wa kutafakari juu ya mambo muhimu ya maisha. Maisha hayo yanahitaji umakini mkubwa  katika kufanya upembuzi wa vipaumbele vya maisha.  Zaidi ya hayo maisha ya kijanafunzi yanahitaji akili yenye kusikiliza ushauri kutoka kwa  4/..    wazee, walimu na  kutathmini fursa za elimu zinazotolewa na Serikali na kuwa tayari kuzitumia vizuri. Naamini kwamba mmeweza  kufaulu vizuri kwasababu mmeweza  kufahamu vizuri wajibu wenu katika maisha ya ujanafunzi na mkafanya yale yaliyopaswa kufanywa kwa kuzingatia maslahi yenu, wazee na maslahi  mapana zaidi ya nchi yenu. Hongereni sana.
 Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi,
Ni dhahiri kwamba vyuo vyetu vyote viwili  vinavyotoa taaluma ya afya vina  historia ndefu na  muhimu. Tunajivunia vyuo vyote hivi tukifahamu kwamba vinafutwa ikiwa tayari vimetudhihirishia misingi imara ya kuendeleza  sekta ya afya kwa kutegemea wataalamu wetu wenyewe ambao tuliowafunza wenyewe.
Historia ya vyuo vyote hivi viwili nimeshaielezea mara kadhaa katika hafla zilizotangulia.  Nimefurahi kuona kuwa  historia   hiyo  leo hapa imeelezwa na kufafanuliwa  vizuri na wenzangu walionitangulia kuzungumza. Kwa hivyo, nakuhimizeni mzingatie historia iliyoelezwa  kwasababu ina  uhusiano wa karibu na maendeleo ya  elimu hapa Zanzibar na maendeleo yenu binafsi; mkifahamu kuwa vyuo hivi vitaendelea kuchangia sana katika kujenga wasifu wenu yaani CV zenu, ingawa vitakuwa  havipo tena.
Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi,
Ni jambo la kufurahisha kuona kuwa wakati tunakaribia kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi  Matukufu ya 1964, Serikali inaendeleza dhamira yake ya kutoa kipaumbele katika kuwapatia wananchi  huduma za afya zilizobora bila ya malipo kwa misingi ile ile iliyowekwa  na Waasisi wa  nchi yetu.
Licha ya kwamba tumekuwa na changamoto kadhaa za kiuchumi, ambazo baadhi ya wakati huzorotesha utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo, Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha utoaji wa  huduma za afya na elimu. Tunafanya hivyo tukitambua wazi kwamba,  maendeleo ya kweli ya nchi yetu yataletwa na nguvu kazi yenye afya bora na elimu. Dhamira ya Serikali ni kuona kuwa wananchi wa Zanzibar  wanakuwa na afya njema, wenye furaha, wakiishi kwa amani huku wakiwa na  elimu, ujuzi  na  maarifa yanayohitajika katika kukabiliana na changamoto na mabadiliko ya karne hii  ya ishirini na moja. Kama ilivyofanywa katika Awamu zilizopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Awamu ya Saba imekuwa ikiwekeza kiwango kikubwa cha fedha  kwa ajili ya  kuimarisha sekta ya Afya na Elimu. 
Wahenga walisema “Mwenye macho haambiwi tazama”. Natarajia kwamba, kwa upande wa hapa Unguja,  sote  tunashuhudia kazi inayoendelea hivi sasa katika Hospitali ya  Mnazi Mmoja. Aidha, sote tunaifahmu   kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita  katika hospitali hiyo kwa lengo la kukamilisha dhamira yetu ya kuifanya kuwa Hospitali ya Rufaa. Leo si siku ya  kuyaeleza kwa undani mambo yote tuliyoyafanya katika hospital hiyo kwa kipindi kilichopita.
Kwa upande wa  Pemba, natarajia kuwa wananchi wengi wanafahamu hatua tuliyofikia sasa katika utekelezaji wa mradi wa kuijenga upya Hospitali ya Abdalla Mzee  iliyoko Mkoani - Pemba. Serikali kwa kushirikiana na wenzetu wa  Serikali ya Jamhuri ya  Watu wa China, katika wiki chache zijazo, tunatarajia kumaliza ujenzi wa Hospitali hiyo na kuifungua kabla ya Sherehe za  Maadhimisho ya  Sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar zitakazofanyika tarahe 12 Januari, 2017.
Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi
Katika  kipindi hiki cha pili cha uongozi wangu, kila siku namuomba  Mwenyezi Mungu atuwezeshe  kutekeleza  kikamilifu dhamira ya Serikali ninayoiongoza  ya  kuifikisha  Hospitali ya Mnazi Mmoja na Hosptali ya Aballa Mzee katika viwango tulichowaahidi wananchi miaka mitano iliyopita.  Namshukuru Mwenyezi Mungu kuona kuwa mipango hiyo inakwenda  vizuri licha ya changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza za kifedha, jambo ambalo haliepukiki katika nchi yoyote inayoendelea.
Vile vile,  tumejidhatiti kuitekeleza dhamira yetu ya kujenga Hospitali ya kisasa ya rufaa katika eneo la  Binguni – Unguja. Tumejidhatiti, katika kuziimarisha hosptali zetu za koteji kuwa hosptali za Mkoa. Hii ni mipango tuliyojidhatiti kuitekeleza kama ilivyobainishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika  Ibara 102 kifungu (c). Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba juhudi hizi za kujenga majengo ya kisasa ya hospital zetu na ya vituo vya afya, zinakwenda sambamba na juhudi za   kuziwekea vifaa vya kisasa pamoja na kusomesha  madaktari, wauguzi  na wataalamu wa kutosha katika sekta ya afya. Serikali imeelekeza nguvu kubwa ya kusomesha wataalamu wa afya na wauguzi katika fani na ngazi mbali mbali ndani na nje ya nchi.
Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi,
Katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na sekta ya afya yenye wataalamu wa kutosha, Serikali imekuwa ikiendeleza mazungumzo mbali mbali na washirika wetu wa maendeleo juu ya kuimarisha mafunzo katika sekta ya afya. Nimekuwa nikizungumza na wageni na mabalozi  wanaonitembelea ofisini kwangu Ikulu juu ya  mipango mbali mbali muhimu yenye lengo la kuiendeleza sekta ya afya. Vile vile, wakati nikifanya ziara za kiserikali nje ya nchi,  mipango ya kuiendeleza sekta ya afya mara nyingi huwa ni miongoni mwa ajenda kuu ninazokuwa nazo katika ziara hizo. Nafarijika kuona kuwa juhudi hizi zimekuwa zikizaa matunda mazuri ambayo wananchi wamekuwa wakiyaona na kufaidika nayo.
Tarehe 03 Oktoba,2016 takriban wiki tatu zilizopita, nilifanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Salvador Antonio Valdes Mesa alipokuwa katika ziara ya siku tatu nchini Tanzania. Niliwaalika mawaziri na viongozi wengine wakuu wa Serikali katika sekta mbali mbali kuja kujumuika nasi ili waweze kuyasikia  maeneo ambayo tumedhamiria kuimarisha mahusiano yetu na mwelekeo wake. Katika mazungumzo yetu, tulijadili juu ya  namna ya kuimarisha  mafunzo ya udaktari , utafiti na kuongeza nafasi za mafunzo katika  kada nyengine muhimu kwa  maendeleo yetu.
Habari njema zaidi, ni kwamba tulikubaliana kuwa Serikali ya Jamhuri ya  Cuba itaharakisha makubaliano yaliyokuwepo ya kutuongezea madaktari wahadhiri na wataalamu wa afya ili waje waongeze nguvu na washirikiane na wataalamu wetu katika utoaji wa mafunzo katika Chuo  Kikuu cha SUZA na katika hospitali zetu. Wakati wowote kuanzia hivi sasa wataalamu hawa wapya kutoka Cuba watafika  hapa nchini.   Vile vile, tulikubaliana kuimarisha mashirikiano katika utafiti na kuanzisha utaratibu wa  kubadilishana wanafunzi.
Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi,
Sote tunakumbuka kwamba madaktari wa Cuba ndio waliotuwekea msingi wa kukianzisha Chuo cha kuwasomesha madaktari wetu hapa Zanzibar.  Uamuzi huu ulifikiwa kwa makubaliano ya pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya Cuba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Jitihada kubwa zilifanyika katika kukianzisha na kukiendeleza chuo hiki.  Wapo waliodhani haitowezekana na wapo waliotubeza.  Lakini imewezekana.  Nina furaha kuona kwamba tangu wakati huo tulipokianzisha chuo chetu hicho hadi hivi sasa madaktari wa Cuba  wanaendelea kutupa mashirikiano makubwa katika utoaji wa taaluma na kuiendeleza sekta ya afya. Napenda nitoe shukurani na pongezi kwa  ndugu zetu wa Cuba kwa kushirikiana nasi kwa kila hali kwa ajili ya kuharakisha maendeleo yetu.  Nawaahidi kwamba  Serikali itafanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuukuza ushirikiano huo.

Kwa hivyo, nakuhimizeni  watendaji wote wa Serikali  mzitumie fursa mbali mbali za mafunzo na kuendeleza tafiti kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Juhudi hizi zitakuwa na tija ikiwa  nyinyi mtazithamini na kuzitumia vizuri.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Mara kadhaa  nimekuwa nikisikia malalamiko kupitia vyombo vya habari; juu ya tabia iliyojengeka kwa  baadhi ya wataalamu mbali mbali wa afya ya kukataa kwenda kufanya kazi Pemba na mashamba.
Aidha,  nimepata taarifa kwamba  kuna baadhi ya Madaktari na Madaktari Wasaidizi ambao hawataki kuishi karibu na maeneo ya kazi kwa kukataa nyumba wanazopewa na badala yake  hufanya safari za kwenda  mjini na kurudi kila siku. Matokeo yake huwa wanachelewa kazini na baadhi ya wakati, huwa hawaonekani  kabisa na wananchi katika vituo vya kazi walivyopangiwa. Hii ni tabia mbaya,  haivumiliki na   ni hatari sana kwa afya za wananchi.  Nauagiza uongozi wa  Wizara ya Afya kuwachukulia hatua kali za kinidhamu kwa dharau  na ukiukwaji mkubwa wa mikataba ya kazi. Msione muhali kwa madaktari na watendaji wa aina hiyo kwani wao wamekiuka misingi muhimu ya kazi zao na wameondosha mapenzi na uadilifu kwa wananchi wanaowahudumia.  Wanaikiuka mikataba walioiridhia kwa kutia saini ya kufanyakazi popote Unguja na Pemba.
Vile vile, naendelea kupata taarifa kwamba wananchi bado wanalalamika  juu  tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa afya kuwatolea maneno wagonjwa na  baadhi ya wakati kuwanyanyapaa. Tabia hiyo, ni kinyume na maadili na mafundisho ya kada hii muhimu ya udaktari na uuguzi. Kwa hivyo, nauagiza tena uongozi wa Wizara ya Afya, uongeze kasi katika kulishughulikia suala hili kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika  kuviendeleza vitendo hivyo.
Ndugu Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi,  
Kabla sijamaliza hotuba yangu,  napenda nizirejee nasaha nilizowapa wenzenu katika mahafali yaliyopita, ambazo zina mambo mengi ya kuzingatia.  Nakunasihini nyote  mwende  mkafanye kazi kwa uzalendo na  kwa moyo mmoja kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu. Kuwa na uzalendo ndio jambo la pekee la kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika kazi zetu.  Uzalendo unaongeza ari na hamasha pamoja na mapenzi ya kuipenda nchi yetu.  Uzalendo ni silaha kubwa ya kuyafikia maendeleo endelevu. Ni lazima mzingatie kuwa Serikali inagharamika sana katika kusomesha madaktari, na wale wote muhimu wanaowahudumia wananchi. Hivi sasa Serikali, wananchi na wazazi wenu wana matumaini makubwa ya kupata huduma zenu kama ni matunda ya jitihada na nyenzo walizokuwa wakiwekeza kwa kipindi chote cha masomo yenu haya na kabla ya haya.  
Lazima  muwe tayari kwenda kufanya kazi popote pale mtakapopangiwa na Serikali kwa kuzingatia sheria ya Utumishi wa Umma na vipengele mbali mbali vya mikataba yenu ya kazi. Mtambue kuwa huduma zenu zinahitajika  sehemu zote, mijini na vijijini, Unguja na Pemba. Daima kumbukeni kuwa  tabia njema, huruma na mapenzi ni vazi la lazima la daktari na muuguzi yoyote duniani. Kwa hivyo, vazi hili mlitaka wenyewe kujivisha kwa kusomea taalum hizi, kwa hivyo, jivisheni vazi hili hata mnapokuwa majumbani. Kuweni tayari  kuwasaidia wananchi hata kama nje ya kazi pale panapohitajika kutoa msaada huo au kuokoa maisha ya watu.  Muwe tayari kuzidi kujiendeleza ili muende sambamba na mabadiliko makubwa na ya kila siku ya sheria na tekenolojia yanayotokezea katika sekta hii ya afya. Nawaahidi kwamba Serikali itaendelea kuimarisha maslahi yenu kwa kadri hali itakavyoruhusu. 
Kabla sijamaliza hotuba yangu, napenda kujibu hoja muhimu zilizotolewa kwenye risala yenu  kama ifuatayo:
1.      Kuhusu  “Scheme of Service”, suala hili litapata ufumbuzi kwa sababu Chuo hiki kinakuwa sehemu ya Skuli ya Tiba na Afya ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, hivyo wafanyakazi wake watapata maslahi sawa na yale yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa mujibu wa stahili zao. 
2.      Kuhusiana na  upungufu wa wafanyakazi wa taaluma mbali mbali,  nauagiza uongozi wa  SUZA uongeze kasi katika kutayarisha  mpango maalum wa kuwaendeleza  wafanyakazi ili waendane na hadhi na sifa za kufundisha katika Chuo Kikuu kwa kuwaendeleza kimasomo ndani na nje ya nchi. 
3.      Kuhusu suala la Chuo kuendelea kutokuwa na hatimiliki ya eneo lake, inashangaza kusikia hivyo, kwani suala hili nimeshalitolea maagizo tangu mahafali yaliyopita. Kadhalika, niliiagiza Kamati ndogo niliyoiunda, kuishughulikia Ripoti ya Wataalamu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoshughulikia vyuo vya utibabu ili ilimalize suala la hatimiliki ya eneo la Chuo.  Natarajia kuwa suala hili lishamalizika.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Namaliza hotuba yangu hii kwa kukupongezeni tena wahitimu nyote mliomaliza masomo yenu pamoja na uongozi wa  chuo hiki kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa makubwa na kupatikana mafanikio makubwa. Pongezi na shukurani maalum ziwaendee walimu kutoka Cuba na Serikali ya Jamhuri ya  Cuba kwa juhudi kubwa mlizofanya katika kuhakikisha kwamba mnatoa taaluma ya afya kwa vijana wetu. Vile vile, natoa shukurani maalum kwa Serikali ya Oman, kwa kuendelea kutuunga mkono katika kutoa elimu ya tiba hapa Zanzibar na kuwa pamoja nasi katika kukiendeleza Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya kwa kipindi chote tangu kilipoanzishwa. Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana nao kwa karibu zaidi katika utoaji wa mafunzo haya kupitia Chuo Kikuu cha Taifa  cha Zanzibar (SUZA) kwa mujibu wa sheria iliotungwa.
Natoa shukurani kwa wale wote walioshiriki katika maandalizi ya mahafali haya na wananchi nyote mliohudhuria. Namuomba Mwenyezi Mungu aizidishie neema na baraka nchi yetu. Nakutakieni nyote safari njema ya kurudi nyumbani.
Ahsanteni kwa kunisikiliza. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.