Habari za Punde

Kijakazi Abdalla/Habari Maelezo                28/10/2016

Ofisi ya mtakwimuu mkuu wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na ofisi ya taifa ya takwimu zinakusudia kufanya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi nchi nzima kwa mwaka 2016.

Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa utafiti huo kwa Zanzibar fahima Mohamed Issa amesema utafanyika katika maeneo ya kuhesabia watu yapatayo 26 Unguja na Pemba na jumla ya kaya mia nane zitahojiwa.

Amesema utafiti huo una lengo la kuangalia hali ya maambukizi ya ukimwi, kiwango cha maambukizi mapya,wingi wa kinga ya mwili kupambana na virusi vya ukimwi, magonjwa ya kaswende na homa ya ini.

Amefahamisha kuwa utafiti huo tayari umeshaanza katika mikoa mitatu ya Tanzania bara ikiwemo Dodoma,Singida na Manyara ambapo kwa Zanzibar unatarajiwa kuanza baada ya wiki mbili zijazo.

Amesema matokeo ya utafiti huo ni muhimu katika sekta ya afya  na utatoa viashiria mbali mbali vitakavyotumika katika utekelezaji wa mipango endelevu ya maendeleo.

Ametoa wito kwa wananchi ambao kaya zao zimechaguliwa kutoa mashirikiano na wataalamu wa zoezi hilo wakati wanapokwenda kukusanya takwimu hizo.
                 
 Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.