Habari za Punde

Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Wakabidhi Vifaa vya Ujenzi wa Skuli ya Matetema.


Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Vifaa vya Ujenzi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Skuli ya Msingi Matetema Nd. Ali Sali Ali ili kuendeleza ujenzi wa jengo lao jipya litakalopunguza msongamano wa wanafunzi skulini hapo.
Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid na Kulia ya Balozi Seif ni Afisa wa Elimu Wilaya ya Kaskazini “B” Mwalimu Juma Omar Haji.


Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Matetema Mwalimu Ali Salim Ali akithibitisha kupokea msaada wa Vifaa kutoka kwa Viongozi wa Jimbo la Mahonda.Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahatri Ali Abeid akiihimiza Kamati ya  Skuli, Walimu na Wazazi kuendelea kujitokeza katika ujenzi wa Taifa wa miradi wanayoianzisha kwenye hafla ya kukabidhi vifaa vya ujenzi kwa skuli ya Msingi ya Matetema.

Afisa wa Elimu Wilaya ya Kaskazini “B” Mwalimu Juma Omar Haji.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis OMPR. 

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema Umoja wa kuunganisha nguvu za Wananchi katika kuimarisha miradi yao ya  maendeleo inastahiki kusimamiwa kwa pamoja kati ya Viongozi na Wananchi wenyewe Majimboni ikiwa ni njia sahihi inayosaidia kuondosha au kupunguza kabisa kero zinazowakabili.

Alisema ipo mifano hai inayoonekana katika baadhi ya Majimbo kuhusu mshikamano unaoendelezwa na pande hizo ambao huleta mafanikio makubwa katika kusimamia maendeleo na miradi ya kijamii Majimboni.

Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na Mbunge wa Jimbo lao la Mahonda alieleza hayo wakati akizungumza na waalimu, wanafunzi na baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Matetema kwenye hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya Ujenzi kwa ajili ya uendelezaji wa Jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Kijiji hicho linalojengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe.

Vifaa hivyo ni pamoja na Saruji Mifuko 80, nondo 28, Matofali 800, mchanga Gari mbili pamoja na fedha za mafundi na vibarua wake, vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 4,100,000/-.

Balozi Seif alisema jitihada za wana jamii katika kuanzisha, kuendeleza na hatimae kukamilisha miradi waliyoianzisha zinahitajika ili kuwapa nguvu viongozi wao kuongeza nguvu za uwezeshaji zitakazoleta faraja kwa wananchi hao.

Balozi Seif aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Matetema kwa juhudi kubwa walizochukuwa katika kuongeza majengo ya Skuli yao kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu watoto wao wa kufuata elimu masafa marefu katika skuli ya Kitope.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliushauri Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Matetema kulielewa eneo zima la Skuli hiyo ili kusaidia udhibiti wa uvamizi wa maeneo ya jamii unaofanywa na baadhi ya wapinga maendeleo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid aliwaeleza wananchi na wanataaluma hao kwamba ziara zinazofanywa na Viongozi wa Jimbo hilo zina lengo la kuunga jitihada zao walizoanzisha za kusimamia miradi yao ya maendeleo.

Mh. Bahati alisema bado wananchi kwa kushirikiana na Viongozi wao watapaswa kusimamia sekta ya Elimu ambayo ndio muhimili wa maendeleo wa Taifa lolote lile Duniani.

Mapema Mwalimu Mkuu msaidizi wa Skuli ya Msingi ya Matetema Mwalimu Ali Salim Ali alisema skuli hiyo kwa sasa inalazimika kujenga madarasa 10   ili kukidhi mahitaji halisi ya wanafunzi 361 waliopo hivi sasa skulini hapo.

Mwalimu Ali alisema kwa sasa walimu wa skuli hiyo wanalazimika kufundisha wanafunzi wasiopungua 65 kwa darasa moja changamoto ambayo imelazimisha hata lile darasa la wanafunzi wa skuli ya maandalizi kutumiwa na wanafunzi wa skuli ya msingi.

“ Tunalazimika kuwachanganya wanafunzi wetu wale wa maandalizi na msingi tatizo ambalo huwaletea usumbufu walimu wetu katika ufundishaji wa wanafunzi hao tofauti “ Alisema Mwalimu Ali Salim.

Msaidizi Mwalimu Mkuu huyo wa Skuli ya Msingi ya Matetema aliuomba Uongozi wa Jimbo kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto kubwa ya ukosefu wa udhibiti wa maadili kwa wanafunzi wa skuli hiyo.

Alisema Changamoto hiyo kwa sasa imekuwa kero kubwa kwa walimu wa skuli hiyo ambayo baadhi ya wakati wanafunzi hufikia hatua ya kutishia maisha ya walimu hao ambao takriban wote ni wanawake. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.