Habari za Punde

Wawakilishi Wawataka Watumishi Kuitumikia Serikali.


Na Mwandishi Wetu.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamewalalamikia baadhi ya watumishi wa Serikali waliopewa dhamana ya kuitumikia Serikali badala yake kuweka mbele maslahi yao binafsi kwenye miradi ya maendeleo, hali waliyoeleza inakwamisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati.
Waliyasema hayo huko ukumbi wa mikutano wa Z-Ocean, Kihinani wakati wakijadili kuhusu mradi wa ujenzi wa kijiji cha utalii Matemwe, mkoa wa Kaskazini Unguja ambao umezusha mvutano mkubwa baina wa mwekezaji na wananchi wa kijiji hicho.

Walisema kucheleweshwa kwa miradi ya maendeleo nchini kunakwambisha 
shughuli za maendeleo sambamba na kuikosesha serikali mapato yake kutoka kwa wawekezaji.

Aidha waliilalamikia Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA) kwa kuchelewa kwao kutoa vibali vya ujenzi kwa baadhi ya wawekezaji nchini, jambo walilolieleza Wawakilishi hao kuwa linarudisha nyuma juhudi za wawekezaji na serikali kwa ujumla.

Wajumbe hao pia walimlalamikia wakala wa mradi wa "Penny Royal" unaotarajiwa kuanza karibuni katika kijiji cha Matemwe, kwa kuchukua kiasi kikubwa cha fedha zilizotolewa kwaajili ya kuwalipa fidia wananchi wa kijiji hicho na badala yake wamezitumia kwa maslahi yao binafsi.

"Ni aibu na fedheha kwa mwekezaji kupigia magoti wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kulalamikia ubadhirifu wa uwekezaji" alisema Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma wakati akichangia mjadala wa ucheleweshwaji wa ujenzi wa kijiji cha utalii Matemwe "Penny Royal" walioulalamikia kucheleweshwa na baadhi ya watendaji wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kijiji cha Matemwe kinakabiliwa na umasikini wa hali ya juu, hivyo alieleza kuwa ujenzi wa kijiji hicho ni mkombozi wa wananchi wanyonge kijijini hapo.

Alisema mradi wa "Penny Royal" katika kijiji cha Matemwe ni mradi mkubwa kuwekezwa katika historia ya visiwa vya Zanzibar kwani unamiradi mingi ndani yake ikiwemo miundombinu ya barabara, maji safi, umeme, ujenzi wa makazi ya wanakijiji, uwanja wa ndege pamoja skuli na hospitali za kimataifa, suala alilolieleza kuwa litatoa nafasi nyingi za ajira kwa wanakijiji cha Matemwe na maeneo jirani ya Mkoa wa Kaskazini.

"Ndugu zetu ZIPA msione kama mnasemwa vibaya kwenye hili, bali tunatekeleza malengo ya rais ya kuwaletea maendeleo wananchi wetu" alisema.

Nae Waziri asiekuwa na Wizara maalum ambae pia ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Said Soud alisema ni jukumu lao kutetea haki na maslahi ya wananchi ili kuwapa imani kwa serikali yao.

Alisema serikali haijakwamisha haki za wananchi bali watu wachache ndio wanaoitia dosari serikali katika utendaji  wake.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na BLM katika kutatua mgogoro uliopo baina ya mwekezaji wa "Penny Royal" na wanakijijiji hicho cha Matemwe Mhe. Soud alisema imeundwa kamati maalumu ya kukabiliana na changamoto za mradi huo kisha kumfikishia rais hatua iliyofikiwa.

Alisema rais wa Zanzibar ni mweledi wa maendeleo nakuongeza kuwa Serikali ya SMZ iko makini sana katika kukabiliana na watendaji wadanganyifu wa miradi ya maendeleo.

"Uwekezaji tunaupenda na wananchi tunawapenda pia kwani  wao ndio walioiweka dola madarakani" alisema

Akizungumzia kuhusu kufeli kwa baadhi ya miradi ya maendeleo nchini, Mwakilishi Hassan Khamis Diaspora (Welezo) alisema miradi mingi inashindwa kuendelea kutokana na kuwepo kwa watumishi wa chache serikalini wanaoelekeza mbele maslahi yao binafsi.

Nae Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Juma Haji alisema mradi wa "Penny Royal" uliwahi kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwaajili ya kulipwa fidia wananchi wa kijiji cha Matemwe badala yake fedha hizo zililiwa na watu wachache waliopewa dhamana ya kusimamia.

Hivyo aliiomba serikali kusimamia tatizo liliopo ili kulipatia ufumbuzi kwa lengo la kuendeleza mradi huo na kuepusha migogoro baina ya wenyeji wa Matemwe na mwekezaji wao.

Kwaupande wake Ofisa mdhamini Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni mratibu wa polisi mkoani humo, Ali Abdalla Kitole alieleza mbali ya serikali kulifanikisha suala la ulipwaji wa fidia kwa wananchi wa jijini cha Matemwe lakini bado mradi unakabiliwa na changamoto kwa wenyeji wa kijiji hicho kwa kumlalamikia mwekezaji huyo kwamba hata kazi ndogo ndogo mathalani za kusogeza mawe na zinazoshabihiana na hizo pia hutumia waajiri wake wakigeni au mashine badala kuwatumia wazawa ili kupunguza tatizo la ajira linalowakabili.

Naibu wa Wizara ya Ardhi, Maji Nishati na Mazingira ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Matemwe aliitaka kamati ya wilaya iliyoteuliwa na serikali kushughuli mgogoro huo pamoja na wadau wote wanaohusika katika uwekezaji huo kukaa pamoja na kujadili jinsi ya kupata suluhu ya mgogoro huo.

Nae Mwakilishi wa mradi huo wa "Penny Royal", Salim Muhammed Said aliiomba serikali kuingilia kati mgogoro huo ili kuwabaini wanaostahiki kulipwa fidia zao kwani alieleza walitoa fedha nyingi kuwalipa wananchi na kadri siku zinavyoendelea wanaibuka wepya na kudai fidia zao jambo aliloeleza kuwa palipita udanganyifu katika mgao wa fidia hizo.


Kampuni ya "Penny Royal" iliyopo chini ya uongozi wa Brian Thomas, kupitia mradi wao "Amber Reasort" wenye lengo la kujenga kijiji cha utalii kijijini Matemwe mkoa wa Kaskazini Unguja, umekumbwa na changamoto ya mgogoro wa ardhi baina yake na wenyeji wa kijiji hicho, jambo linalokwamisha juhudi za ujenzi wa mradi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.