Maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi
(TKU)
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (The Mwalimu Nyerere
Foundation) zinaujulisha umma kwamba tarehe
21 Oktoba, 2016 kutakuwa na Maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tume
ya Kudumu ya Uchunguzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu matumizi mabaya ya
madaraka, yatakayofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa saba mchana.
Maadhimisho hayo
yatakayowashirikisha viongozi, watu mashuhuri na wawakilishi kutoka taasisi
mbalimbali ndani na nje ya nchi, yatahusisha Kongamano litakalojadili mada
mbalimbali kuhusu utawala bora na utawala wa sheria nchini.
Mgeni rasmi katika Maadhimisho
hayo atakuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.
Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) atakaye mwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Tume ya Kudumu ya Uchunguzi
ilikuwa taasisi ya kwanza ya ‘Ombudsman’ kuanzishwa barani Afrika mwaka 1966. Kauli
mbiu ya Maadhimisho ni: “Utawala wa
Sheria ndiyo Msingi Mkuu wa Utawala Bora”
(Rule of law is the foundation for good governance).
Aidha, Maadhimisho haya yanalenga
kuangalia uzoefu tulioupata na kujifunza kutokana na mafanikio/mapungufu na
changamoto zilizojitokeza katika kipindi hicho, kwa lengo la kuangalia hali
ilivyo hivi sasa; ikiwa ni tathimini ya kuona iwapo TKU ilifikia matarajio ya
wananchi au la; na kuona jinsi ambavyo THBUB imeendelea na majukumu ya TKU tangu
mwaka 2001 hadi sasa.
Pamoja na Kongamano litakalofanyika,
Maadhimisho haya yatatumika kutambua
michango ya watu mbalimbali katika kuinua masuala ya utawala bora nchini.
Kwa
upande wa Kongamano, miongoni mwa mada zitakazowasilishwa ni pamoja na: Chimbuko,
changamoto na mafanikio ya TKU: 1966 – 2001 (Origin, challenges and successes
of PCE: 1966 – 2001), itakayotolewa na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Gad Mjemmas, ambaye pia aliwahi kufanyakazi TKU, kama Mwanasheria
(Legal Officer) na baadaye kama Katibu Mtendaji wa THBUB.
Mada
nyingine ni: Uzoefu wa Afrika wa Taasisi za ‘Ombudsman’ (African Experiences with
Ombudsman Institutions), itakayowasilishwa na Mwakilishi kutoka Jumuiya
ya taasisi za Uchunguzi wa Malalamiko ya Wananchi na Wapatanishi Afrika
(African Ombudsman and Mediators Association – AOMA).
Prof.
Paramagamba Kabudi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam atawasilisha mada itakayoangalia
“Kutoka
TKU hadi THBUB: Tathimini Linganifu ya Changamoto zilizopo na Matarajio” (From
PCE to CHRAGG: Comparative Analysis of Contemporary Challenges and Expectations.
Aidha,
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania, Mhe. Jaji mstaafu Damian Lubuva atatoa
hotuba itakayoeleza uzoefu wake na TKU ukizingatia kuwa alifanyakazi kama
Mwanasheria (Legal Officer) wa TKU na baadaye kushika nyadhifa muhimu hapa
nchini.
Hivyo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
inapenda kukumbushia umuhimu wa kuzingatia utawala wa sheria, na kwa kufanya
hivyo tutakuwa tunamuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na
kudumisha mawazo yake ambayo ndiyo ulikuwa msingi wa kuanzishwa kwa Tume ya
Kudumu ya Uchunguzi.
Nimalize kwa kuwashukuru ndugu
zangu waandishi wa habari kwa ushirikiano wenu na kwa kuitikia wito wetu na kuhudhuria
mkutano wa leo.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
“Utawala wa Sheria ndiyo Msingi Mkuu
wa Utawala Bora”.
(SIGNED)
Iddi Ramadhani Mapuri
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA
BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
+255 784 329 900; 714 000 341; 784
345 352
No comments:
Post a Comment