Na Haji Nassor, Pemba
WAJUMBE wa baraza la wawakilishi,
wameshauriwa kujenga utamaduni wa kutembelea hospitali na vituo vya afya kila
muda mfupi, ili kubaini changamoto zilizomo na kuisaida serikali kuzitatua.
Rai
hiyo imetolewa na mjumbe wa baraza la wawakilishi nafasi za vijana mkoa wa
kusini Pemba, Mhe: Zulfa Mmaka Omar, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari, mara baada ya kushiriki usafi katika hospitali ya Chakechake na
kutembelea wodi ya watoto na kuwapa zawadi.
Alisema
wajumbe wa baraza hilo, kama wakijenga utamaduni wa kuvitembelea vituo hivyo,
wanaweza kukumbana na changamoto kadhaa na kisha kuzitatua.
Alisema suala la huduma za afya kwa jamii, wala halihusiana na chama chochote, bali ni
la wananchi wote wakiwemo hao wawakilishi, ambao wanaweza kuishauri serikali
wakati wowote.
Mhe:
Zulfa alisema pamoja na wizara ya afya kujitahidi katika kutoa huduma kwa
wananchi na kwa wakati, lakini changamoto kubwa inayojitokeza, ni ongezeko la
idadi ya watu kila siku.
“Mimi
naona huduma zipo vizuri, lakini na sisi wajumbe wa baraza la wawakilishi,
tunayo nafasi ya kuisaidia serikali yetu, kwa kutembelea na kujiona kwa macho
yetu mapungufu yaliomo’’,alifafanua.
Akizungumzia
zoezi la usafi alioufanya kwa kushirikiana na vijana, alisema waliamua kutokana
na jengo hilo kutumiwa na kila mmoja.
“Hatukupenda
kufanya usafi kwenye majengo ya chama wala ofisi na taasisi za serikali, maana
humo wamo wahusika tu, lakini hapa hospitali kila mmoja anafika kufuata huduma’’,alifafanua.
Aidha
alisema waliamua kufanya usafi huo, ili kuunga mkono juhudi za viongozi wa nchi,
ambao wamekuwa wakihamasisha usafi wa mazingira katika maeneo kadhaa.
Akizungumza
mara baada ya usafi huo, mkuu wa bustani wa hospitali hiyo Ali Omar Ali, alisema hatua ya kushirikiana
katika usafi huo, umempa ahuweni kwa vile pana upungufu wa wafanyakazi katika
sekta hiyo.
Nae
Mwenyekiti wa Vijana shehia ya Wara alieungana na mwakilishi huyo Halib Bedui Khamis, alisema kwa sasa wanafikiria
kila mwisho wa mwezi, kufanya usafi katika hospitali hiyo.
“Mwakilishi
wetu wa vijana mkoa wa kusini Pemba, ametuamsha kwamba usafi ni lazima, sasa na
sisi tunafikiria kukutana kila mwezi ili kufanya usafi’’,alifafanua.
Nae
daktari dhamana wa hospitali hiyo Ali Habib, alimpongeza mwakilishi huyo
kuendeleza sera ya usafi na kuamua kuingia hospitalini hapo.
“Mimi
kwa niaba ya uongozi na wafanyakazi wa hospitali hii ya Chakechake, niseme
tumefarajika sana kupata kikundi cha vijana wakiongozwa na Mwakilishi kufanya
usafi, na hii ni sadaka kubwa’’,alifafanua.
Nae
mwakilishi wa Jimbo la Chakechake Mhe: Suleiman Zaharan alisema wataendelea
kufanya usafi na kusaidia dawa kwenye hospitali mbali mbali, ili kuunga mkono
juhudi za serikali.
Mwakilishi
huyo wa nafasi za vijana mkoa wa kusini Pemba, pamoja na vijana na wananchi
wengine walifanya usafi nje za wodi za watoto, wagonjwa wa TB na kukata majani
hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment